Wanafunzi waliodanganya mtihani darasa la saba, kikaangoni tena wiki ijayo
- Wanafunzi hao ni wale ambao shule zao zimehusika na udanganyifu na wizi wa mitihani iliyofanyika Septemba mwaka huu.
- NECTA yafuta vituo 7 vya mitihani mpaka itakapojiridhisha kuwa havitakiuka tena kanuni za mitihani.
- Waziri Jaffo amesema waliohusika katika udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba watachukuliwa hatua kali.
Dar es Salaam. Wahitimu wa mtihani wadarasa la saba katika baadhi ya shule nchini watalazimika kurudi mtihani huo wiki ijayo, baada ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kufuta matokeo ya shule hizo kutokana na vitendo vya udanganyifu.
Uamuzi huo uliotolewa na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde, huenda ukawaathiri wanafunzi ambao tayari wako nyumbani na wanasubiri kujiunga na elimu ya sekondari mwaka 2019.
Kwa mujibu wa Dk Msonde, shule ambazo zitafanya tena mtihani huo Septemba 8 na 9, 2018 ni shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Nchemba mkoani Dodoma; Hazina na New Hazina (Kinondoni), Fountain of Joy na Aniny Nndumi (Ubungo); Aliance, New Aliance na Kisiwani (Jiji la Mwanza) na Kondoa Integrity (Kondoa).
Wanafunzi hao wana siku 6 tu za kujiandaa kuingia tena katika mtihani huo ili kutetea elimu yao ambayo wamesota kwa miaka saba mfufululizo.
Aidha, NECTA imebainisha kuwa ili kuzuia udanganyifu usitokee tena wanafunzi hao watafanya mitihani ya marejeo katika vituo vingine tofauti na walivyofanya awali.
Wanafunzi wa shule za msingi za Hazina na New Hazina watafanyia shule ya msingi Osterbay, wakati wale wa Fountain of Joy na Aniny Nndumi watafanyia shule ya msingi Mbezi.
Shule ya msingi Kakebue itakuwa mbadala wa shule ya msingi kisiwani, shule ya msingi (Alliance na New Alliance) huku shule ya msingi Kondoa Integrity mbadala wake ni shule ya msingi Bicha.
Hata hivyo, NECTA imeenda mbali na “Kufuta vituo vya mitihani vya Hazina na New Hazina; Fountain of Joy na Aniny Nndumi; Alliance na New Alliance na Kondoa Inegrity hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa havitakiuka tena kanuni za mitihani.”
Zinazohusiana:
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri.
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari.
- Udanganyifu mitihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kuthibitika kuwepo kwa taarifa za wizi wa mitihani katika vituo hivyo ikiwamo waalimu wa shule za Alliance kukutwa na mitihani kwenye simu zao za mikononi na kubainisha kupata mitihani hiyo kutoka kwa waalimu ya shule ya msingi Aniny Nndumi.
Matukio mengine yaliyoonyesha udanganyifu ni pamoja na wanafunzi kukamatwa wakiwa wameandika majibu kwenye mapaja na kwenye mapindo ya fulana zao wakati mtihani wa hesabu ukiendelea kufanyika.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kisiwani walimtaja Mwalimu Mkuu kuwa aliwapatia majibu kabla ya mtihani kuanza.
Baraza hilo limeweka wazi kuwakamata wahusika wote wa udanganyifu huo ikiwamo waalimu wa shule hizo pamoja na wasimamizi wa mitihani na kuahidi kuwa sheria itafuata mkondo wake.
Baadhi ya shule zilizoingia katika kadhia ya kufutiwa matokeo zimekua zikifanya vizuri kitaifa kwenye matokeo ya darasa la saba.
Mathalani, takwimu za msingi za Tanzania (BEST-2016/2017) zinaonyesha kuwa shule ya Alliance iliingia kwenye orodha ya shule 10 bora kwa mwaka 2015 na 2017 ambapo shule ya Fountain of Joy iliingia 10 bora mwaka 2016.
Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2018 mtihani ulifanyika Septemba 5 na 6 na jumla ya wanafunzi 960,202 walisajiliwa kufanya mtihani huo kwenye shule za msingi 16,845 Tanzania bara.
Serikali yachukua hatua kali
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema watu wote waliohusika katika udanganyifu wa mitihani ya darasa la saba watachukuliwa hatua kali kwasababu wizara iliamua kufanya uchunguzi ili kuwabaini wote waliohusika na udanganyifu huo.
Kutokana na hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Elimu, Tixon Nzunda amesema Serikali imetengua uteuzi wa Maafisa Elimu waliohusika na udanganyifu katika Halmashauri za Wilaya ya Nchemba na Kondoa. Pia waratibu elimu kata na walimu wakuu wameshimamishwa kazi ili kupisha mamlaka kuchukua hatua stahiki.
–