Takukuru Mwanza yaonya rushwa kipindi cha uchaguzi
- Yasema wataotoa na kupokea rushwa wote watachuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imewaonya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu kuacha tabia ya kutoa rushwa kwa wananchi kuwashawishi ili wawachague.
Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Idirisa Kisaka aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Novemba 21,2024 amesema taasisi hiyo imejipanga kufuatilia vitendo vyote vya rushwa katika uchaguzi kabla, wakati na baada ya uchaguzi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
“Mara nyingi wagombea wasiokuwa waaminifu wanatumia nafasi hii kuwashawishi wananchi kwa kuwapatia chochote ili wawachague, na pia kuna baadhi ya wananchi ambao nao wanatumia kishawishi kwa wagombea ili wawapatie chochote wote kwa pamoja tunawafuatilia,” amesema Kisaka.
Kisaka ametoa angalizo kwa wananchi kuacha tabia hiyo na kwamba wawachague viongozi ambao ni waadilifu na watoe taarifa pale ambapo wataona kuna viashiria vya wagombea kutoa rushwa.
Pamoja na kuwachukulia hatua Takukuru imejipanga kutoa elimu kwa makundi mbalimbali juu ya madhara ya rushwa na makosa yatokano na rushwa katika uchaguzi huo.
Aidha, Takukuru ifanya uchambuzi wa mifumo, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuchunguza makosa ya rushwa kwa mujibu wa sheria.