BoT yabakiza riba ya benki kuu 6% robo ya kwanza 2025
- Kamati ya fedha inatarajia kuwa uchumi utaendelea kuwa imara Tanzania Bara na Zanzibar
Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imeamua kiwango cha riba ya benki kuu kuendelea kuwa asilimia sita katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Hii ni mara ya tatu kamati hiyo imeendelea kubakiza kiwango hicho katika asilimia 6. Mara ya kwanza kiwango hicho kilianza kutumika robo ya pili ya mwaka 2024 baada ya kupanda kidogo kutoka asilimia 5.5 kilichoanza robo ya kwanza mwaka 2024 wakati mfumo mpya wa sera ya fedha ulipoanza kutumika rasmi.
Uamuzi huo wa kamati hiyo ya fedha iliyokutana jana utafanya kiwango cha asilimia 6 kitumike kwa robo nne za mwaka sawa na mwaka mmoja.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa uamuzi wa kamati kutobadili Riba ya Benki Kuu (CBR) unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia tano.
“Uamuzi huo unalenga kuwa na utulivu wa thamani ya Shilingi dhidi ya fedha za kigeni ili kuendelea kuwa na mfumuko wa bei mdogo. Utulivu wa thamani ya Shilingi dhidi ya fedha za kigeni utachangia jitihada za kuwafanya wananchi kutofanya miamala yao kwa fedha za kigeni,” amesema Tutuba leo.
Bosi huyo wa BoT amesema kuna viashiria chanya vya ukuaji wa uchumi katika ngazi ya dunia na ndani ya nchi ambavyo kwa sehemu kubwa ni mwendelezo wa ukuaji uliorekodiwa katika robo ya mwisho ya mwaka 2024.
Katika mwaka 2024, Tutuba amesema uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024 na unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya mwisho ya mwaka.
Huko visiwani Zanzibar, Tutuba anasema wanatarajia uchumi utakua kwa kasi zaidi kwa asilimia 6 katika robo ya tatu na asilimia 6.8 katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2024.
Katika kudhibiti mfumuko wa bei, amesema wanatarajia mfumuko wa bei utaendelea kuwa tulivu katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 ukibakia katika viwango vya kati ya asilimia 3.1 na asilimia 4.
Mfumuko wa bei nchini uliendelea kuwa chini ya asilimia 4 mwaka jana hadi Novemba 2024 ukidumu zaidi katika kiwango cha asilimia 3 kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Matarajio ya kuimarika kwa mfumuko wa bei yanatokana na uwepo wa chakula cha kutosha, utulivu wa thamani ya Shilingi dhidi ya fedha za kigeni, umeme wa uhakika na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la la dunia hususan mafuta ghafi.
Tutuba amesema thamani ya Shilingi inatarajiwa kuwa imara katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na uwepo wa ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya mwisho ya mwaka jana kutokana na baadhi ya mataifa kushusha riba na kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi hususan dhahabu, utalii, korosho na tumbaku.
Thamani ya Shilingi iliimarika zaidi miezi ya Novemba na Desemba mwaka jana hadi kufikia kiwango cha Sh2,290 kwa Dola ya Marekani, baada ya kuwa juu ya Sh2,500 kwa Dola moja ya Marekani kwa zaidi ya robo tatu zote za mwaka 2024 jambo lililochochea kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.