Mamlaka ya wenyeviti/wajumbe wa vijiji Tanzania kukoma Oktoba19, 2024

October 18, 2024 11:57 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa ajili ya kupisha zoezi la kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024.
  • Majukumu yao kuendelea kutekelezwa na maafisa watendaji wa vijiji, mtaa au kata.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa amesema mamlaka ya wenyeviti na wajumbe wa halmashauri za vijiji nchini utakoma Oktoba 19, 2024 kupisha zoezi la kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo.

Kwa mujibu wa kanuni ya 21 ya Tangazo la Serikali namba 572 ya Julai 12, 2024, na kanuni ya  22 ya tangazo la Serikali namba 571,573 na 574 ya Julai 12, 2024 zinatoa ukomo wa viongozi kwa wenyekiti wa kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji, mwenyekiti wa kitongoji, mwenyekiti wa mtaa, wajumbe wa kamati za mtaa katika mamlaka za wilaya, miji na mamlaka za miji midogo siku saba kabla ya siku ya kuchukua fomu.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari Mchengerwa amebainisha kuwa kwa kuwa zoezi la kuchukua fomu linatarajiwa kuanza Oktoba 26 mpaka Novemba Mosi, 2024, viongozi hao wanatakiwa kukabidhi madaraka Oktoba 19 mwaka huu.

“Madaraka ya wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa halmashauri za vijiji, na wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za wilaya, miji na mamlaka ya miji midogo yatakoma kuanzia Oktoba 19, 2024, nafasi za viongozi hawa zitajazwa kufuatia uchaguzi utakaofanywa Novemba 27, 2024,” amebainisha Mchengerwa Oktoba 17 mwaka huu.

Aidha, Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuweka mazingira yatakayowezesha uchaguzi wa nafasi hizo kuwa wa demokrasia huru na wa haki na kuongeza kuwa majukumu ya utendaji katika vijiji au mitaa yataendelea kutekelezwa na maafisa watendaji wa mtaa au kijiji husika kwa kushirikiana na maafisa watendaji wa kata.

Hata hivyo, Mchengerwa ameongeza kuwa watendaji wa vijiji au mtaa hawataruhusiwa kutekeleza jukumu lolote la kisheria ambalo linapaswa kuamriwa na halmashauri ya kijiji au kamati ya mtaa hivyo afisa mtendaji wa kijiji au mtaa husika ataliwasilisha jambo hilo kwa afisa mtendaji wa kata ambaye atalazimika kuliwasilisha kwa mkurugenzi wa halmashauri husika ili kupata idhini ya kutekeleza jambo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks