Majirani wafunguka mazito kifo cha binti wa miaka 12 Arusha

October 13, 2024 7:57 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasema mtuhumiwa wa mauaji hayo alikuwa jirani mwema hakuna aliyedhani kuwa angeweza kufanya kitendo hicho.
  • Walitaka jeshi la polisi kuwasaka alioshirikiana nao kutekeleza mauaji hayo.

Arusha. Siku moja baada ya kifo cha mtoto aitwaye Mariam Juma kilichotokea mtaa wa Ramadhan, Morombo jijini Arusha, baadhi ya majirani wa marehemu huyo wamelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka watuhumiwa wote waliohusika na mauaji hayo.

Wakazi hao wametoa maoni hayo leo Oktoba 13, 2024 walipokuwa wakizungumza na vyombo vya habari ikiwa yamepita masaa kadhaa tangu Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha litangaze kumkamata mtuhumiwa wa mauaji hayo anayefahamika kama Jaina Mchomvu katika mji wa Moshi akitoroka baada ya kutekeleza tukio hilo.

Jaina anatuhumiwa kutekeleza tukio hilo Oktoba 12 mwaka huu majira ya asubuhi ambapo alimuuwa mtoto huyo na kuukata kata mwili wake kisha kuuficha chini ya uvungu wa kitanda kwenye nyumba yake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo, mtuhumiwa huyo alihojiwa na kukiri kutenda tukio hilo la mauaji ya mtoto huyo na uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha tukio hilo unaendelea.

Tecla Mremi, Jirani wa marehemu huyo ameiambia Nukta Habari kuwa tukio hilo limeibua taharuki mtaani hapo hususani kwa wanawake wenye watoto na kulitaka jeshi la polisi kuwasaka wale wote waliohusika na mauaji hayo.

“Tukio hili limetuhuzunisha mno, kwa sababu kwanza ni jirani yangu kabisa na mama wa huyo mtoto ni rafiki yangu…Tunaomba Serikali itusaidie hao watu wapo mtaani na mtandao wao ni mkubwa,”amesema Tecla.

Wengine wamemuelezea mwanamke huyo kuwa jirani mwema na haendani na waliyoyabaini nyumabani kwake ikiwemo chupa za damu, hirizi na risiti za kafara za mauaji aliyoyafanya tangu mwaka 1996 akianzia Usangi, Kilimanjaro na baadae kuhamia jijini humo.

“Huyo mama (Jaina Mchomvu) alikuwa jirani mwema kwa sababu allikuwa ana kibali sana, alikuwa anauza mboga na asilimia kubwa tulinunua mboga kwake hakuna aliyedhani kuwa alikuwa muuaji kwa miaka mingi…

…Tunaomba tu watafutwe na aliokuwa anashirikiana nao maana hatuamini kuwa kazi kubwa hii anaweza kuifanya peke yake,”amesema Rehema Ally Mkazi wa mtaa wa Ramadhani,

Kwa upande wake Francis Mbise, Diwani wa Kata ya Muriet ameishukuru Jeshi la Polisi kwa kufanikisha kukamatwa kwa mwanamke huyo na kuwataka wananchi kuwa makini katika malezi ya watoto ili kuwaepusha na vitendo vya kikatili.

“Nitoe wito kwa wazazi kama kiongozi wazazi tuwalinde watoto wetu jamani dunia imebadilika usimuamini mtu…na watoto wenyewe wafundishwe wasiwe wanaingia kwa mtu, kwenye gari au bajaji kama hamjui asiingie,”amesema Diwani Mbise.

Aidha, Taarifa ya SACP Masejo imewataka wananchi kutoa ushirikiano katika kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo  pamoja na kuendelea kuripoti matukio hayo ili watuhumiwa wachukuliwe hatua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks