Ratan Tata afariki siku chache kabla ya tamasha la Land Rover Arusha

October 10, 2024 3:45 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Mjukuu wa Ratanji Tata mwanzilishi wa Kampuni za Tata
  • Ndio kampuni inayotengeneza gari za Discovery, Defender pamoja na Range.

Arusha. Ikiwa zimesalia siku chache kuelekea tamasha la magari la Land Rover Festival linalotarajiwa kufanyika mkoani Arusha, tajiri mashuhuri wa India na aliyekuwa mwenyekiti wa kampuni za Tata (Tata Group),  Ratan Tata, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86.

Tata alikuwa mmoja wa viongozi wa biashara wanaotambulika kimataifa kutoka India, na Tata Group ni moja ya makampuni makubwa zaidi nchini humo ambayo yanatengeza magari ya Land Rover ikiwemo Range ambayo ni maarufu kwa muonekano mzuri pamoja na uimara wake.

Awali magari hayo yalitengenezwa na kampuni ya Uingereza ya Jaguar Land Rover ambayo ilinunuliwa na Ratan Tata akiwa Mwenyekiti wa Kampuni za Tata  mwaka 2008 kwa Dola za Marekani bilioni 2.3 sawa na Sh6.267 trilioni kwa viwango vya kubadili fedha vya sasa.

Tata alistaafu uenyekiti wa kampuni za Tata Group mwaka 2012, ingawa alihudumu kwa muda mfupi kama kaimu mwenyekiti na mpaka umauti unamfika alikuwa mwenyekiti wa heshima kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo.

Kifo cha Tata ni pigo kuwa katika sekta ya biashara nchini India ambapo Tata Group ni moja ya kampuni kubwa zaidi nchini humo yenye mapato ya kila mwaka yanayokadiriwa kufikia dola bilioni 100 sawa na zaidi ya Sh300 trilioni za Tanzania.

Safari ya Ratan Tata kibiashara

Baada ya kuhitimu Shahada ya Usanifu Majengo katika Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani mwaka 1962, Ratan Tata alirudi India na akaanza kufanya kazi kwenye kampuni za Tata ikiwemo Telco, na Tata Steels ambazo zilianzishwa na babu yake Ratanji Tata karibu miongo 10 iliyopita.

Mwaka 1992 Ratan alishika usukani wa uongozi kwenye kampuni hizo na miaka nane baadae kampuni hiyo chini ya uongozi wake ilitanua wigo kwa kuyanunua makampuni mengine ya Uingereza ikiwemo kampuni ya chai ya Teley iliyonunuliwa kwa Dola milioni 432 za Marekani na Kampuni ya ufuaji vyuma ya Corus iliyonunuliwa kwa Dola  bilioni 13 za Marekani mwaka 2007.

Kwa wakati huo ndio uilikuwa ununuzi mkubwa zaidi wa kampuni ya kigeni na kampuni ya India.

Baadae,Tata Motors ilinunua chapa za magari ya kifahari ya Uingereza ya Jaguar na Land Rover kutoka kwa Ford Motor Co (F.N).

Tata Motor ilianzishwa mwaka 1885 kama kiwanda cha kutengeneza baiskeli na kwa sasa wanazalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo chai, vinywaji laini, magari, vifaa vya mawasiliano pamoja na uchakataji wa kemikali.

Land Rover, moja ya bidhaa inayozalishwa na Tata kwa sasa ina  matoleo saba ikiwemo Defender, Discovery, pamoja na Range Rover. 

Matoleo hayo ya Land Rover ndiyo yanayotegemewa kupamba tamasha la magari  linalotarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 12 hadi 14 2024 jijini Arusha ambapo zaidi ya mataifa tisa kutoka barani Afrika yanatarajiwa kushiriki.

Akizungumza na wanahabari Septemba 23, mwaka huu Paul Makonda Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema paredi hiyo ya matoleo yote ya Land Rover itakuwa na urefu wa kilomita zaidi ya 12 ambapo washiriki zaidi ya 1000 wa tamasha hilo watapata fursa ya kutalii bure kwenye hifadhi ya Taifa Arusha kwa kutumia magari hayo.

Enable Notifications OK No thanks