Mkuranga walivyojipanga kuongeza matumizi ya nishati mbadala

February 1, 2022 1:45 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanakusudia kuongeza elimu ya nishati hiyo kwa wananchi.
  • Pia watajenga kituo cha maalum cha mafunzo ya nishati mbadala.
  • Wadau wa nishati wasisitiza madiwani kuwa mfano.

Dar es Salaam. Tofauti na wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam waliofikiwa na umeme kwa asilimia 100, asilimia 14.2 ya wakazi wa Mkoa wa Pwani wapo kwenye kiza kinene kwa kukosa umeme kabisa.

Ripoti ya Hali ya Upatikanaji na Matumizi ya Nishati Tanzania Bara ya mwaka 2020 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ikishirikiana na Wakala wa umeme vijijini (REA) inaeleza kuwa, asilimia 85 ya wananchi wa Mkoa wa Pwani wamefikiwa na nishati ya umeme.

Hali hiyo inachochea kuendelea kwa matumizi ya nishati zisizo safi na salama ikiwemo mkaa na kuni na kuwaweka wananchi katika hatari ya kupata athari za kiafya na kiuchumi.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wamesema kinachosababisha matumizi ya nishati hizo ambazo siyo rafiki kwa mazingira ni kukosekana kwa elimu ya nishati mbadala kwa wananchi wa Mkuranga.

Ili kudhibiti hali hiyo, Madiwani hao wamesema moja ya suluhu ya hali hiyo ni kuendelea kutoa elimu kwa wakazi wa Mkuranga ili waangazie nishati mbadala ikiwemo biogesi na umemejua.

Kutoka kulia, Katibu Mtendaji Tangsen, Hezron Kajange Diwani wa kata ya Tengelea, Shabani Manda (kati kati) na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Dk Mbikilwa Ally  (kushoto). Picha| Rodgers George.

Elimu itasaidia?

Madiwani wa halmashauri hiyo wametoa mapendekezo yao kuongeza matumizi ya nishati mbadala wilayani humo wakati wa mkutano uliofanyika jana (Jumatatu, Januari 31 2022) baina ya Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Baraza la Madiwani ya uchumi, ujenzi na mazingira ulioandaliwa na Mtandao wa Nishati na Jinsia Tanzania (Tangsen).

Akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz), Diwani wa Kata ya Tambani wilayani humo, Dickson Mwaisibe amesema shughuli za uzalishaji za zinahitaji nishati ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na wakijua teknolojia za kuwasaida, watazitumia.

Mwaisibe amesema wengi wao wamejikita kwenye kufyatua matofali, ufugaji, ushonaji na viwanda vidogo vya usindikaji na wanatumia teknolojia zinazowapatia uzalishaji mdogo.

Ukosefu ya nishati ya umeme unasababisha kutokuwepo kwa ufanisi katika uzalishaji wa kazi hizo ikilinganishwa na wazalishaji wa sehemu zingine zenye umeme ikiwemo Dar es Salaam.

“Mahitaji ya nishati kwa wana Tambani ni makubwa. Kuna baadhi ya sehemu hazina umeme kabisa hivyo wanabaki wakitegemea kuni na mkaa, nishati ambazo ni mbaya kwa mazingira,” amesema Diwani Mwaisibe.


Soma zaidi:


Vitengenezwe vituo vya mafunzo

Mwenyekiti Kamati ya Uchumi na Mazingira  ambaye ni Diwani wa kata ya Tengelea, Shabani Manda amesema katika mkutano huo ya kuwa, ipo haja ya kuwepo kwa kituo cha kujifunzia ambacho madiwani wamependekeza kiwe kata ya Njia Nne kwa ajili ya kufikika kiurahisi.

“Ukifanyika utaratibu ikawepo centre (kituo) ya kujifunzia, baada ya muda mchache tutakuwa na wadau wengi watakaochagua nishati safi,” amesema Manda.

Naye Diwani wa kata ya Kipalang’anda Shomari Mwambala amesema uwepo wa kituo  hicho utasaida madiwani kujua nini cha kuwaeleza wananchi wao pale wanapokwenda kuwapatia elimu.

Madiwani wa Mkuranga wameshauri elimu iendelee kutolewa kwa wakazi wa Mkuranga. Picha| Rodgers George.

Ianze na Madiwani kuweka mikakati

Mafanikio yote huanza na mipango. Endapo madiwani watapanga kufikia malengo fulani kuongeza matumizi ya inishati safi na salama itasaidia watu wengi kutumia nishati hiyo katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Afisa Programu kutoka Tangsen, Thabit Mikidadi amesema, endapo kila diwani ataweka mpango wa kuhakikisha wakazi wa kata yake wanatumia teknolojia za nishati zilizoboreshwa, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia malengo ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

“Kila mmoja wetu humu ndani akiazimia watu wake watumie majiko banifu walau kwa asilimia 90, tutafanikiwa. Kwa hiyo tutazungumza yote lakini mabadiliko yanaanza na sisi humu ndani,” amesema Mikidadi.

Mikidadi amesema Tangsen iko tayari kuongea na wadau ili kufanikisha utolewaji wa elimu ya tekolojia za nishati mbadala kwa madiwani na baadhi ya wakazi wa Mkuranga ili wahamasike kutumia nishati hizo katika uzalishaji na kupikia majumbani.

“Wanaohusika na teknolojia hizi ni wafanyabiashara tukiwaambia waje kuonyesha biashara zao, wengi wapo tayari kufanya hivyo,” amesema Mikidadi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW