Ajira 1,056 zanukia kwa watunza kumbukumbu Tanzania
- Ajira hizo ni zile zitakazotolewa kwa mwaka 2024/25
- Waziri Simbachawene asema idadi hiyo ya ajira ni kubwa kuliko miaka mingine.
Arusha. Serikali ya Tanzania imesema inatarajia kuajiri watunza kumbukumbu 1,056 katika mwaka wa fedha 2024/25 ili kukabiliana na uhaba wa watumishi hao.
Waziri wa Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema idadi hiyo ya watumishi watakaoajiriwa kwa mwaka huu ni kubwa kulinganisha miaka iliyopita.
Simbachawene ameyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa 12 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbumbukumbu na Nyaraka Tanzania (Trampa) uliofanyika leo Oktoba 30,2024 mkoani Dodoma.
“Bajeti ya mwaka huu tumepata vibali vya kuajiri watumishi 1,056 idadi hii ni kubwa kulinganisha na miaka mingi nyuma, ni hatua inayohitaji kupongezwa sana tumpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuijali kada hii na kutupa vibali vingi kuliko miaka mingi iliyopita,” amesema Simbachawene.
Mbali na idadi hiyo, Waziri Simbachawene amesema kuwa wataajiri watunza kumbukumbu wasaidizi 1,041, huku nafasi 15 pekee zikiwalenga watunza kumbukumbu wenye elimu ya ngazi ya shahada.
Kutokana na kuwepo kwa wimbi kubwa la wanaohitimu kada hiyo kwa ngazi ya shahada Simbachawene amesema atafanya mazungumzo na katibu mkuu wa wizara yake kuona uwezekano wa kuongeza nafasi hizo kwa wahitimu ngazi hiyo.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutano huo amezitaja faida za kada hiyo nchini kuwa ni pamoja na kuisaidia Serikali kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Kumbukumbu na nyaraka zinasaidia serikali kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma na nyenzo muhimu ambazo zinamsaidia Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua na kuthibitisha uhalali wa matumizi ya fedha za umma,”amesema Abdulla.
Faida nyigine kwa mujibu wa kiongozi huyo ni kuboresha vyanzo vipya vya ukusanyaji wa mapato kwa kuwa kupitia taarifa zilizohifadhiwa tunafahamu maeneo ya uwekezaji yakiwemo ya utalii na hatimaye kukuza pato la Taifa na kuchangia uimarishaji wa miradi ya maendeleo.
Kutokana na umuhimu huo amewataka watunza kumbukumbu hao kusimamia maadili ina miiko ya taaluma kwa kuwa ndiyo msingi mkuu wa kulinda kada zote nchini.