Mambo anayopaswa kufanyiwa binti aliyebakwa Tanzania

August 7, 2024 7:09 pm · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kwenda kupimwa afya haraka baada ya tukio la kubakwa na kumpatia tiba ya kisaikolojia ili aweze kurejea kwenye hali yake ya kawaida.
  • Baadhi ya mikoa matukio haya yamekua yakijirudia mwaka hadi mwaka.
  • Inawezekana kuwa sawa ingawa itachukua muda. 

Dar es Salaam. Kwa siku tatu sasa kumekuwa na shinikizo kubwa kwa vyombo vya usalama kuwakamata vijana watano wanaodaiwa kumbaka na kumlawiti binti mdogo anayedaiwa kutokea Yombo Dovya Shuleni jijini Dar es Salaam, katika tukio lililoibua hisia kali za kutaka uwajibikaji na ulinzi wa kisaikolojia wa binti huyo. 

Tangu kuvuja kwa video hizo mwishoni mwa juma lililopita wananchi, mawakili, wanasiasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamejitokeza kwa wingi kupinga ukatili huo huku wakitaka mamlaka zichukue hatua za haraka kuwafikisha watuhumiwa wa tukio hilo mahakamani. 

Jumapili iliyopita vilisambaa vipande vya video kwenye mitandao ya kijamii vilivyoonyesha vijana watano wakimbaka binti huyo kwa zamu wakidai “wametumwa na afande” ikiwa ni mwendelezo wa makosa dhidi ya binadamu nchini yakiwemo ubakaji na ulawiti.

Baada ya kusambaa video hiyo Jeshi la Polisi lilieleza kuwa linachunguza tukio hili ili kuwakamata watuhumiwa ili wachukuliwe hatua za kisheria huku likiwasihi watumiaji wa mitandao kuacha kusambaza video hizo kulinda utu na kupunguza maumivu ya kisaikolojia ya binti huyo. 

Hadi sasa polisi hawajaeleza iwapo wamewakamata watuhumiwa wa tukio hilo au la japo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alinukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema kuwa “tayari” wametiwa nguvuni. 

Binti huyo ni miongoni mwa mamia ya Watanzania wanaobakwa au kulawitiwa nchini na tukio lake limeonesha ueneaji wa makosa dhidi ya binadamu hususani ubakaji na ulawiti kwenye mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar. 

Ubakaji ni tatizo Tanzania

Uchambuzi wa takwimu za uhalifu nchini uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa baadhi ya mikoa matukio haya yamekua yakijirudia mwaka hadi mwaka wakati waathirika wakikabiliana na madhara ya kusambazwa kwa video za utupu zenye malengo ya udhalilishaji kupitia mtandao ya kijamii na hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa na Ukimwi.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu za hali ya uhalifu Tanzania zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi jumla ya matukio 39,447 ya ubakaji na 7,561 ya ulawiti yameripotiwa Polisi ndani ya kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni. 

Kwa mwaka 2023 pekee, kulikuwa na matukio ya ubakaji 8,691 yakiwa yameongezeka kidogo kutoka matukio 6,827 mwaka 2022. Hali hiyo ilionekana pia katika makosa ya ulawiti yaliyofikia 2,488 mwaka 2022 kutoka makosa 1,586 ya ubakaji na ulawiti sawa na ongezeko la asilimia 56.9.Hili ni ongezeko kubwa zaidi la uhalifu wa aina hii kuripotiwa ndani ya miaka mitano ya hivi karibuni.

Mikoa ya kipolisi ya Kinondoni, Tanga, Mbeya, Kilimanjaro na Morogoro imeongoza kwa kujirudia matukio ya makosa ya ubakaji na ulawiti.

Ripoti ya mwaka 2020 ya hali ya uhalifu Tanzania inataja utandawazi, imani za kishirikina, tamaa za kimwili na kukosa maadili ya kidini na kijamii kuwa miongoni mwa sababu za kujirudia mara kwa mara kwa matukio ya ubakaji na ulawiti katika maeneo mengi nchini.

Msaada anaotakiwa kupatiwa binti aliyebakwa

Waathirika wa matendo hayo ya kihalifu kama binti huyo, aliyebakwa na kisha video zake kusambazwa mtandaoni, hupitia nyakati ngumu hali inayohitaji msaada wa watu wa karibu, matibabu ya wataalamu wa afya ya mwili na afya ya akili.

Watalaam wa saikolojia na tiba wameelezea kuwa tukio hilo linaoendelea katika mitandao ya kijamii lina athari kubwa sana kisaikolojia kwa mtu hivyo jamii inayomzunguka isitumie tukio hilo kumnyoshea kidole na kumlaumu kwa makosa ambayo tayari yameshatokea badala ya kumsaidia kukaa sawa.

Daktari wa Saikolojia Tiba, Nickson Katavi ameiambia Nukta Habari kuwa miongoni mwa madhara yanayowakumba waathirika ni pamoja na msongo wa mawazo, kuhisi hofu na hatari muda wote, sonona, kukosa usingizi, hali ya kutojithamini na kuona hafai tena baada ya kufanyiwa ukatili ‘Post Traumatic Stress Disorder’.

Dk Nickson amebainisha hatua za awali na endelevu ambazo zinapaswa kuchukuliwa ili kumsaidia muathirika wa tukio hilo la ubakwaji kuwa ni kumpeleka hospitali ili kufanyiwa vipimo vya afya yake pamoja na tiba ya kisaikolojia.

“Tunahitaji kujua hali yake ya kiafya kwa sababu hatuna uhakika na usalama wa watu waliofanya hilo jambo inawezekana wameathirika na VVU au magonjwa mengine ya kingono ili kuweza kumsaidia dawa ambazo anaweza akatumia kuzuia maambukizi au kutibu magonjwa anayoweza kua ameambukizwa” amesema Dk Nickson.

Binti asilaumiwe, kutengwa

Mwathirika anapaswa kufika kituo cha afya ili kufanya vipimo na kuanza taratibu za matibabu kwa mujibu wa ushauri wa wataalamu wa afya.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wanafamilia wanapaswa kuzingatia viashiria muhimu vya kihisia na tabia mpya zinaoonekana muda mfupi baada ya ndugu wao kufanyiwa ukatili, mfano wa tabia ni mhanga kupendelea kujitenga kwa sababu ya kujiona hafai hali inayoweza kusababisha mwathirika kuchukua maamuzi yasiyofaa.

“Ukisikia anatoa kauli za kukata tamaa kwenye maisha na kujidhuru ni wakati ambapo unatakiwa uwe makini na usichukulie kirahisi, hiyo ni changamoto kubwa sana…inawezekana mwisho wa siku akajiondoa uhai,” amesema Dk Nickson.

Mwenza wa mwathirika wa tukio la ubakwaji hususan lililowahi kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Dk Nickson amesema anapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za kiakili na kimwili zinazoweza kudumu kwa wastani wa muda mrefu kutokana na ugumu wa kupotea kabisa kwa video kama hizo.

Watu wa karibu na mwathiriwa wanasisitizwa kuepuka kabisa kauli za kumlaumu, kumhukumu, wanapaswa kutomuuliza maswali yasiyo na maana yenye lengo la kukidhi matakwa binafsi kama kumuuliza namna walivyomfanyia unyama kwa kuwa humsababishia hasira kali badala ya kumsaidia.

“Kitu ambacho hutakiwi kufanya ni kumpuuza au kupunguza uzito wa tukio, kumlaumu, kumlazimisha aongee, kumuepuka na kumshinikiza arudi katika hali ya kawaida haraka,” ameongeza Dk Nickson.

‘Binti huyo ni mshindi’

Kwa upande wa mtaalamu wa saikolojia na mahusiano Leyla Abubakari amesema kuwa jamii inapaswa kumchukulia muathirika huyo kama mshindi aliyeshinda vita dhidi ya uhai wake.

“Kuna watu wengine wakifanyiwa matukio kama haya wanakimbilia kutoa uhai wao, hivyo kwa huyu jamii inatakiwa kumchukulia kama mshindi kwa sababu yupo hai na inawezekana kuwa sawa ingawa itachukua muda hivyo ni vyema familia, ndugu na Taifa kwa ujumla kumfanya asijihisi mwenye makosa,” amesema Leyla Abubakari.

Leyla amewataka Watanzania wote kujifunza kupitia tukio hilo hususani mabinti kwa kuthamini na kujali maisha yao ili kuepusha matatizo ambayo yatachangia kwa namna moja au nyingine kuharibu mpangilio wa maisha ya

Enable Notifications OK No thanks