CAG azidi kuchokonoa vitambulisho vya NIDA

April 20, 2022 1:55 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • CAG abaini kuwa mamlaka hiyo ilizalisha vitambulisho milioni 1.7 kati ya milioni 13.9 mwaka 2020/21.
    Asema kutofikiwa kwa malengo yaliyowekwa kunaongeza hatari ya Serikali kushindwa kuwatambua raia wake.

Dar es Salaam. Huenda Watanzania wakaendelea kusubiri kwa muda mrefu kupata vitambulisho vya Taifa baada ya ripoti ya CAG kubaini kasi isiyoridhisha ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika uzalishaji na utoaji wa vitambulisho vya Taifa. 

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere kuhusu Serikali Kuu ya mwaka 2020/21 imeeleza kuwa katika mapitio ya Mpangokazi wa Mwaka wa NIDA (2020/21) pamoja na taarifa za ufuatiliaji za robo mwaka amebaini kuwa mamlaka hiyo ililenga kuzalisha vitambulisho vya Taifa milioni 13.9 lakini ilizalisha milioni 1.7. 

NIDA ilishindwa kufikia lengo la uzalishaji wa vitambulisho vya Taifa milioni 12.2 sawa na asilimia 88 chini ya lengo husika.

Hiyo ni sawa kusema takriban vitambulisho 9 kati ya10 vilivyotarajiwa kuzalishwa mwaka 2020/21 havikuzalishwa huku baadhi ya vilivyozalishwa havikuwafikia walengwa.

“Pia, kati ya vitambulisho milioni 1.7  vilivyozalishwa, NIDA ilisambaza vitambulisho milioni 1.5 kwa wananchi waliojiandikisha, hivyo kushindwa kusambaza vitambulisho 242,544,” amesema CAG katika ripoti hiyo.

Katika mwaka 2020/21, NIDA ililenga kuzalisha nambari za vitambulisho vya Taifa milioni 1.9 lakini CAG amebaini ilifanikiwa kuzalisha nambari milioli 1.1 pekee sawa na asilimia 44. 


Soma zaidi: 


“Zaidi ya hayo, nilibaini kuwa utendaji kazi usioridhisha ulitokana na kutumia kadi za awamu ya kwanza kwenye printa zinazoruhusu kadi za awamu ya pili, pamoja na kukosekana kwa matengenezo ya mara kwa mara kwa mashine za kutengeneza vitambulisho,” amesema CAG.

Mathalan, katika kituo NIDA cha kuzalisha vitambulisho cha Kibaha mkoani Pwani, mashine tatu za kuzalisha vitambulisho zilizonunuliwa kutoka kampuni ya IRIS Co. Behard zilikuwa hazitumiki, hasa wakati wa ukaguzi wa CAG wa Desemba 2021.

“Ni maoni yangu kuwa kutokufanya matengenezo ya mashine kunaongeza hatari ya mashine husika kuharibika na hivyo kuathiri utengenezaji wa vitambulisho vya Taifa,” amesema CAG. 

Kitambulisho cha Taifa ni moja ya nyaraka muhimu kwa sasa Tanzania kwa sababu hutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo huduma za kifedha, usajili wa biashara na utambuzi wa watu.

Kwa mujibu wa CAG, kutofikiwa kwa malengo yaliyowekwa kunaongeza hatari ya Serikali kushindwa kuwatambua raia wake, pamoja na kushindwa kupata taarifa zao kwa matumizi mbalimbali. 

“Ninapendekeza NIDA kuhakikisha kuwa mashine za kuzalisha vitambulisho zinatengenezwa kwa mujibu wa ratiba za matengenezo na pia iboreshe ubora wa kufanya shughuli zake ili malengo yaliyowekwa na Taasisi yatimie kama yalivyopangwa,” amependekeza.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW