Waliopoteza maisha katika ajali ya kuporomoka kwa jengo Kariakoo wafikia 20

November 20, 2024 6:34 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Samia amesema ajali hiyo ni funzo kwa Serikali na jamii nzima katika kuangalia hali ya usalama wa majengo.
  • Aagiza viongozi wa Serikali kuhakikisha ajali hiyo haijirudii tena na kuleta maafa kwa jamii.

Arusha. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Idadi ya Watanzania waliofariki katika ajali ya kuporomoka kwa jengo Kariakoo imefikia 20 huku majeruhi waliobakia hospitali kwa ajili ya matibabu wakiwa watatu.

Rais Samia ametoa takwimu hizo wakati akizungumza na wananchi pamoja na wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam leo Novemba 20, 2024 ambapo amesema tukio hilo limetoa funzo kwa Serikali na jamii nzima katika kuangalia hali ya usalama wa majengo.

“Niseme kwamba tukio hili limetupa ujumbe mkubwa wa kuangalia usalama wa majengo yetu katika eneo la Kariakoo, ukiliangalia jengo lenyewe lilivyojengwa kuta zake na nondo, jengo halikusimamiwa vizuri,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo wa nchi amefika katika eneo ilipotokea ajali ya kuporomoka kwa jengo Kariakoo jijini Dar es Salaam leo kwa mara ya kwanza akitokea nchini Brazil ambapo alihudhuria mkutano wa nchi tajiri zaidi duniani G20 uliomalizika Novemba 19 mwaka huu.

Baada ya kujionea hali halisi ya eneo hilo Rais Samia ameagiza viongozi wa Serikali kuhakikisha tukio hilo halijirudii tena na kuleta maafa kwa jamii.

“Niwaombe watu wote tunaohusika kwenye mambo haya, Serikali kuu, halmashauri, viongozi wa Serikali za mitaa, asasi za kiraia na wananchi wote kwa ujumla, tuseme kwa pamoja kwamba matukio ya namna hii yasijirudie kwa sababu tukio hili ni huzuni kubwa sana kwa Taifa letu,” ameongeza Rais Samia.

Itakumbukwa kuwa Novemba 17 mwaka huu Rais Samia alimuagiza Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kuongoza timu ya ukaguzi wa majengo kukagua eneo lote la Kariakoo na kutoa hali ya taarifa kamili ya hali ya majengo katika eneo hilo mara baada ya zoezi la uokoaji kukamilika.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akikagua eneo la maafa ya ajali ya kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo, Jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ililenga kutathmini hali ya majengo katika eneo hilo linalotajwa kuwa kitovu cha biashara baada ya kuwepo kwa malalamiko juu ya uchakavu wa majengo hayo huku baadhi ya wamiliki wakibadili matumizi kutoka kwenye majengo ya makazi hadi kuwa majengo ya biashara.

Aidha, Rais Samia amewaambia wafanyabiashara walioko mbali na eneo lililopata maafa kuendelea na biashara, huku wale walio katika eneo la hatari kufunga ili wataalam wa uokoaji waendelee na zoezi la kufumua jengo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks