Elimu chanjo ya Uviko-19 inahitajika zaidi mipakani Tanzania
- Muamko wa wafanyabiashara na madereva malori uko chini.
- Dhana potofu na ukosefu wa elimu vyachangia.
- Serikali yaanza kampeni maalum kuongeza hamasa.
Songwe. Ni asubuhi na mapema katika kituo cha forodha kilichopo Tunduma katika mpaka wa Tanzania na Zambia mkoani Songwe.
Rashidi Musa (45), dereva roli ametoka kukaguliwa nyaraka zake akiwa amevalia tisheti yenye mchanganyiko wa rangi ya bluu na nyeupe anaingia katika gari lake kuanza safari ya kwenda Zambia.
Baada ya kufika ndani ya gari, Rashidi anaiondoa barakao yake ambayo alikuwa ameivaa wakati wote akiwa anakaguliwa na yeye mwenyewe anasema hiyo ni tahadhari ya muhimu kwake kutokana na uwepo wa janga la Uviko-19.
“Ugonjwa upo lakini tahadhari tunachukuliwa ikiwemo kuepuka kwenda kwenye mkusanyiko kama unalazimika kwenda mikusanyikoni basi tunavaa barakoa pamoja na kutumia vitasa mikono ambapo itakusaidia kujikinga na maambukizi” anasema Rashidi.
Mbali na uvaaji barakoa, kutumia vitakasa mikono na kuzingatia umbali, suala la chanjo ni miongoni mwa afua muhimu za kijikinga na janga la Uviko-19.
Mtihani uliobaki kwa Rashidi ni kuchanjwa chanjo ya ugonjwa huo. Mpaka sasa hajafanya uamuzi kwa sababu anatafakari kuhusu chanjo hiyo na faida zake.
“Chanjo mimi bado sijaipokea kwasababu kila mtu anaamini kwa jinsi anavyoona kwamba chanjo ina faida au hasara kwangu hivyo bado sijapewa matumaini kuwa chanjo inaweza kunisaidia,” anasema Rashidi.
Pamoja na kuwepo kwa watu kama Rashidi ambao wanachelewa kuchukua maamuzi, Serikali imeendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kuikubali chanjo ili wajikinge na ugonja huo.
Dereva wa gari la mizigo kutoka Tanzania kuelekea nchini Congo, Sospeter Kifutumo anasema mbali na kwamba hajapata elimu ya kutosha kuhusu chanjo lakini hutumia njia za asili zaidi kujikinga na Uviko-19.
“Mimi huwa natumia juisi ambayo nimechanganya kitunguu saumu, tangawizi pamoja na limao ambapo natengeneza mchanganyiko wa lita moja ninaoweza kuutumia kwa siku tatu hadi nne” anasema Kifutumo.
Endapo atapa elimu ya kutosha ya chanjo na masharti ya kuchanjwa yataongezeka katika nchi anazokwenda atalazimika kuchanja la sivyo ataendelea kutumia njia za asili ambazo anasema anaziamini.
“Kinachofanyika hivi sasa ni kupima na kupata cheti kwani tumekuwa na mizunguko mingi, tangu nianze kutumia njia hii ya asili sijawahi kupimwa na kukutwa na maambukizo,” anasema dereva huyo, rais wa Tanzania.
Madereva wa maroli ni miongoni mwa watu wanaotakiwa kuwa mstari wa mbele kupata chanjo ya Uviko-19 kwa sababu kuzunguka katika nchi mbalimbali. Picha| Isakwisa Mbyale.
Kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu mpakani hapa bila shaka wakazi hawa wanahitaji kujiweka salama kwa kupokea chanjo ambayo wataalamu wa afya wanasema inasaidia kupunguza makali ya Uviko-19 endapo mtu ataambukizwa.
Wakazi hawa ambao wengi ni wafanyabiashara wanasema bado hawajapata ufahamu wa kutosha kuhusiana na umuhimu wa kupokea chanjo ingawa wachache wao tayari wanaufahamu kidogo.
“Chanjo ingekuwa inasaidia kwamba ukisha chanjwa mara moja tu hautapata tena maambukizo ingekuwa afadhali lakini inasemekana ukichanjwa bado unaweza kupata na hili ni wimbi la tatu,” anasema Neema Nzunda, mfanyabiashara katika mpaka wa Tunduma.
Hata hivyo, Neema anachotakiwa kufahamu ni kuwa chanjo inamuongezea kingamwili ambayo itaweza kupambana kingamilifu na ugonjwa huo na hata akipata maambukizi hawezi kuugua hadi katika hatua ya kulazwa hospitali.
Jamii inapaswa kufahamishwa faida na hasara za kila uamuzi watakaouchukua kuhusiana na chanjo.
“Kwa sisi bado hatujapata elimu, tunataka elimu kwamba nikichanjwa kuna faida gani na nisipo chanjwa kuna hasara gani,” amesema Sibonike Moses, mfanyabiashara katika mpaka huo wa Tunduma.
Utoaji chanjo ukoje Tunduma?
Kutokana na muingiliano mkubwa wa watu mpakani, Serikali imeweka kituo cha kutolea chanjo mpakani hapo ili kutoa fursa kwa watu kuchanjwa na kujikinga na ugonjwa huo.
Afisa afya katika kituo cha forodha cha Tunduma, Meshack Msuku anasema licha ya kwamba eneo hilo limetengwa kwa ajili ya kuwapa fursa madereva na wakazi wanaotumia kituo hicho kupata chanjo lakini bado mwamko wa watu kupokea chanjo ni mdogo kutokana na kutokuwepo kwa elimu ya kujitosheleza.
“Kuhusiana na mwamko wa chanjo ya Corona ni mdogo sana kwa takwimu mpaka sasa saa 11:00 jioni hakuna hata mtu mmoja amekuja kuchanja,” anasema Msuku.
Jengo la forodha katika mpaka wa Tunduma mkoani Songwe ambalo hutumika kwa ukaguzi wa madereva na kutoa huduma za chanjo ya Uviko-19. Picha| Isakwisa Mbyale.
Wadau, Serikali waingilia kati
Licha ya kuwa suala la kuchanja ni hiari, wadau wa masuala ya afya na elimu wanasema kuna haja Serikali na taasisi za kijamii kuungana na kutumia mbinu mbadala za ushawishi ili kuongeza idadi ya watu wanaopata chanjo.
“Serikali iongeze uelimishwaji kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo kupitia vyombo vya habari na kutumia watu wenye ushawishi kama wasanii,” anasema Festo Sikagonamo, Mkurugenzi wa shirika la Elimisha la mkoani Mbeya.
Jitihada za kuhakikisha umma wa Watanzania unapata elimu sahihi ya chanjo zinaendelea kufanywa na Serikali ili kuongeza idadi ya watu wanaopata chanjo hiyo na kuwaepusha na upotoshaji unaofifisha jitihada hizo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dk Hamad Nyembea anasema katika mkoa wake umekuwa na mwitikio wa wastani wa watu kupokea chanjo kama njia ya kukabiliana na Uviko-19.
Ili kuongeza idadi ya watu wanaopata chanjo, Dk Nyembea anasema wameweka mikakati ya kuhakikisha elimu inafika kwa jamii, na kuongeza idadi ya vituo vya kutolea chanjo.
“Mwanzoni wakati tunaanza kutoa chanjo kila halmashauri ilikuwa na vituo vitatu pekee lakini sasa vituo vimekuwa vingi ambapo kuna baadhi ya halmashauri wana vituo mpaka 10 lakini sisi tunaendelea kutoa elimu kwa kuwa ndiyo afua namba moja,” anasema Dk Nyembea.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi anasema wanashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi ili kuongeza kasi ya utoaji chanjo kwa watu.
“Tulikua tumeshafikia kiwango cha kuchanja wananchi 50,000 kwa siku kabla chanjo ya JJ haijaisha, sasa tunaendelea kutoa chanjo ya Sinopharm yenye dozi mbili, hivyo wananchi waitikie kuchoma chanjo hiyo. Kama Serikali tumeona tuwashirikishe wadau katika kutoa elimu,” anasema Prof Makubi.
Hata hivyo, Serikali tayari imeanza mchakato wa kutengeneza chanjo ya Uviko-19 hapa nchini itakayokidhi mahitaji ya ndani.
“Sasa hivi tumeanza kutengeneza chanjo yetu dhidi ya Uviko-19 kwa kushirikiana na sekta na tupo makini kwenye hili, endapo tutafanikiwa kwenye chanjo tutakua tumefanikiwa kwenye sekta binafsi,” anasisitiza Prof Makubi.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest