Fahamu faida za kutumia mboga mboga na matunda ya rangi
- Zinasaidia kupambana na kujikinga na magonjwa ikiwemo yasiyoambukiza kama saratani.
- Wataalamu wa afya wameshauri mboga mboga zipikwe kwa mda mfupi ili rangi yake ya asili isibadilike.
Arusha. Matumizi ya matunda na mboga mboga kama sehemu ya mlo yanaendelea kushika kasi katika maeneo mengi nchini huku wengine wakiyatumia kama njia ya kupunguza uzito na kuimarisha afya zao.
Licha ya umuhimu huo, ripoti ya hali ya usalama wa chakula Tanzania Bara kwa mwaka 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu (NBS) pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) inabainisha ulaji wa matunda na mboga mboga nchini ni gramu 148 kwa siku ambao ni chini ya kiwango kinachoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
WHO inashauri ulaji wa angalau gramu 400 za matunda kwa siku kumlinda mtumiaji na magonjwa ya yasiyoambukiza pamoja na vifo.
Wakati matumizi ya kundi hilo yakiendelea kushamiri ni vyema kufahamu umuhimu wa rangi ya tunda au mboga unayochagua kutumia kwa siku kwa sababu kila rangi ina faida fulani za kipekee katika mwili wa binadamu.
Tovuti ya afya ya Healthline imesema miongoni mwa rangi hizo zinazopatikana katika matunda na mboga mboga ni pamoja na kijani, njano, machungwa, nyekundu, buluu, zambarau pamoja na nyeupe.
Kwa mujibu wa Malimi Kitunda, mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) ni lazima kula mboga mboga na matunda yenye rangi tofauti ili uweze kujipatia faida nyingi nyingi zaidi za kiafya.
“Kila kundi la mboga mboga za rangi lilnatofautiana na kundi lingine kwa kuwa linaweza kuwa na kirutubishi au virutubishi fulani kwa wingi lakini likawa na upungufu wa virutubishi vya kundi lingine…
…Ndiyo maana tunashauriwa tujitahidi kula mboga zenye rangi tofauti tofauti ili tupate faida za kutoka katika kila kiundi,” amefafanua Malimi.
Mboga mboga za rangi ya Kijani
Kundi hili linahusisha matunda na mboga mboga kama mboga za majani, pilipili hoho za rangi ya kijani, parachichi, matango ambayo hutumiwa mara kwa mara na watu wengi kulinganisha na matunda au mboga mboga za rangi nyingine.
Malimi amebainisha kuwa mboga mboga na matunda ya rangi ya kijani zinakemikali ya karotenaid, saphronmy na fragonoid zinazosaidia kuimarisha afya ya ini, mapafu,afya yamacho, fizi, seli na mishipa ya damu.
Mboga mboga, matunda ya rangi ya njano
Kwa wale wapenzi wa ndizi mbivu, pasheni na sweet melon na mengineyo kila wakati mkapokula matunda hayo mnaweza kujipatia faida nyingi ikiwemo kuimarisha afya ya ngozi, kusaidia macho kuona vizuri , kusaidia kuimarisha kinga ya mwili kupambana na magonjwa mbalimbali pamoja na kusaidia katika ukuaji wa mimba na mtoto aliye tumboni.
Faida zote hizo hupatikana baada ya kemikali ya asili ya betakarotone inayopatikana katika matunda hayo kubadilishwa na kuwa vitamin A.
Matumizi ya pilipili hoho za rangi humuwezesha mlaji kupata faida nyingi za kiafya.Picha|Jikopoint.
Mboga mboga, matunda ya rangi Nyekundu
Katika kundi hili utazipata mboga mboga na matunda kama nyanya, matunda damu, ‘strawberries’ na pilipili hoho nyekundu ambazo Malimi anayataja kuwa na kemikali za asili ikiwemo lycopene, athohthayanile, na fragonide zinasaidia kuimarisha afya ya moyo. tezi dume, mfumo wa njia ya mkojo.
“Pia matunda na mboga mboga za rangi nyekundu zinaimarisha kiwango cha rehani. mfumo wa sukari na kulinda mwili usipate magonjwa yasiyoambukiza kama saratani.” amesema Malimi.
Kwa upande wa maandalizi mtaalamu huyo anashauri mboga mboga zipikwe kwa mda mfupi ili rangi yake ya asili isibadilike huku matunda yakitakiwa kuoshwa kwa maji safi na kutumiwa yakiwa mabichi.
Matunda na mboga mboga hizi hutakiwa kutumika wakati wote na watu wa rika zote isipokuwa watoto chini ya miezi sita ambao hawajaanza kula.