Mbinu zitakazowasaidia wahudumu kuvuta wateja wengi mgahawani

November 23, 2018 3:12 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link
  • Lakini mhudumu unapaswa kujua kuwa mteja mmoja ndio atakuletea wengine na kama ukimjibu vibaya basi unaweza kupoteza wateja wengi zaidi.
  • Lakini wachambuzi wa masuala ya biashara wanasema mhudumu mzuri ni yule anayemhudumia mteja kwa unyenyekevu na kuheshimu muda wa mteja wake vizuri. 
  • Hakikisha unaongea kwa lugha ya upole ili usivute watu wengine kuja kuangalia kinachoendelea, hata kama mteja anaongea kwa nguvu jaribu kushusha sauti yako. 

Dar es Salaam. Ukiwa mfanyabiashara au mfanyakazi suala la kula katika mgahawa nyakati za usiku au mchana ni la kawaida sana, lakini kumekuwa na tabia ya wauzaji wa chakula mgahawani kuwazoe wateja wao, jambo linaloathiri utoaji wa huduma husika.

Unakuta mteja amekuja kununua chakula mhudumu hana habari naye zaidi ya kumuangalia tu, mpaka amuite dada naomba kitu fulani. Hii inaonyesha picha ya kwamba una dharau au hujui majukumu yako.

Lakini wachambuzi wa masuala ya biashara wanasema mhudumu mzuri ni yule anayemhudumia mteja kwa unyenyekevu na kuheshimu muda wa mteja wake vizuri. 

Kumbuka kuwa ukitoa huduma mbaya kwa mteja mmoja unaharibu soko, kwasababu wanatabia ya kuambiana juu ya huduma inayotolewa sehemu fulani.

Utafiti toka mtandao unaujihusisha na masuala ya biashara wa Oracle juu ya uzoefu wa wateja, unaeleza kuwa wateja wanaacha kutumia brand (bidhaa) fulani kwasababu ya kuwa na huduma mbaya na kutokuwa na lugha nzuri kwa wateja.

Kama ilivyozoeleka muda wa kula chakula cha mchana,  wafanyakazi  huwa wanatoka kwa wakati mmoja hapo unahitaji kuwa na lugha nzuri na uchangamke katika utoaji huduma maana kuchelewa kwako kunaweza kukufukuzia wateja.

Unyenyekevu kwa mteja ni nguzo muhimu katika kuwavutia wateja wengi zaidi. Picha| Mtandao.

Biashara sio uchawi bali ni ujuzi wa mtu pamoja na lugha nzuri kwa mteja sasa jaribu mbinu hizi uone wateja watakavyokuwa na upendo na biashara yako.

Hatua muhimu za kuchukua

Fanya vitu vizuri tangu mwanzo yaani vile mteja anaingia katika mgahawa wako tu, mkaribishe kwa tabasamu na kwa heshima, angalia nani wa kwanza kumhudumia na muulize kwa ukarimu, kumbuka kusikiliza oda kwa umakini ili umletee mtaje anachokihitaji. 

Usisubiri mteja hadi akwambie niletee bili ya kulipa yaani unatakiwa uhakikishe unamtajia bei na unaweka mazingira safi, maana unaenda mgahawani mteja ndiyo anamwita mhudumu afute meza au ampe bili, hii inawafukuza wateja kwasababu wanaona haujali.

Usimsubirishe mteja kwa muda mrefu yaani kama chakula kitachelewa mwambie ukweli kwamba kitakuwa tayari baada ya muda fulani, au kushauriana nae kuwa kwa hiki ulichoagiza inapaswa uwe mvumilivu kutokana na kuwa na oda nyingi. Hii itamfanya mteja ajione amepewa heshima na umejali muda wake.


Zinazohusiana: Acha kuwaza kuwa mfanyabiashara, anza kufanya biashara

                            Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara


Kuwa mtu wa kutatua changamoto kwa haraka bila kuathiri heshima au hadhi ya mteja wako, mfano umemletea mteja chakula akaanza kulalamika juu ya chakula kutokuiva vizuri, au kutokuwa katika hali ya usafi. Badala ya kununa, mjibu vizuri.

Unatakiwa umjibu kwa kuomba ladhi na kuahidi kuwa mtafanya mabadiliko au kama kuna haja ya kubadilisha chakula au kinywaji mbadilishie.

Hakikisha unaongea kwa lugha ya upole ili usivute watu wengine kuja kuangalia kinachoendelea, hata kama mteja anaongea kwa nguvu jaribu kushusha sauti yako. 

                Muhimu kujali wateja wanapokuwa wanahitaji huduma za mtandao wapatie kwa nafasi. Picha|Mtandao

Lakini mhudumu unapaswa kujua kuwa mteja mmoja ndiye atakuletea wengine na kama ukimjibu vibaya basi unaweza kupoteza wateja wengi zaidi.

Tumia njia ya kumfanya mteja awe huru kutoa maoni yake juu ya huduma zenu ili muweze kuboresha zaidi. Hapa unaweza kuwa unamuuliza vipi chakula kimekuwaje, au ukaweka kadi za kutoa maoni au kuuliza ungependa nini kiboreshwe ili mteja akwambie uweze kujirekebisha au kuongeza ubora zaidi wa kazi yako

Lakini wengi wa wafanyabiashara hawapendi kuambiwa ukweli kuhusu huduma zao lakini ukiuliza unaweza kupewa majibu mazuri yatakayo kujenga na kukuza biashara yako. 

Si kila mtu anayekwambia ukweli au kukukosoa hakupendi bali wanafanya hivyo kwa manufaa yako, hivyo wahudumu wa migahawa inabidi muwe wapole katika kupokea maoni ya wateja wenu.

Enable Notifications OK No thanks