Namna unavyoweza kupata wazo la kuanzisha biashara

March 1, 2019 10:04 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Tafuta ujuzi kukamilisha unachopenda kufanya, nunua haki ya umiliki wa mfumo au jina la biashara kutoa huduma au kusambaza bidhaa.
  • Jifunze kutatua matatizo katika jamii yako na kukubali kujichanganya na watu wenye uwezo na ujuzi unaolingana na mipango yako.

Kuanzisha biashara inayojiendesha vema siyo kazi rahisi kutokana na mchakato ambao mwanzilishi unatakiwa kupitia. 

Huenda wewe ni kijana mbunifu ambaye una matamanio ya kuwa na biashara yako mwenyewe lakini licha ya kuwa umeehudhuria makusanyiko mengi ya kuanzisha biashara ‘startups’ na mikutano ya kuuza mawazo za kibiashara lakini bado hujapata wazo halisi kukuwezesha kuwa na kampuni. Na hujui ufanye nini kufikia ndoto zako?

Kama bado hujakata tamaa katika kuzifikia ndoto zako, basi jaribu njia hizi kupata wazo la kibiashara litakalojenga msingi wa kuianzisha. Nafahamu kuna wengi wameandika masuala haya lakini pia hapa unaweza kujifunza vitu ambavyo vinaweza kukufanya milionea wa kesho kupita mambo yafuatayo. 

Tafuta ujuzi wenye faida

Tafuta kitu unachopenda na unaweza kukifanya vizuri ambacho unaamini kinaweza kukamilisha ndoto zako. Hapa naamanisha tafuta kusudi lako. Mfano, unapenda kuchora picha basi anza kutengeneza mazingira ya kupata ujuzi na maarifa ya jinsi ya kuwa mtu mahiri wa uchoraji. 

Mhamasishaji wa mitandao ya kijamii na mmiliki wa kampuni ya Losers to Legends ya nchini Marekani, Sania Khiljee anaeleza kuwa maarifa utakayoyapata yatakuwa yanaibua uwezo ulionao, kuunoa zaidi na kukukamilisha hata kufikia hatua ya kuwa wazo kamili la biashara unaloweza kuliendeleza kwa kuanzisha startup. 

“Maarifa unaweza kuyapata kwenye vitabu, mtandaoni, kwenda shule, kusoma kosoma kozi za eneo unalotaka kubobea na hata kumtafuta mwalimu atakayekusimamia kwa unachofanya,” anaeleza Khiljee katika moja ya makala zake katika mtandao wa Quora.


Soma zaidi:


Nunua umiliki, wazo

Khiljee anaeleza zaidi kuwa siyo kila biashara anatakiwa uanzie chini. Unaweza ukanunua haki (franchise) ya kutumia jina la mfumo au biashara ya mtu kutoa huduma au kuuza bidhaa kwa kipindi fulani na makubaliano ya kugawana faida. 

Umiliki una faida kwa mtoaji na mpokeaji kwa sababu wote wawili wanachangia mafanikio ya biashara na mchango wanaoutoa katika shughuli husika. 

Tatua tatizo

Pale watu wanapoona tatizo, wewe unatakiwa kutumia kama fursa ya kuitafuta suluhu ambayo ndiyo itakuwa biashara yako. Kaa chini na tafakari katika jamii inayokuzunguka unaona chochote kinachohitaji suluhisho? Ni huduma au bidhaa unayoweza kuuza kuwaondolea changamoto zinazowakabili. Watu watakulipa ikiwa matatizo yao yatatatuliwa.

Umiza kichwa kutafuta suluhisho kwa kila tatizo unaloliona itakusaidia kuona fursa mbalimbali za kuanzisha startup.

Kukutana na watu wenye mitazamo tofauti ni fursa ya kupata maarifa na ujuzi kukusaidia kuanzisha biashara. Picha| Daniel Samson.

Jichanganye

Kwa lugha nyingine fanya ‘networking’. Kutana na watu mbalimbali wenye mawazo yanayolingana na unachopenda kufanya. Mnaweza kuingia ubia na kushirikiana kutumia ujuzi wenu kuanzisha biashara na baadaye kampuni kubwa itakayoajiri watu wengi. 

Mtaalamu wa programu za kompyuta na Mjasiriamali wa teknolojia, John EId anasema katika kujichanganya na watu, utafahamu kwa undani kipi kinafanya kazi na kisichofanya kazi. Watu wanapataje mafanikio na wanatumia njia zipi kuyafikia?

Mchakato huo utakusaidia pia kuepuka makosa waliyofanya wenzako waliokutangulia na kupita katika njia sahihi ya mafanikio.

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa zipo njia nyingi zinazoweza kukusaidia kupata wazo la kuanzisha startup. Ni vema kujaribu njia zitakazojenga msingi imara wa biashara yako kukua. Jifunze kila siku ili upate maarifa yatakayoifanya biashara yako kuwa bora.

Enable Notifications OK No thanks