Unaweza kuishi Dar es Salaam kwa Sh3,000 kwa siku?

September 3, 2024 3:41 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamesema kuishi Dar kwa Sh3,000 ni mtihani.
  • Wengi wao hutumia zaidi ya Sh10,000 kwa siku.

Dar es Salaam. Hapana shaka kupanda kwa bei za bidhaa na huduma muhimu kama vile chakula na usafiri nchini kunaendelea kuongeza maumivu kwa wananchi hasa wenye kipato kidogo kutokana na kuongeza gharama za maisha. 

Baadhi ya vyakula na bidhaa zisizo za chakula bei zake zimeongezeka miaka ya hivi karibuni kiasi cha kufanya baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam kushindwa kuishi chini ya Sh5,000 kwa mtu mmoja kwa siku. 

Nukta Habari tuliwauliza baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam iwapo wanaweza kumudu gharama za maisha kwa Sh3,000 kwa siku na kama si hivyo ni kiwango gani cha chini kinawatosha? 

Swali hili lilitokana na takwimu za Ripoti ya Utafiti wa Bajeti ya Kaya (Household budget survey report) wa mwaka 2017/18 iliyoeleza kuwa mtu mzima mmoja Tanzania Bara alikuwa anatumia wastani wa Sh94,997 kwa mwezi sawa na Sh3,166 kwa siku. 

Utafiti huo uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unabainisha kuwa mtu mzima alikuwa anatumia wastani wa Sh49,045 kwa mwezi kwa ajili ya chakula na Sh45,952 kwa ajili mahitaji yasiyohusu chakula. 

Mkazi wa Mwananyamala jijini Dar es Salaam Petro Berenado (52) anaeleza kuwa Sh3,000 haitoshi kumudu gharama za maisha yake kwa siku kutokana na gharama za maisha kuwa juu.

“Huwezi kuishi kwa Sh3,000 hata Sh10,000 huwezi kuishi nayo kwa sababu mimi napanda gari hapa naenda Kariakoo, Kariakoo peke yake ndio nauli rahisi Sh600 kwenye buku (Sh1,000) inabaki bei gani, sijanywa chai bado, haya mimi sisafiri kila siku?” amesema Berenedo. 

Anasema kuwa ukiachana na gharama zake mwenyewe kwa watu wenye familia gharama za maisha zimepanda kiasi kwamba hata Sh20,000 kwa siku bado haitoshi. 

“Nina mtoto wa ‘form one’ (kidato cha kwanza) kwa siku yeye peke yake anatumia Sh3,000 anaenda shule…nina mjukuu wangu anatumia Sh3,000, kabla sijaamka kitandani Sh6,000 tayari imeisha,” anasema Berenado.

Ripoti hiyo ya NBS inabainisha zaidi kuwa kwa wakati huo mwaka 2017/18 kaya moja Tanzania Bara ilikuwa inatumia wastani wa Sh416,927 kwa mwezi huku kaya zilizopo Dar es Salaam zikiongoza kwa kutumia wastani wa Sh720,946 kwa mwezi. 

Wastani wa mtu mzima jijini Dar es Salaam alikuwa anatumia Sh186,605 kwa mwezi sawa na Sh6,220 kwa siku kiwango ambacho Berenedo anasema kinamtoka kabla ya kutoka kitandani. 

Kwa Hamis Ally, anayefanya kazi ya kufyatua matofali Kinondoni, akiwa na Sh 3,000 mfukoni hachukulii kama ana pesa.

Ally anasema ili na yeye ajisikie “tajiri” anahitaji kupata angalau Sh7,000 kwa siku. 

“Mimi mwenyewe asubuhi na kunywa chai ya Sh1,000, mchana nakula chakula cha Sh2,000 sio kama nakula hivi kwamba nimeshiba yaani nasogeza tu ilimradi nisije kukata uhai, je jioni nakula nini?” amehoji. 

Ugumu wa maisha si tu kwa watu wa chini tu wanaofanya vibarua na kazi nyingine zisizo rasmi bali hata kwa baadhi ya waajiri kwenye kazi rasmi na wafanyabiashara ndogo ndogo wanaotegemea mapato katika biashara hizo kumudu gharama za maisha. 

Joyce Julius (46), mkazi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam, aliiambia Nukta Habari kutokana na hali ngumu ya maisha, hata mzunguko wa pesa umekuwa mgumu na ni vigumu kukidhi mahitaji kwa kutumia Sh3,000 kwa siku.

“Kwa siku mimi kama mimi ninaweza kutumia peke yangu Sh5,000 bado sijajua wanangu wanakula nini hela ya shule kila siku wanatumia Sh1,000 hadi Sh2,000…nimejibana sana inabidi kutumia Sh5,000 kwa sababu siwezi kunywa maji ya 600 lita moja lazima ninywe lita mbili,” anaeleza Joyce.

Umaskini ni miongoni mwa matatizo ambayo yameendelea kuikumba Tanzania licha ya jitihada kubwa zilizofanyika kupunguza idadi ya watu wanaoishi kwenye umaskini wa kutopea.  

Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi ya Taifa katika mwaka 2023 iliyochapishwa Juni mwaka huu Serikali inaendelea kuboresha ustawi wa jamii na kupunguza umaskini uliokithiri kupitia programu mbalimbali ikiwemo Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf). 

Utekelezaji wa mpango huo kwa mwaka 2023, ulihusisha uhawilishaji wa fedha kwa kaya maskini, kutoa ajira za muda mfupi kwa kaya za walengwa na kuhamasisha uundaji wa vikundi vya kuweka akiba, kukopeshana na kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali kupitia vikundi hivyo. 

Hadi Desemba 2023, kaya zilizonufaika na mpango huo wa Tasaf zilikuwa zaidi ya 1.371,916 zenye wanufaika 6,938,481 ikilinganishwa na kaya 1,371,038 zenye wanufaika 6,596,820 katika kipindi kama hicho mwaka 2022. 

Ongezeko hilo lilitokana na marekebisho ya taarifa kwa baadhi ya kaya zilizokuwa kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya tathmini ya mpango, ripoti hiyo imeeleza.

Enable Notifications OK No thanks