Tanzania yatajwa kwenye nchi 10 za mwisho duniani matumizi ya Tehama

October 26, 2018 7:09 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Mfumo thabiti wa teknolojia ya habari na mawasiliano ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa. Picha|CPA Canada.


  • Imeshika nafasi ya 135 katika ya nchi 140 zilizofanyiwa utafiti na Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF).
  • Imebainika kuwa matumizi ya mtandao wa intaneti kwa njia ya simu nchini bado ni ya kiwango cha chini licha ya kuwa na watumiaji wa intaneti milioni 23.
  • Kasi ndogo ya intaneti, utekelezaji wa sera na sheria usioridhisha bado ni kikwazo kwa ukuaji wa sekta ya tehama.
  • Serikali imesema inajidhatiti kuongeza ubunifu na mafunzo ili kupata wataalam wengi wa sekta

Dar es Salaam. Ripoti mpya ya utafiti wa Ushindani Duniani imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kwa kasi ndogo ya matumizi ya teknolojia ya habari na mawasilino (TEHAMA) jambo linalofanya ishindwe kutumia ipasavyo fursa zitokanazo na sekta hiyo katika kuleta maendeleo.

Ripoti hiyo kwa Kiingereza ‘Global Competitiveness Index 2018’ iliyotolewa na Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) juma lililopita imeiweka Tanzania katika nafasi ya 135 katika ya nchi 140 zilizofanyiwa utafiti huo. Mwaka 2017, Tanzania ilishika nafasi 122 kati ya nchi 137 zilizofanyiwa utafiti.

Mbali na kushuka katika kipengele hicho cha matumizi ya Tehama (ICT adoption), ripoti hiyo imebainisha kuwa kiujumla Tanzania pia imeshuka kwa nafasi mbili katika ushindani wa kibiashara hadi nafasi ya 116 kutoka 114 mwaka jana.

Nchi zingine ambazo zimeshika mkia katika kuchamkia fursa ya matumizi ya Tehama ni Burundi, Liberia, Guinea, Ethiopia. Congo DRC, Cameroon, Benin na Chad ambayo imekuwa ya mwisho.

Utafiti huo uliofanyika katika nchi 140 duniani kati ya Januari na Aprili mwaka huu ulihoji watu 16,658 huku kati yao 90 wakitoka Tanzania. Katika utafiti huo, watafiti walikuwa wakihoji mwenendo wa sekta za kiuchumi katika nchi zao kwa kutumia viashiria mbalimbali ikiwemo ujuzi, ubunifu, rasilimali watu na Tehama.

Katika kupima uwezo wa nchi kutumia Tehama, utafiti huo umeangazia idadi ya watu wanaomiliki simu za mkononi ukilinganisha na idadi ya watu waliopo katika nchi husika ambapo Tanzania imeshika nafasi ya 128 kwa wananchi wake kumiliki simu duniani.

Pia imebainika kuwa matumizi ya mtandao wa intaneti kwa njia ya simu nchini bado ni ya kiwango cha chini ikilinganishwa na nchi za Afrika Mashariki kama Kenya na Uganda, jambo linalowanyima wananchi fursa ya kunufaika na taarifa za maendeleo zinazopatikana mtandaoni. 

Ripoti hiyo inadai kuwa licha ya kuwepo kwa vyanzo mbalimbali vya upatikanaji wa mtandao bado kasi ya intaneti inayotumiwa na taasisi na mashirika (Fixed-broadband Internet subscriptions ) kwajili ya shughuli za kiofisi ni ndogo. 

Hii ikiwa na maana kuwa taarifa zinazopakuliwa mtandaoni huchukua muda mrefu kumfikia mtumiaji jambo linalochelewesha utendaji katika taasisi zinazotegemea teknolojia ya kisasa kama nyenzo ya kurahishisha utoaji wa huduma na bidhaa.


Zinazohusiana: 


Lakini matumizi ya intaneti iliyounganishwa kwa nyaya (Fibre Internet subscriptions) bado yako chini ambapo Tanzania iko nafasi ya 114. Kwa kawaida intaneti hii humuhakikishia mtumiaji kupata muunganiko wa taarifa ukilinganisha na aina nyingine ya intaneti ambayo hutegemea zaidi utendaji wa mtandao na mawaimbi ya mawasiliano ya simu. 

Ripoti hiyo ambayo hutolewa kila mwaka, inabainisha kuwa bado matumizi ya mtandao wa intaneti miongoni mwa wananchi wa kawaida sio ya kuridhisha ambapo Tanzania iko katika nafasi ya 129 kwa viwango vya chini vya wananchi wake kutumia intaneti, licha ya ongezeko la watu wanaotumia simu za mkononi.

Hata hivyo, Ripoti ya Mawasiliano ya robo ya pili ya mwaka 2018 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania  (TCRA) inaonyesha kuwa watumiaji wa simu za mkononi wamefikia milioni 41.4. Watumiaji wa intaneti, kwa mujibu wa TCRA, walifikia milioni 23 mwaka jana sawa na asilimia 45 ya wanaofikiwa na huduma hiyo. 

Uwezo mdogo wa Tanzania kutumia miundombinu ya Tehama kama nyenzo muhimu ya maendeleo hautofautiani na nchi zingine za Afrika. Katika ushindani wa mabara, Afrika inashika nafasi ya mwisho kwa kupata alama 29 ukilinganisha na mabara mengine ya Ulaya na Amerika Kusini.

Katika maeneo mengine ya ushindani ambayo Tanzania imefanya vibaya ni pamoja na mfumo wa uvumbuzi, ubunifu na ujuzi kwa watu wake licha ya juhudi mbalimbali za Serikali na wadau wa maendeleo kuanzisha programu na vituo wezeshi vya teknolojia kwa wajasiriamali (Teck hubs).

Pamoja na changamoto zilizopo katika sekta ya Tehama, bado inafanya vyema katika ukuaji wa uchumi ambapo iko katika nafasi ya 86 duniani kwa viwango vizuri vya ukuaji wa pato la mwananchi mmoja mmoja na Taifa. 

Hiyo inatokana kuwa miongoni mwa nchi sita ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi duniani  kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika miundombinu ya barabara, reli, majengo marefu na sekta ya utalii. 

Utafiti wa Ushindani Duniani pia uliangazia sekta muhimu kama miundombinu, taasisi za utendaji, soko la bidhaa na ajira, mfumo wa fedha, ukubwa soko, mabadiliko ya kibiashara na uwezo wa uvumbuzi wa kila nchi ili kuwasaidia watunga sera na wawekezaji kutambua maeneo muhimu ya kushughulikia changamoto za maendeleo endelevu ulimwenguni.

Ripoti ya Ushindani Duniani imesanifiwa kuwasaidia watunga sera, viongozi wa biashara na wadau wengine duniani kote kuweka sawa mikakati ya kiuchumi katika kipindi hiki cha nne cha mapinduzi  ya viwanda,” Klaus Schwab, Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa WEF.  

Watafiti Steve Esselaar na Lishan Adam katika kuangazia mfumo wa teknolojia Tanzania, wamebaini kuwa baadhi ya sera na sheria, gharama za intaneti, ukosefu wa ujuzi na ubunifu zimekuwa kikwazo katika maendeleo ya Tehama nchini.

Mkurugenzi wa Tehama wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mulembwa Munaku amesema Serikali inaimarisha mfumo wake teknolojia kuhakikisha watumishi wanapata mafunzo ya utendaji wa mifumo mbalimbali ya mawasiliano ili kuendana na mabadiliko ya dunia. 

“Kwa sababu ya mchango mkubwa wa sekta ya tehama katika kukuza uchumi duniani, tunahitaji jitihada za pamoja za wadau wote kutoa mafunzo ya vitendo ili kuendana na mabadiliko ya dunia,” amenukuliwa Munaku na vyombo vya habari katika Mkutano Mkuu wa Tehama nchini unaomalizika leo jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Serikali iko katika mchakato wa kuwatambua na kuwasajili wataalam wote wa tehama nchini ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya ubora wa kimataifa na kuisaidia kuwa na teknolojia endelevu.

Enable Notifications OK No thanks