Wakulima Tanzania kufaidika na fursa ya uhaba wa chakula duniani?

September 21, 2018 7:38 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Katika msimu wa 2017/2018 wakulima wamezalisha ziada ya mahindi yanayofikia tani 970,000.
  •  Nchi 39 zikiwemo za Kusini na Mashariki mwa Afrika zina uhitaji mkubwa wa chakula.
  •  Ubora ukizingatiwa, wakulima watafaidika na soko la kimataifa.

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuzuia usafirishaji wa mahindi nje ya nchi, bado wakulima wana nafasi ya kufaidika na fursa ya uhaba wa chakula unaotokea katika maeneo mbalimbali duniani ikiwa watawekewa utaratibu mzuri wa kibiashara.

Hilo linawezekana ikizingatiwa kuwa mapigano na mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea duniani hasa katika nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika yamesababisha maeneo hayo kukosa chakula cha kutosha na kuzidisha njaa kwa wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Chakula ya mwaka 2018 iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kati ya nchi 39 zenye uhaba wa chakula, 31 zinatoka Afrika, saba za Asia na moja (Haiti) zinahitaji msaada wa chakula ili wananchi wake waendelee kuishi.

Baadhi ya nchi hizo ni Kenya, Burundi, Uganda, Sudan, Sudan Kusini na Congo DRC ambazo zote zina mafungamano ya karibu ya kibiashara na Tanzania yanayounganishwa na uwepo wa bandari ya Dar es Salaam na reli ya kati na TAZARA.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa hali ya watu wanaohitaji chakula itaongezeka zaidi ikizingatiwa kuwa ongezeko la uzalishaji wa nafaka ni dogo kuweza kuhimili mahitaji yote duniani.  “Mwaka 2017, idadi ya watu ambao hawakupata chakula cha uhakika ilikadiriwa kufikia 821 milioni sawa na mtu mmoja kati ya 9 duniani,” inaeleza ripoti hiyo.

Hata hivyo, katika ripoti hiyo Tanzania haijatajwa kuwa na upungufu wa chakula kwasababu katika msimu wa 2017/2018 wakulima wamelima mazao mengi ambayo yako ghalani yakisubiri wananunuzi.


Zinazohusiana:


Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Vumilia  Zikankuba amesema ziada ya mazao yote yaliyozalishwa na wakulima msimu huu imefikia tani 2 milioni huku ziada ya mahindi pekee ni tani 970,000.

Amebainisha kuwa NFRA imetengewa Sh15 bilioni kwa ajili ya kununua tani 28,000 kwa awamu ya kwanza ikiwa ni asilimia 2 tu ya ziada ya mahindi iliyopo.

Hiyo ina maana kuwa wakulima bado wana ziada ya mahindi yanayofikia asilimia 98 ambapo NFRA haiwezi ikanunua mahindi yote yaliyobaki kwasababu mahindi yanayonunuliwa ni kwa ajili ya dharura kama kumetokea majanga kama mafuriko, njaa, tetemeko na majanga mengine ambayo wanachi watahitaji msaada wa chakula.

Ikiwa serikali itafungua milango na kuwawekea utaratibu mzuri wakulima kuuza mahindi katika nchi zenye migogoro na uhitaji mkubwa wanaweza kufaidika zaidi na bei ya soko la kimataifa na kujipatia faida ili kufidia gharama za uzalishaji wa mazao hayo.

Shirika la World Vision linaeleza kuwa takribani watu 22 milioni wa Afrika Mashariki wanahitaji msaada wa chakula ambapo watoto 9 milioni wana changamoto ya lishe. Idadi kubwa ya watu hao wanatoka katika nchi za South Sudan, Somalia, and Ethiopia ambako wanakabiliwa na changamoto ya machafuko ya kisiasa na ukame.

Lakini changamoto iliyobaki ni kuhakikisha mahindi ya wakulima yakidhi viwango vya ubora unaohitajika katika soko la kimataifa.

“Haiwezekani NFRA itumia fedha za Serikali kununua mahindi yasiyokidhi viwango vya ubora na machafu kutoka kwa wakulima. Hivyo wakulima wanapaswa kuzalisha mahindi kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyokidhi vigezo vya soko,” amesema Zikankuba.

Kwa muda mrefu wakulima nchini wamekuwa wakilima mazao kwa njia za kienyeji kutokana na kukosa uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ya kuzalisha mazao bora yanayoweza kushindana katika soko la kimataifa.

Mahindi ambayo hayana ubora yakitunzwa kwa muda mrefu ghalani yanakuwa na nafasi kubwa ya kupata vimelea vya fangasi ambao husababisha uwepo wa sumu kavu katika nafaka hiyo ambayo ni hatari sana kwa afya ya mlaji.

Tatizo hili kwa kiasi kikubwa, linaweza kuepukika kwa mkulima kwa kufuata mbinu bora za kilimo, mbinu bora za utayarishaji nafaka na mbinu bora za kuhifadhi nafaka baada ya kuvuna.  

Upatikanaji wa chakula cha kutosha na cha uhakika ni nguzo muhimu ya kuimarisha afya za watu. Picha| imtfi.

Enable Notifications OK No thanks