Mwenge wa uhuru kuzindua miradi 58 Mwanza
- Mbio za mwenge huo zitafanyika katika wilaya zote saba na halmashauri nane za jiji la Mwanza.
- Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa kilele cha mbio hizo Oktoba 13 mwaka huu.
Mwanza. Mwenge wa uhuru unatarajiwa kukimbizwa jijini Mwanza kwa zaidi ya kilomita 627 na kuzindua miradi 58 yenye thamani ya zaidi ya Sh99.3 bilioni katika vijiji, wilaya na halmashauri zilizopo mkoani humo
Mwenge huo, utakaokimbizwa kwa siku saba, utapokelewa Oktoba 6 mwaka huu katika kijiji cha Nyamadoke, Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema ukitokea mkoa wa Geita na kuhitimishwa Oktoba 13 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 1, 2024 amesema mwenge huo utakimbizwa katika wilaya zote saba na halmashauri nane za mkoa huo na kukagua, kuweka mawe ya msingi, kuzindua na kutembelea miradi ya mbalimbali ya maendeleo.
“Kati ya fedha hizo (zilizotengwa kwa ajili ya miradi) Sh 2.6 bilioni zinatokana na michango ya wananchi, Sh2.7 bilioni zinatokana na halmashauri za Mkoa wa Mwanza na Sh19.7 bilioni zimetolewa na Serikali kuu huku wahisani na wadau wa maendeleo wakichangia Sh74.2 bilioni,” amesema Mtanda.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kilele cha mbio hizo za uhuru kitafanyika jijini humo Oktoba 14, 2024 katika uwanja wa CCM Kirumba huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Mbali na uzinduzi wa miradi ya maendeleo, kilele cha mbio hizo za mwenge kitatanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki Oktoba 14 mwaka 1999.
Aidha, katika mbio hizo za mwenge kutafanyika kilele cha wiki ya vijana nchini itakayofanyika Oktoba 13 mwaka huu itakayohusisha maonesho ya kazi na miradi mbalimbali inayofanywa na vijana na kuhitimishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Latest