Benki ya dunia yaridhia kutoa mkopo wa zaidi ya 600 bilioni: Ikulu

November 16, 2018 10:25 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Habari za kutolewa mkopo huo zimetolewa leo baada ya Rais Magufuli kukutana na kigogo wa juu wa benki hiyo barani Afrika.
  • Rais Magufuli amesema mazungumzo aliyofanya leo ni uthibitisho kuwa “Benki ya Dunia haitatuacha”.
  • Awali benki hiyo yenye makao yake makuu, Washington Dc nchini Marekani, ilieleza kuwa mkopo huo umesitishwa kutokana na kutoridhishwa na sera ya kuzuia wanafunzi wajawazito kurudi shule.  

Dar es salaam. Serikali imesema Benki ya Dunia imeridhia kutoa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 300 Milioni (zaidi ya Sh680 bilioni) kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini ikiwa ni siku chache tu tangu benki hiyo iripotiwe kusitisha mkopo huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo “kutoridhishiwa na sera ya kuzuia wanafunzi wanajawazito kurudi shule”.

Taarifa za kutolewa kwa mkopo huo zimetolewa leo (Novemba 16 ,2018)) na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu baada ya Rais John Magufuli kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa rais wa benki hiyo Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem.

Mkopo huo unakusudia kuongeza ubora wa elimu kwa kujenga vyumba vya madarasa, maabara, mabweni na nyumba za watumishi na vifaa vya kufundishia. 

Katika mkutano huo na Rais, Dk Ghanem amesema wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi.

Rais John Magufuli akiwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem Ikulu jijini walipofanya mazungumzo yao. Kushoto ni Mwakilishi wa benki hiyo nchini, Bella Bird. Picha| Ikulu.

Dk Hafez amempongeza pia Rais Magufuli kwa matokeo mazuri ya mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za kijamii.

Rais Magufuli ameishukuru benki hiyo kwa ushirikiano mzuri na Tanzania na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kukuza uhusiano huo na kumhakikishia fedha zote zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitatumika kama iliyokusudiwa .

“Namshukuru Dk Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, hizo Dola 300 milioni ambazo baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali amesema zitaletwa. Pia, Benki ya Dunia imetoa Dola Bilioni 5.2 ambazo zinafadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji ni miradi mikubwa na mingi,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;

“Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha.”


Soma zaidi: 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James ametaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kuwa ni mradi wa uboreshaji wa  Bandari ya Dar es Salaam ambao ujenzi wake umefikia asilimia 24 na ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo jiji Dar es salam.

Miradi mingine ni ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya kwanza na ya pili na miradi mingine mbalimbali.

Katika taarifa za hivi karibuni zilizochapishwa na Mashirika ya habari ya kimataifa ikiwemo CNN ni kwamba Benki ya Dunia iliamua kusitisha mkopo huo muhimu katika sekta ya elimu kutokana na kutoridhishwa kwake na sera ya Serikali kuwazuia wanafunzi wajawazito kwenda shule.

Enable Notifications OK No thanks