Bei ya petroli, dizeli yashuka kiduchu Tanzania

June 6, 2024 4:59 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Petroli yashuka kwa Sh53 na dizeli kwa Sh84
  • Lita moja ya petroli jijini Dar es Salaam inauzwa kwa Sh3,261 na dizeli Sh3,112.
  • Wakazi wa Kyerwa mkoani Kagera ndiyo wanaonunua mafuta hayo kwa bei ya juu zaidi kulinganisha wakazi wa mikoa mingine nchini.

Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania sasa watakuwa na ahueni baada ya bei za mafuta mwezi Juni kupungua kidogo ikilinganishwa na ilivyokuwa mwezi uliopita ikichangiwa na kuporomoka kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.

Bei mpya zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) leo Juni 5, 2024 zinabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli imeshuka kwa Sh53 kwa lita huku ile ya dizeli ikipungua kwa Sh84 kwa lita.

Kutokana na bei hizo mpya lita moja ya petroli jijini Dar es Salaam inauzwa kwa Sh3,261 kutoka Sh 3,314 iliyokuwa inatumika mwezi Mei na dizeli inauzwa kwa Sh3,112 ikipungua kutoka Sh3,196 iliyorekodiwa mwezi uliopita.

Hali ni tofauti kwa mafuta ya taa ambayo yamepanda kwa Sh421 kwa lita kutoka Sh 2,840 iliyotumika mwezi Mei hadi Sh3,261 inayotumika mwezi Juni.

Ahueni hiyo ya kushuka kwa bei ya mafuta imeenda pia kwa watumiaji wa mkoa wa Tanga ambao wananunua petroli kwa Sh3,263 kutoka Sh3,360 na dizeli kwa Sh3,121 kutoka Sh3,242 na mkoani Mtwara wananunua petroli kwa Sh3,267 kutoka Sh3,317 na dizeli kwa Sh 3,122 kutoka Sh3,200 iliyotumika mwezi Mei.


Soma zaidi:Matinyi: mkopo wa Jamhuri ya Korea utalipwa kwa miaka 40


Kwa mujibu wa Ewura kushuka kwa bei hiyo ya mafuta iliyopaa kwa miezi miwili mfululizo kumechangiwa na kushuka kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.

“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Juni 2024 yamechangiwa na kupungua kwa bei za mafuta yaliyosafirishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 11.82 kwa mafuta ya petroli, asilimia 7.77 kwa mafuta ya dizeli,” imesema taarifa Ewura.

Wakazi wa Kyerwa mkoani Kagera ndio wanaonunua mafuta hayo kwa bei ya juu zaidi kulinganisha wakazi wa mikoa mingine nchini ambapo lita moja ya Petroli inauzwa kwa Sh3,499, dizeli Sh3,350 na mafuta ya taa kwa Sh3,498.

Wakati wakazi wa Kyerwa wakitoboa mifuko yao kupata nishati hiyo kwa ajili ya vyombo vyao vya moto wakazi wa Kibaha mkoani Pwani wananunua nishati hiyo kwa bei ndogo zaidi ukitoa mikoa ya Dar es Salaam na Tanga ambapo lita moja ya dizeli inauzwa kwa Sh3,121 na petroli kwa Sh3,263.

Enable Notifications OK No thanks