Vodacom Tanzania yazindua huduma za matengenezo ya simu kwa wateja wake

September 27, 2024 3:25 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni huduma ya kwanza Tanzania na itaanza kutolewa kwa watumiaji wa simu za Neon Ultra, Samsung, Vivo, Motorola, Honor na Oppo.

Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc imezindua vituo vya huduma za matengenezo ya simu kwa wateja wao ikiwa ni mkakati wa kuboresha huduma zake kwa wateja jambo litakalowapunguzia muda na gharama watumiaji.

Kwa mujibu wa Vodacom huduma hizo zinatolewa kwa ushirikiano wa watengenezaji wa simu za Neon Ultra, Samsung, Vivo, Motorola, Honor na Oppo na zitakuwa zinatolewa katika maeneo mbalimbali nchini ingawa kwa sasa wameanza na duka la Vodacom Mlimani City kama mfano.

Geogre Lugata, Mkuu wa Idara ya Mauzo na Usambazaji aliyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo Septemba 25, 2024 kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc Philip Besiimire amesema huduma hiyo mpya ni muendelezo wa huduma bora zinazotolewa na kampuni yake na kuongeza kuwa itatolewa kwa ufanisi na urahisi.

“Kipaumbele chetu daima ni kutoa huduma bora kwa wateja wetu na huduma hii mpya ni mwendelezo wake. Kwa kushirikiana na washirika wetu hawa, tunaweza kuhakikisha kwamba wateja wetu wanapata huduma kirahisi na kwa ufanisi zaidi. Uzinduzi huu ni mwanzo tu, tunapanga kuongeza vituo zaidi ili kukidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka kote nchini,” amesema Lugata.

Huduma hiyo itakuwa mkombozi kwa baadhi ya watumiaji wa simu ambao hukumbana na changamoto ya kutopata mafundi sahihi au kukosa kabisa jambo linalosababisha kuingia gharama ya kununua simu mpya pale walizonazo zinapoharibika. Picha l Vodacom

Kwa mujibu wa Lugata mpaka sasa Vodacom ina vituo 11 vya huduma za matengenezo katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania kikiwemo cha Mlimani City Dar es Salaam ambapo kutokana na ongezeko la mahitaji kampuni hiyo inapanga kupanua mtandao wa vituo vyake vya matengenezo ili kusaidia wateja wengi zaidi.

Hata hivyo kwa kuanzia kampuni hiyo itafanya matengenezo ya simu za Neon Ultra, Samsung, Vivo, Motorola, Honor na Oppo pekee huku ikiwa na mpango wa kukaribisha makampuni mengine ya simu kuungana nao ili kuongeza ujumuishwaji wa kidijitali nchini. 

Kwa upande wake Meneja wa Maduka ya Rejareja, Vanessa Mlawi amesema huduma zinatotolewa na  vituo hivyo si tu sio tu zinaongeza ujumuishi bila kubagua wateja bali pia zinaimarisha chapa ya kampuni ya Vodacom. 

“Inatusaidia kushughulikia changamoto za wateja huku pia ikitoa fursa ya kuuza bidhaa na huduma zingine za Vodacom. Zaidi, vituo hivi vinatupa mwangaza kujua mahitaji ya wateja wetu, na namna bora ya kuboresha huduma zetu,” amesema Mlawi aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja, Harriet Lwakatare.

Aidha, mbali na kuboresha huduma kwa wateja, ushirikiano huu unaendana na dhamira ya Vodacom ya kuwa kinara wa mabadiliko ya kidijitali kote nchini ambapo vituo vya matengenezo vitasaidia kuwahudumia wateja wa kampuni hiyo huku pia vikiongeza matumizi ya simu na uelewa wa kidijitali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks