TCU yakamilisha awamu tatu za udahili wa wanafunzi elimu ya juu

October 19, 2024 11:30 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja watakiwa kuthibitisha kuanzia Oktoba 19 hadi 21 mwaka huu.

Arusha. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imesema imekamilisha awamu tatu za udahili wa  wanafunzi wa elimu wa juu kwa ngazi ya shahada ya kwanza huku ikiwataka waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja kuthibitisha kabla ya Oktoba 21 mwaka huu.

Dirisha la udahili wa awamu ya tatu lilifunguliwa kwa siku nne kuanzia Oktoba 5 hadi 9 mwaka huu na kuwapa nafasi wanafunzi ambao walishindwa kudahiliwa katika awamu zilizopita kutuma maombi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TCU, Prof Charles Kihampa leo Oktoba 19, 2024 waliodahiliwa katika awamu ya tatu wanatakiwa kuthibisha udahili wao katika chuo kimoja kupitia namba maalum itakayotumwa katika simu zao au kwa njia ya barua pepe.

“Waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika Awamu ya Tatu na wale ambao hawakuweza kuthibitisha udahili katika awamu zilizopita, wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia tarehe 19 hadi 21 Oktoba, 2024…

….Uhibitisho huo unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili,” imesema taarifa ya Kihampa.

Aidha, ambao hawatapata ujumbe huo kwa wakati wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika.

TCU imesisitiza kuwa uthibitisho wa udahili unafanyika kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia wakati wa kuomba udahili na si namna nyingine yoyote.

Mwanafunzi anaweza kurejea orodha ya majina ya waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja inapatikana kwenye tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz) ili kuhakikisha anafanya uhakiki wa chuo kimoja kwa muda uliopangwa.

Waliodahiliwa katika awamu hii watajiunga na wengine 98,890 waliodahiliwa katika awamu ya kwanza na wale wa awamu ya pili katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vilivyopo nchini.

Enable Notifications OK No thanks