TCRA yaifungia Mwananchi Communications kwa siku 30

October 3, 2024 9:41 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeeleza kuwa kampuni hiyo ya habari imekiuka masharti ya leseni kwa kuchapisha maudhui yaliyozuiwa. 

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha leseni zote za kuchapisha maudhui mtandaoni za kampuni ya Mwananchi Communication Ltd kwa siku 30 kwa tuhuma za kuchapisha maudhui yaliyozuiwa kisheria, uamuzi ambao ni pigo kwa chombo hicho cha habari kikubwa nchini. 

Katika taarifa iliyotolewa usiku wa Jumatano, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dk Jabiri Bakari amesema Mwananchi Communication Ltd hawatakiwi kutangaza maudhui yaliyozuiwa ikiwa ni pamoja na yale “yanayolenga kudhihaki au kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. 

Hata hivyo, Dk Bakari amesema Oktoba 1, 2024 Mwananchi Communication walichapisha maudhui mjongeo na sauti (Audio-visual content) kwenye mitandao yake ya kijamii ambayo yamezuiwa kwa mujibu wa kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni. 

“Maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa Taifa jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa,” amesema. 

Kutokana na tuhuma hizo, TCRA imesema imesitisha leseni za kuchapisha maudhui za kampuni hiyo zinazojumuisha The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti kutoa huduma mtandaoni kwa siku 30 mpaka masuala mengine ya kiusimamizi yatakapofanyiwa kazi. 

Oktoba Mosi The Citizen walichapisha video ya vikaragosi (animation) kwenye mitandao ya X na Instagram ikimwonyesha mwanamke mmoja aliyevalia gauni la njano na ushungi wa kijani akiangalia televisheni inayoonyesha habari za watu wanaolalamika kupotelewa au kuuawa kwa ndugu zao. 

Hata hivyo, baada ya muda The Citizen waliifuta video hiyo waliyoeleza kuwa ililenga kuonyesha matukio yanayoonesha masuala ya ulinzi na usalama wa watu Tanzania. 

Katika taarifa yake mtandaoni, The Citizen ilisema kuwa maudhui hayo yalitafsiriwa vibaya, kinyume na malengo yake ya awali. 

Mwananchi Communication Ltd imesema kutokana na zuio hilo la TCRA, watasitisha uchapaji wa maudhui mtandaoni katika mitandao yao yote kwa siku 30. 

“Mwananchi Communications Ltd (MCL) inaahidi kuwaletea wateja na wasomaji wetu habari, taarifa na maudhui bora yanayowezesha taifa kupitia magazeti yetu, na huduma zetu nyingine zisizo za mtandaoni wakati tukiendelea kuzungumza na mamlaka husika ili kupata muafaka,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Victor Mushi na Mhariri Mkuu Mtendaji Msaidizi, Mpoki Thomson. 

Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii na watetezi wa haki za binadamu wamekosoa uamuzi wa TCRA kufungia leseni za MCL wakieleza kuwa kunarudisha nyuma jitihada za kuimarisha demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari nchini. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks