Uchaguzi Mkuu 2020: Vyama vya siasa Tanzania vinazungumziaje fursa za utalii?
- Baadhi vyaahidi kushughulikia athari za COVID-19 katika sekta ya utalii.
- CCM, ACT-Wazalendo kujenga miundombinu ya utalii ikiwemo hoteli.
- Chadema kushirikiana na sekta binafsi kufanya maboresho ya sheria zinazosimamia utalii.
Dar es Salaam. Ukiitaja Tanzania hutaacha kuitenganisha na umaarufu wake wa kusifika kama kisiwa cha amani duniani. Laki ni zaidi ya hapo.
Tanzania ni kituo muhimu cha shughuli za utalii kutokana na kuwepo kwa utajiri mkubwa wa maliasili za mimea na wanyama ambao wameifanya kuwa kivutio cha wageni wanaotoka maeneo mbalimbali duniani.
Kutoka Kusini hadi Magharibi hadi katika kilele cha mlima Kilimanjaro, utakutana na kila na namna ya uzuri ulio tofauti na maeneo mengine duniani.
Rasilimali hizo zimekuwa ni mazao muhimu kuvutia shughuli za utalii kufanyika katika hifadhi za Taifa, jambo linatoa fursa kwa nchi kupata mapato kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii.
Lakini sekta ya utalii ambayo huchangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la Taifa, inapitia kipindi kigumu kutokana na athari za janga la Corona ambalo limevuruga masoko ya utalii duniani yaliyokuwa yanategemewa na Tanzania kupata mapato.
Hata hivyo, kwa sasa janga hilo limetokomezwa nchini na tayari Serikali imefungua milango kwa watalii kuja nchini.
Makundi ya tembo ambao wanapatikana katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Tembo hao wamekuwa wakivamia mashamba ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Picha|Mwaramu Mpunde.
Kutokana na changamoto hizo za utalii, baadhi ya ilani za vyama vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu zimeeleza mikakati mbalimbali vitakayotekeleza kuinua sekta hiyo pale serikali zao zitakapoingia madarakani. Nini kimezungumziwa?
CCM watamba kuongeza mazao ya utalii
CCM katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 imesema itabuni na kutekeleza mikakati ya kuongeza na kukuza wigo wa mazao ya utalii ili kufikia watalii milioni 5 kwa mwaka kufikia mwaka 2025 na kuongeza mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 (Sh6.1 trilioni) mwaka 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 6 (Sh13.9 trilioni) mwaka 2025.
Chama hicho tawala kimeeleza katika ilani yake kuwa ili azma hiyo ifanikiwe kitakuza na kuimarisha uwindaji wa wanyamapori na utalii wa mikutano kwa kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano wa kisasa utakaojumuisha hoteli zenye hadhi ya kimataifa jijini Dar es Salaam.
“Kuendeleza utalii wa fukwe kwa kutenga maeneo mahsusi ya fukwe, kuyasimamia na kuyaendeleza kimkakati; kujenga miundombinu ya kimkakati ya kuwezesha meli za kitalii kuzuru nchini; na kutekeleza mikakati mingine ya kuongeza wigo wa utalii,” inasomeka sehemu ya ilani ya CCM ya 2020-2025.
Pia, CCM imeahidi kuwa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) itaimarishwa ili iweze kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kwenye masoko ya kimkakati na kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia sekta ya utalii nchini ikiwemo kuhamasisha na kusimamia utalii endelevu na wenye kuzingatia masilahi ya nchi.
Sekta binafsi nayo itashirikishwa na Serikali ya CCM kwa kuandaa na kuwatambua wataalam wenye ukarimu, ujuzi na weledi unaohitajika katika utoaji wa huduma za utalii ili kukuza sekta hiyo na kuongeza ajira kwa wananchi na Pato la Taifa.
“Kuhamasisha jamii ili iweze kujua umuhimu wa utalii kuanzia ngazi ya chini ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mitaala inayojumuisha utalii katika shule na vyuo kimkakati,” inaeleza ilani ya chama hicho.
Soma zaidi:
- Chadema, CCM vyaahidi kukuza uchumi wa kidijitali Tanzania
- CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
- Uchaguzi Mkuu 2020: Kodi yateka ajenda vyama vya siasa Tanzania
Chadema kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 2 kwa mwaka
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitabeba gharama za mkakati wa mawasiliano wenye kulenga kushawishi utalii kurudi katika hali yake ya hapo awali ikiwemo kuongeza idadi ya watalii, kufungua vivutio vipya vya utalii na kuwa na ulinzi wa uhakika kwa watalii.
Ikiwa kitafanikiwa kuingia madarakani, kitaongeza idadi ya watalii nchini hadi kufikia milioni 2 kwa mwaka katika kipindi cha utekelezaji wa ilani yake.
Pia chama hicho ambacho kimemsimamisha Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu kugombea nafasi ya urais, kimesema kitashirikiana na sekta binafsi kuanzisha miundombinu ya utalii yenye viwango vya kimataifa kwa ajili ya kutoa huduma kwa watalii kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo bahari.
“Serikali ya Chadema itaanzisha mfumo wa haki miliki katika filamu na picha zitakazopigwa katika maeneo yenye vivutio nchini,” inasomeka sehemu ya ilani ya Chadema ya 2020-2025 huku msisitizo ukiwa ni kujenga miundombinu ya utalii ikiwemo hoteli na kuimarisha mafunzo.
Suala la kuukuza utalii pia limezungumziwa na chama cha ACT-Wazalendo katika ilani yake ya mwaka huu ambapo kimeeleza kuwa kitarekebisha sera za kodi ili kuirejesha katika hali yake ya kawaida sekta ya utalii pamoja na mnyororo wake wa thamani ambao umeathirika na janga la virusi vya Corona.
Marekebisho hayo yatahusisha kutoa ruzuku kwa kampuni za utalii na kulinda ajira za wafanyakazi wa sekta hiyo.
Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote Afrika umekuwa kivutio muhimu kwa watalii wanaopenda kupanda milima. Picha| Mtandao.
Kama ilivyo kwa CCM na Chadema, chama hicho kimeeleza kuwa kitawekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya maeneo ya utalii ili kufungua vivutio vipya na kuvifanya kufikika kwa urahisi na kwa usalama.
“Itawezesha sekta binafsi kuongeza vyumba vya hoteli kwenye vivutio vya utalii, itaanzisha kampeni maalumu ya kufikisha idadi ya watalii milioni 5 watakaoingia nchini ifikapo Mwaka 2025,” inaeleza ilani ya ACT-Wazalendo.
Katika Serikali mpya ya chama hicho itatumia sekta ndogo za michezo na burudani kimkakati kama nyenzo za kukuza utalii nchini.
Bado una nafasi ya kuangazia sera za vyama vingine vitakavyoshughulikia masuala ya utalii ikiwa vitachaguliwa Oktoba 28 ili upate fursa ya kufaidika nazo huku ukiboresha maisha yako.
Latest