Rais Magufuli kuzuru Mwanza, Simiyu na Mara kwa siku saba
Wananchi wa Mwanza katika uzinduzi wa daraja la watembea kwa miguu la furahisha uliofanywa na Rais John Magufuli.
- Ziara hiyo inatarajiwa kuwa ya siku saba akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
- Ni fursa kwa mkoa wa Mara ambao unatembelewa kwa mara ya kwanza tangu Rais Magufuli aingie madarakani.
- Baada ya ziara hiyo, mikoa ya Katavi, Rukwa , Songwe na Mbeya wajiandae kumpokea Rais.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku saba katika mikoa ya Mwanza, Simiyu na Mara inayolenga kukagua, kufungua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo.
Ziara hiyo inayoanza Septemba 3 na kumalizika Septemba 10, 2018 itakuwa ni ya fursa ya kwanza kwa wakazi wa Mara kutembelewa na kiongozi huyo wa juu wa Taifa tangu alipochaguliwa kuingia madarakani Novemba 2015.
Katika ziara alizofanya katika mikoa mingine nchini, Rais amekuwa akitoa fursa kwa baadhi ya wananchi kueleza kero zao katika mikutano ya hadhara au anaposimamishwa kwenye msafara na kisha kuagiza viongozi kuzitatua kero hizo haraka iwezekanavyo.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotolewa leo (Agosti 30, 2018) inaeleza kuwa taarifa za kina kuhusu ziara hiyo zitatolewa na viongozi husika wa mikoa hiyo atakayozuru.
Tayari Rais Magufuli alishawahi kufanya ziara katika mikoa ya Mwanza na Simiyu na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mara ya mwisho Rais Magufuli kutembelea Simiyu ilikuwa Januari 12, 2017 alipoweka jiwe la msingi katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu iliyopo Halmashauri ya Mji wa Bariadi na baadaye alifungua barabara ya Lamadi hadi Bariadi yenye kilomita 72.
Mwanza umekuwa na bahati ya kutembelewa zaidi na Rais Magufuli ambapo katika ziara zizolivuta hisia za watu wengi ilikuwa ile ya Oktoba 30, 2017 alipofungua daraja la juu la watembea kwa miguu lilipo eneo la Furahisha, wilaya ya Ilemela lililojengwa kwa gharama ya Sh4.7 bilioni. Katika ziara hiyo pia alizindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona kilichopo Nyakato Jijini Mwanza.
Hata hivyo, viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali wameshafanya ziara mkoani Mara tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani. Juni 2017 Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kikazi katika mkoa huo na kuongea na wakazi wa maeneo ya mkoa huo, ikiwemo kutembelea Kituo cha Afya cha Nyamagwa wilaya ya Tarime kilichojengwa kwa msaada wa mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya dhahabu ya Acacia Mining Plc.
Ziara za Rais katika mikoa hiyo mitatu inatajwa kuwa ni fursa nyingine kwa wananchi kufaidika na fursa mbalimbali za maendeleo ikiwemo sera ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Baada ya ziara hiyo, taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Rais Magufuli anatarajiwa kuzuru pia mikoa ya Katavi, Rukwa, Songwe na Mbeya.
Taarifa kutoka Ofisi ya Rais-IKULU pic.twitter.com/exlD5fhzjc
— Msemaji Mkuu wa Serikali (@TZMsemajiMkuu) August 30, 2018