Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki

September 7, 2018 5:06 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei ya zao hilo itaendelea kushuka kutokana na kuongezeka kwa mavuno na serikali kupiga marufuku kusafirisha mazao nje ya nchini.
  • Wachambuzi washauri wakulima kutumia teknoloji ya Uhandisi Jeni kuongeza mavuno na soko.

Dar es Salaam. Licha wakulima wa mahindi kupata mavuno mengi katika msimu wa 2017/2018, huenda wasifaidike na soko la zao hilo kutokana na kushuka kwa bei katika mipaka ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa ya Biashara ya mipakani ya Afrika Mashariki ya robo ya kwanza ya mwaka 2018 (Januari-Machi), bei ya mahindi itaendelea kushuka mpaka msimu mpya wa kupanda mazao utakapoanza. 

“Mabadiliko ya bei yanategemea kuwa makubwa kuliko mwaka uliopita wakati wakulima na wafanyabiashara wakihifadhi mavuno mapya ghalani kupisha ya zamani,” inaeleza taarifa hiyo. 

Kushuka kwa bei ya mahindi kutoka Tanzania yanayosafirishwa kwenda katika nchi za Afrika Mashariki kumechochewa zaidi na uamuzi wa serikali kuzuia wakulima kuuza mahindi nje ya nchi ili kuepusha mfumuko wa bei na uhaba wa chakula.

Kutokana na hali hiyo sehemu ya shehena ya mahindi ya msimu uliopita bado ipo ghalani jambo linaloleta changamoto kwa mavuno mapya yanayoweza kukosa sehemu ya kuhifadhiwa na soko la uhakika. 

Dalili za kushuka kwa bei ya mahindi zilianza kushuhudiwa tangu robo ya pili ya mwaka huu (AprilI-Juni) ambapo Tanzania ilisafirisha tani 49,421 kwenda Kenya ukilinganisha na tani 76,723 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Kenya ambayo ni muugiza mkubwa wa mahindi kutoka Tanzania, mwaka huu ilipata mvua za kutosha na kuongeza mavuno, jambo linalopunguza uagizaji na ushindani wa bei wa zao hilo. Kwa mfano, kati ya Machi na June, Uganda ilisafirisha tani 59,545 kwenda Kenya ukilinganisha na tani 87,282 zilizosafirishwa kati ya Januari na Machi mwaka huu. 


Zinahusiana: 


Kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania nako kumechangia mabadiliko ya bei ya mazao licha kuwepo kwa juhudi za serikali kuimarisha mzunguko wa fedha ambao kwa kiasi kikubwa umeathiriwa na sera mpya za kodi na kufungwa kwa biashara mbalimbali nchini. 


Nini kifanyike kuwasaidia wakulima?

Wakulima wa mahindi bado wana nafasi nzuri ya kufaidika na soko la mataifa mengine ya Sudan Kusin na Ethiopia ambayo katika msimu uliopita yalikabiliwa na ukame, machafuko ya kisiasa yaliyoziacha nchi hizo katika mzozo wa chakula. 

Ikiwa serikali italegeza masharti na kuruhusu wakulima kusafirisha mahindi nje ya nchi hasa Sudan Kusin, mshirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakulima wanaweza kupata bei nzuri lakini watakabiliwa na ushindani kutoka Kenya na Uganda, Mexico na Ukraine ambao wana mafungamano ya kibiashara na nchi hiyo. 

Kuendelea kuzuia mahindi kutoka nje ya nchi, huenda kushusha bei zaidi na wakulima wakapata hasara kutokana na gharama kubwa walizotumia kulima na kuhifadhi katika maghala. 

Mshauri wa Jukwaa la wazi la Kilimo cha Kibayoteki (OFAB), Dk. Nicholas Nyange anasema hata kama serikali ikiruhusu wakulima kuuza mahindi nje ya nchi haitawainua wakulima kwasababu ziada ya mahindi yanayozalishwa kila mwaka ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa eneo la kilimo tulinalo.

“Inakadiriwa kuwa Tanzania kwa sasa ina watu wapatao milioni 55 na idadi hii inaongezeka kila siku na kama sayansi haitatumika kusaidia kuzalisha chakula cha kutosha basi huenda taifa likasumbuliwa na njaa kila mwaka kwenye maeneo mengi”, anasema Dkt. Nyange.

Kwa mujibu wa Dk. Nyange, Tanzania inazalisha takribani tani  milioni 1.5 hadi tani 2 pale ambapo hali ya hewa na mtawanyiko wa mvua utakuwa mzuri lakini kwa nchi zilizoendelea kama vile Marekani wanazalisha tani 8 hadi 9 kwa ekari moja kutokana na kutumia teknolojia ya kisasa.

Anabainisha kuwa njia pekee iliyobaki ni wakulima kuwezeshwa kutumia teknolojia ya Uhandisi Jeni (Genetically Modified Organism) inayotumika kutengeneza mbegu zilizoboreshwa (Mazao ya Kibayoteki) zinazoongeza uzalishaji wa mazao na soko kwasababu ya uwezo wake wa kudhibiti wadudu waharibifu, magonjwa na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo, Tanzania bado haijaruhusu  kutumia mbegu hizo, lakini utafiti wa mbegu za GMO unaendelea katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Makutopora mkoani Dodoma ambapo ukikamilika utatoa jibu kama wakulima wataruhusiwa kutumia mbegu hizo.

Mahindi ni nafaka inayotemegemewa na watu wengi kama chakula. Picha| Tanzaniatoday.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Chama cha Kibayoteki Tanzania (BST), Dk. Emmarold Mneney anasema kama teknolojia ya uhandisi jeni itaruhusiwa nchini itasaidia kuboresha maisha ya wakulima kama ilivyo kwa mataifa ya Marekani na Brazil ambayo yanatumia teknolojia hiyo kwa muda mrefu sasa. 

Kutokana na mabadiliko na mwenendo wa biashara ya mazao, wachambuzi wa masuala ya kilimobiashara wanaeleza kuwa wakulima wanapaswa kuyageukia mazao mengine kama mpunga na maharage ya soya ambayo soko lake ni la uhakika.


Serikali yajipanga kutafuta soko la kimataifa

Rais John Magufuli anasema  serikali inatafuta soko la mazao hasa mahindi ili kutowavunja moyo wakulima ambao katika msimu huu wamezalisha ziada ambapo nchi ina chakula cha kutosha kinachoweza kuuzwa kwenye nchi zingine.

“Kama kuna chakula kinatakiwa kupelekwa kwa refugees (wakimbizi) kwa nini mkanunue chakula kutoka nje huko Ulaya na kukisafirisha kwa gharama kubwa, si chukua hapa tu Songea,” alinukuliwa Rais Magufuli wakati alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Beasley Ikulu Jijini Dar es Salaam Julai 26, 2018.  

Enable Notifications OK No thanks