Fahamu aina na faida za kula viazi vitamu
- Ni pamoja na kurekebisha mzunguko wa damu na kiwango cha sukari mwilini.
- Kiazi chenye uzito wa gramu 200 huwa na vitamini A mara tatu ya kiasi kinachopendekezwa kula kwa siku.
Dar es Salaam.Viazi vitamu ni miongoni mwa mazao muhimu yanayotumika kama chanzo kikuu cha chakula katika maeneo mengi nchini.
Zao hili ni maarufu kutokana na uwezo wake wa kuvumilia ukame na hivyo husaidia katika kupunguza njaa katika maeneo hayo.
Kiasili viazi vitamu vimetokea Amerika ya kati na ya kusini ingawa nchini Tanzania zao hili hulimwa zaidi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na Ruvuma.
Viazi hivi hutumika kama chakula na hutayarishwa kwa aina yake kulingana na asili ya kabila au eneo husika, mathalan jamii ya wasukuma wanaotokea mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Geita huviita viazi hivyo vilivyochemshwa na kukaushwa juani matobolwa na huweza kutumiwa kwa muda mrefu zaidi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, kuna makundi matatu ya ya viazi vitamu ambayo ni viazi vitamu vya rangi ya chungwa (Orange-fleshed),viazi vitamu vya rangi ya zambarau (Purple-fleshed) na viazi vitamu vya rangi nyeupe (White-fleshed).
Viazi vitamu hivi hupatikana kwa wingi na hutumika katika maandalizi mengi ya vyakula vya chumvi ili kuongezea ladha zaidi.Picha /The Pioneeer Woman.
Viazi vitamu vya rangi ya chungwa mara nyingi huitwa kiazi lishe na hii ni kwa sababu ukikikata kina rangi ya chungwa ndani.
Rangi hii ya chungwa inatokana na kirutubishi aina ya beta-karotini ambayo ni moja ya vitamini A na kadiri rangi inavyokuwa imeiva na kiasi cha beta-karotini kinakuwa nyingi.
Viazi vya rangi ya chungwa vina kiasi kikubwa cha vitamini A ukilinganisha na viazi vitamu vingine. Ukiachana na viazi vitamu vyakula vingine venye rangi ya chungwa ni pamoja na karoti, maboga, machungwa, papai na embe.
Viazi hivi siyo kwamba ni vitamu tu, vilevile ni vizuri kwa afya kwani vina vitamini A na virutubishi vingine ambavyo kwa ujumla husaidia kuondoa utapiamlo na upungufu wa vitamini A kama vikitumiwa ipasavyo.
Viazi vitamu vya rangi nyeupe vina utajiri wa nyuzinyuzi, vitamini na madini ingawa havipatikani kwa wingi kama vile vya rangi ya machungwa. Picha/Udip Fresh.
Virutubisho vingine ni wanga, nyuzi nyuzi, anti-oksidanti, vitamini C, vitamini B1, B3, B2, B5, B6, vitamini E, vitamini K, potasi, manganizi, protini, kalisi, sodiamu, madini chuma na foleti ambavyo vyote ni muhimu kwa afya ya mtuamiaji.
Kwa mujibu wa wa chapisho la elimu ya lishe, umuhimu na Matumizi ya Viazi vitamu lililochapishwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), gramu 125 za kiazi lishe kilichochomwa au kuokwa hutoa vitamini A inayotakiwa na watoto wenye umri wa chini ya miaka 5, watoto wenye umri wa kwenda shule na kina mama wajawazito na wanyonyeshao.
Umuhimu wa viazi vitamu kwa afya
Faida kuu za viazi vitamu katika afya ni pamoja na kusaidia kujikinga na magonjwa ya moyo, kiharusi, na saratani, kurekebisha mzunguko wa damu kulingana na madini yaliyomo, kurekebisha kiwango cha sukari mwilini kulingana na virutubishi vya karotenoid ambavyo havina rehemu pamoja na kuzuia uyabisi wa tumbo kwa sababu ya nyuzinyuzi zilizomo katika viazi hivyo.
“ Wanga wake hupandisha kiasi cha sukari polepole ukilinganisha na wanga unaotokana na vyakula vingine kwa hivyo ni chakula kizuri kwa watu wenye kisukari. (Hii hupelekea kutumika kwa sukari nyingi wakati wa usagaji wa viazi tumboni ukilinganisha na sukari utakayoipata kwenye kiazi)…
…Viazi vitamu vina beta-karotini, vitamini C, na E ambazo ni anti-oksi, pamoja na faida hizo pia wanga wake hupandisha kiasi cha sukari polepole ukilinganisha na wanga unaotokana na vyakula vingine kwa hivyo ni chakula kizuri kwa watu wenye kisukari,” Wizara ya Kilimo.
Aidha, kiazi chenye uzito wa gramu 200 huwa na vitamini A mara tatu ya kiasi kinachopendekezwa kula kwa siku kwa mtu mmoja, huku vitamini hivyo vikiwa muhimu katika afya ya macho, ngozi, utumbo, kukua kwa mifupa, Pia husaidia mfumo wa uzazi, mfumo wa upumuaji na ukuaji bora, kuongeza kinga ya mwili, kusaidia watu wasizeeke haraka.
Picha hii inaonyesha viazi vitamu vya zambarau ambavyo pia vina nyama yenye rangi ya zambarau iliyokolea, mbali na hili, ngozi yake ya nje, umbo, na mwonekano kwa ujumla vinafanana kwa kiasi kikubwa na viazi vitamu vyenye rangi ya machungwa. Picha/Nutrition Advance.
Kwa upande wa tovuti ya Heathline gramu 200 za viazi vitamu vilivyookwa na ngozi vinaweza kutoa, kalori 180, wanga gramu 41,protini gramu 4,mafuta gram 0.3, nyuzinyuzi gramu 6.6,Vitamini A asilimia 213 ya thamani ya Kila Siku (DV), vitamini C asilimia 44 ya DV, manganizi 43% ya DV, shaba asilimia 36 ya DV, asidi ya Pantothenic asilimia 35 ya DV, vitamini B6 asilimia 34 ya DV, Potasiamu asilimia 20 ya DV pamoja na Niacini asilimia 19 ya DV.
“Ni muhimu kwa watu wote kuhakikisha kuwa wanatumia viazi kulingana na kuwa na asilimia kubwa vya virutubisho vya vitamini A na gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine vya vitamini A, kama mayai, maziwa, samaki na maini,” Healthline.
Vyanzo vingine vya vitamini A ni mapapai, maboga, koroti, parachichi na pilipili nyekundu ingawa upatikanaji wake sio rahisi kama upatikanaji wa viazi vitamu.