Vodacom, UNDP, Funguo, washirikiana kuandaa Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025

February 5, 2025 6:12 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Inatarajiwa kufanyika kwa siku tano kuanzia Mei 12 hadi 16, 2025

Dar es Salaam. Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa Tanzania(UNDP), kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania na Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), wametangaza kushirikiana kuandaa maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu wakikusudia kuimarisha ubunifu na kuendesha mabadiliko ya kidijitali.

Maaadhimisho ya wiki hiyo yatayofafanyika kuanzia Mei12 hadi  Mei 16, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam yatakwenda sambamba na Mkutano wa Future Ready wa Vodacom.

Maadhimisho hayo ni fursa ya kuongeza ujuzi wa namna ya kutumia majukwaa ya kidijitali pamoja na ubunifu kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana ikiwemo ukosefu wa ajira na mitaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Phillip Besiimire amebainisha kuwa ushirikiano huo unaleta mabadiliko katika sekta ya ubunifu nchini Tanzania kwa kuunganisha wabunifu na wajasiriamali wa kimataifa kutoka sehemu mbalimbali za dunia. 

“Kwa kuleta mitazamo na taaluma za kimataifa kwenye mijadala hii, tunalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mabadiliko ya kidijitali, sambamba na kuanzisha mifumo ya ikolojia ya ubunifu inayoongozwa na vijana,” amesema Besiimire.

Besiimire ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia kwa lengo la kuboresha maisha yanayoongozwa na kampuni yake  ndio yanayounda msingi wa ushirikiano huo unaoendeshwa na maono ya kuwawezesha watanzania kuendelea kupitia uchumi wa kidijitali ulioendelevu na jumuishi.

Kwa kushiriki katika matukio hayo vijana  wa Tanzania wanaweza kufungua milango kwa fursa mpya za kujikuza kiujuzi, kujenga mitandao na wataalamu wa kimataifa, na kujifunza jinsi ya kutumia ubunifu na teknolojia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.

Kwa mwaka 2025 maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu yataongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Kubadilisha hatma ya miji: Usasa, Uendelevu na Jumuishi”, ambayo inadokeza umuhimu wa kuibadili miji ya Tanzania kwa ajili ya kutatua changamoto zinazotokana na ukuaji wa kasi, mabadiliko ya tabia nchi na mabadiliko ya teknolojia.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara akieleza faida za Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 Picha |Funguo

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara amesema kupitia ushirikiano huo wanalenga kuwainua Watanzania, hasa vijana na wanawake, kuwa chachu ya mabadiliko chanya. 

“Wiki ya Ubunifu Tanzania 2025 (IWTz2025) itaonyesha ari ya ubunifu Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa, kuvutia uhamasishaji na ushirikiano kupitia na mifumo iliyofanikiwa duniani,” amesema Komatsubara.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo na Uhamisho wa Teknolojia kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Athumani Ngumia amesema taasisi yake itaendelea kuwaunganisha wadau kwa lengo la kuchochea utafiti, teknolojia na ubunifu ambao unaendana na vipaumbele vya nchi katika maendeleo na dira ya mwaka 2050.

Wiki ya ubunifu 2025 na mkutano wa Future Ready Summit inatarajia kuwaleta pamoja washiriki, wazungumzaji na wabunifu kutoka Tanzania, Afrika na sehemu mbalimbali duniani na kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana maarifa, kuendeleza ushirikiano wenye tija na kuhamasisha mawazo yenye kuleta mabadiliko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks