Mahakama ilivyomaliza mzozo mpaka wa Kenya, Somalia baharí ya Hindi

October 13, 2021 5:16 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

ICJ yatoa mwongozo wa mpaka wa majini kati ya Kenya na Somalia. Picha| ICJ.


  • Ni mpaka uliopo baharini ambao unadhaniwa kuwa na mafuta na gesi.
  • Mahakama ya ICJ  yagawa eneo hilo nusu ili kila nchi ifaidike.
  • ICJ yasema huo ndiyo uamuzi wa mwisho hakuna kukata rufaa.

Dar es Salaam. Hatimaye uMahakama ya Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya haki (ICJ) imefunga kesi ya kugombania mpaka wa baharini kati ya Somalia na Kenya kwa kupitisha uamuzi unaogawa nusu eneo lililokuwa linagombewa.

Eneo hilo la pembetatu katika bahari ya Hindi lina ukubwa wa kilometa za mraba 100,000 na linadhaniwa kuwa na mafuta na gesi ambapo kila upande ulikuwa ukisema ni la kwake.

Hukumu hiyo ya Oktoba 12 iliyoko katika kurasa 79 imepitishwa The Hague, Uholanzi ambapo katika vipengele sita vya kesi hiyo, majaji wamekubaliana kwa kauli moja katika vipengele vinne huku wakipishana katika vipengele viwili tu.

ICJ katika  taarifa yake iliyotolewa mjini The Hague, kwa kauli moja majaji wamekubali hoja ya Somalia ya kwamba hakuna mpaka wa majini kati ya Somalia na Kenya.

Halikadhalika wametupilia mbali hoja ya Somalia kuwa Kenya katika eneo hilo linalogombaniwa, imekuwa ikikiuka wajibu wake kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Mvutano huo umekuwa kitovu cha mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo jirani na kwa kipindi cha miongo minne, Kenya imekuwa inasema upande wa mashariki ambako nchi hizo zinakutana kwa upande wa pwani ndiyo mpaka wa majini huku Somalia ikidai mahakamani kuwa mpaka wa majini unapaswa kufuata mpaka wa ardhini.

Awali Kenya ilishasema kuwa haitakubali uamuzi wowote utakaotolewa janakwa madai kuwa ICJ imekuwa na upendeleo, na tayari mahakama hiyo imesema uamuzi huo ni wa mwisho na hakuna fursa ya kukata rufaa.

Kwa uamuzi huo, mahakama imegawa nusu eneo linalogombaniwa na kwa taarifa ya kuwa Kenya haitokubali uamuzi huo, bado haijafahamika mwelekeo utakuwa ni upi.

ICJ ni moja ya vyombo vikuu vya Umoja wa Mataifa na moja ya majukumu yake ni kutatua migogoro ya mipaka baina ya nchi wanachama wa Umoja wa huo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW