Wavuvi watahadharishwa kupungua samaki Ziwa Victoria
- Hali hiyo inatokana na mabadiliko ya mwenendo wa mvua, upepo na joto la bahari.
- Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yawataka kuchukua tahadhari na kupata ushauri kwa wataalamu wa uvuvi.
- Uvuvi ni moja ya shughuli kuu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na mauzo ya samaki kutoka Ziwa Victoria huchangia Sh1.48 trilioni kwa mwaka.
Dar es Salaam. Licha ya Ziwa Victoria kuwa chanzo muhimu kwa mazao ya samaki nchini, huenda mapato ya baadhi ya wavuvi wa ziwa hilo yakapungua katika kipindi cha miezi mitatu ijayo kutokana na mabadiliko ya mfumo wa hali ya hewa yanayotarajiwa kutokeo katika eneo la maziwa makuu.
Mfumo huo unahusisha mabadiliko ya mwenendo wa mvua, joto na upepo ambao unatokea katika maeneo yanayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka likiwemo eneo la Magharibi mwa Ziwa Victoria hasa katika mikoa ya Kagera na Geita.
Taarifa ya mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2018, iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaeleza kuwa eneo la Magharibi mwa Ziwa Victoria litapata mvua za kawaida na zinaweza kuathiri upatikanaji wa samaki kutokana na kupungua kwa chakula chao.
“Hata hivyo upungufu wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori, ufugaji samaki, kupungua kwa samaki katika maji ya asili kutokana na kupungua kwa chakula cha samaki unaweza kujitokeza katika maeneo machache ya Magharibi mwa Ziwa Victoria,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi katika taarifa hiyo.
Dk Kijazi amesema kuwa mvua hizo zitakuwa za kawaida lakini zitapungua kuelekea Novemba na kusababisha ukavu katika baadhi ya maeneo na kwamba mvua za wastani na vipindi vya mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera, Geita na wilaya ya Kibondo.
Anabainisha kuwa hali hiyo itasababisha pia kupungua kwa unyevunyevu kwenye udongo na kuongezeka kwa joto katika maeneo hayo na kusababisha matokeo hasi katika mfumo wa mazalia ya samaki.
“Upungufu wa unyevunyevu unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani,” amesema na kuongeza kuwa hali hiyo itategemea zaidi joto la bahari na kuvuma kwa upepo kutoka misitu ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Taarifa ya TMA inaeleza kuwa mwenendo wa mvua hutegemea zaidi joto la bahari ya Hindi na Pasifiki na msukumo wa upepo kutoka kwenye eneo la bahari kuu na hali ya misitu ya Congo DRC ambayo iko karibu na Kanda ya Ziwa.
“Aidha, matukio ya Vimbunga yanayotarajiwa kujitokeza katika eneo la Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi sambamba na hali ya joto la chini ya wastani katika eneo la pwani ya Angola, vinatarajiwa kuchochea msukumo wa upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo katika maeneo mengi,” inaeleza sehemu ya taarifa ya TMA.
Chanzo: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Madhara hadi kwa wafuga samaki
Kutokana na hali hiyo, wavuvi wa eneo la Magharibi mwa Ziwa Victoria, wanashauriwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa uvuvi ili kukabiliana na hali hiyo ya kupungua mvua na samaki. Athari za msimu huo zitawagusa hadi wale wanaofuga samaki kwenye mabwawa.
Hata hivyo, wavuvi wa maeneo mengine katika ziwa hilo huenda watafaidika na ongezeko la mazalia ya samaki kwa sababu watapata mvua nyingi na ongezeko la unyevunyevu kwenye udongo.
Pamoja na neema hiyo kwa baadhi ya wafugaji na wavuvi, wanapaswa kuchukua tahadhari kwa sababu ya magonjwa ya wanyama na upotevu wa samaki kutokana na uharibifu wa miundombinu ya kufugia samaki unaoweza kujitokeza kutokana na mvua za wastani na juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo.
Kwa muda mrefu wavuvi wamekuwa wakitegemea Ziwa Victoria kama sehemu ya kujipatia kipato kwa kuvua samaki ambao wanauzwa katika masoko yaliyopo ndani na nje ya nchi. Lakini mabadiliko haya hali ya hewa yanaweza kuwaweka katika wakati mgumu kwa kukosa mazao ya uhakika ya samaki.
Uvuvi huchangia ajira kibao
Taasisi ya Uvuvi wa Ziwa Viktoria (LVFO) iliyo chini ya Jumuiya Afrika Mashariki (EAC) inaeleza kuwa kuna wavuvi 200,000 na mitumbwi 60,000 na kila mwaka vyombo 2,000 vipya vinaingia katika ziwa hilo kwa shughuli za uvuvi, ikiwa ni sehemu ya kujipatia kipato.
Maeneo mengi ya ziwa hilo sasa samaki hawawezi kuishi kutokana na uchafuzi na sumu mbalimbali za viwanda na shughuli za kilimo zikiwamo mbolea na madawa ya pamba na kuhitaji usimamizi makini.
Uvuvi ni moja ya shughuli kuu katika ukanda wa ziwa nchini baada ya Shirika la chakula Duniani (FAO) kukisia kuwa zaidi ya watu 280,000 wameajiriwa katika shughuli za uvuvi zikiwamo wavuvi, waanika samaki, wakaanga samaki, wanunuzi na wachuuzi wa samaki, watengeneza nyavu, wajenzi wa mitumbwi na wafanya matengenezo ya mitumbwi.
Viwanda zaidi ya kumi vimejengwa kuchakata samaki kwenye Ziwa Victoria ambao huwasafisha, kuwakata kwenye minofu, kuwaweka kwenye maboksi na kuwasafirisha samaki nje, ambapo kwa mujibu wa LVFO zaidi ya Dola za Marekani 650 milioni (Sh1.48 trilioni) hupatikana kutokana na mauzo ya samaki na mzao yake kila mwaka.