Rais Samia afanya uteuzi
- Amemteua Profesa Othman Chande Othman kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS.
- Amemteua Dk Kalimwage Mlimuka kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC).
Dar es Salaam. Huenda sikukuu za mwisho wa mwaka zikawa chungu na tabasamu kwa baadhi ya viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali baada Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko katika taasisi hizo.
Rais Samia amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo Profesa Othman Chande Othman kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Prof Othman ambaye alikuwa Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anachukua nafasi ya Dk Fenella Mukangara ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu katika taarifa yake iliyotolewa leo Desemba 23, 2021 amesema pia Rais Samia amemteua Dk Kalimwage Mlimuka kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani (FCC).
“Dk Mlimuka anachukua nafasi ya Prof Humphrey Moshi aliyemaliza muda wake. Dk Mlimuka ni Mkurugenzi Mstaafu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE),” amesema Haniu katika taarifa hiyo.
Aidha, Dk Andrew Kutua ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) akichukua nafasi ya Dk Deudatus Mtasiwa ambaye amemaliza muda wake.
Uteuzi huo umeanza leo Desemba 23, 2021.
Latest