Guterres: Itakuwa kosa kubwa kuamini Uviko-19 umeisha

March 10, 2022 8:19 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link
  • Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema Corona bado ipo.
  • Asisitiza usawa katika upatikanaji wa chanjo duniani.
  • Watu miloni 6 wafariki kwa ugonjwa huo duniani.

Dar es Salaam. Ni zaidi ya miaka miwili sasa tangu janga la Corona (Uviko-19) liikumbe dunia na kuathiri shughuli mbalimbali za binadamu, pamoja na kugharimu maisha ya watu zaidi ya milioni 6 duniani, ugonjwa huo bado upo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kuwa itakuwa ni kosa kubwa endapo dunia itadhani kuwa ugonjwa huo umekwisha.

Katika taarifa yake iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Machi 9, 2022 amesema kuwa  jitihada za kiafya na utengenezaji wa kasi kubwa wa chanjo katika maeneo mengi ya dunia unahitajika ili kuhakikisha kuwa ugonjwa huo unadhibitiwa.

Kutokana na ukosefu wa usawa katika kusambaza chanjo za Uviko-19, Guterres amesema kuwa ni muhimu kuondoa matabaka katika kujikwamua kutoka katika gonjwa hilo.

“Mgao wa chanjo unasalia usio na uwiano. Watengenezaji wanazalisha dozi bilioni 1.5 kila mwezi lakini watu bilioni 3 duniani kote bado wanasubiri dozi yao ya kwanza,” amesema Guterres.

Guterres ameongeza kuwa hali hiyo inatokana na uamuzi usio sahihi wa kisera na kibajeti ambao unatoa kipaumbele afya za watu kwenye nchi tajiri na kusahau nchi maskini.


Zinazohusiana:


Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa mwelekeo huo ni kosa la kimaadili kwa dunia na pia ni kichocheo cha kuibuka kwa lahaja nyingine za virusi na kusababisha pia watu kuendelea kuwekwa karantini.

 “Hii italeta machungu kwa kila nchi,” amesema Guterres.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi Machi 6, 2022, zaidi ya watu milioni 448 walikuwa wameambukizwa Uviko-19 duniani, zaidi ya milioni 6 wakipoteza maisha, huku zaidi ya dozi za chanjo bilioni 10 za ugonjwa huo zikitolewa duniani.

Guterres anakumbusha kuwa licha ya majanga mengine yanayoikumba dunia, ni muhimu kufikia lengo la kuchanja asilimia 70 ya wakazi wa dunia dhidi ya Uviko-19 ifikapo katikati ya mwaka huu wa 2022.

Kufikia lengo hilo ni lazima kuwepo na mshikamano kati ya kampuni za kutengeneza dawa na serikali ili kuongeza idadi ya nchi zinazoweza kutengeneza vifaa vya uchunguzi, chanjo na tiba, ushirikiano ambao amesema utawezesha kuongeza leseni na hataza za uzalishaji wa dawa na chanjo hizo.

Kwa sasa tayari kuna nchi barani Afrika ambazo zimeanza mchakato wa kutengeneza chanjo za ugonjwa huo ikiwemo Afrika Kusini na Rwanda.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW