Mabadiliko makubwa vigogo wa jeshi la polisi

March 1, 2019 9:29 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mabadiliko hayo ya teuzi mpya, kupandishwa vyeo na kuhamishwa vituo vya kazi yametangazwa leo na IGP Simon Sirro jijini Dar es Salaam.
  • Rais John Magufuli awateua makamishna wapya wa polisi huku wengine wakihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani.
  • Makamanda watano wapya nao wateuliwa kuongoza mikoa ya Ruvuma, Temeke, Ilala, Arusha na Njombe.
  • Mabadiliko hayo pia yamegusa idara na kamisheni za jeshi hilo.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limefanya mabadiliko ya kiuongozi, baada ya Rais John Magufuli kufanya uteuzi na kuwapandisha vyeo baadhi maofisa wa polisi kuwa makamishna na kuwahamisha wengine vituo vya kazi. 

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro aliyetangaza mabadiliko hayo leo (Machi 1, 2019) jijini Dar es Salaam amewataja makamishna walioteuliwa na Rais Magufuli kuwa ni Charles Mkumbo ambaye anakwenda kuongoza kamisheni ya intelijensia na Liberatus Sabas ambaye anakuwa mkuu wa operesheni na mafunzo. 

Amewataja makamishna wengine kuwa ni Leonard Lwabuzala ambaye ataongoza kamisheni ya fedha na lojistiki na Benedicto Wakulyamba ambaye anakuwa mkuu wa kamisheni ya utawala na menejimenti ya utumishi.

Naibu Kamishna wa polisi, Shaaban Mlai Hiki amepandishwa cheo na kuteuliwa kuongoza kamisheni ya maabara ya uchunguzi wa kisayansi.

Katika hatua nyingine, Sirro amefanya mabadiliko kwa maofisa wa jeshi hilo ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renata Mzinga amerudishwa Makao Makuu. Hadi uteuzi wa leo Mzinga alikuwa akishughulikia visa vya mauaji wa watoto katika mkoa huo vilivyoripotiwa siku za hivi karibuni. 

James Mushi ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma anaenda kuongoza Chuo cha Polisi (CCP) Moshi. 


Soma zaidi: Polisi kumsaka Mo Dewji nje ya Tanzania


Sirro amewataja makamanda wapya wa mikoa walioteuliwa na Rais kuwa ni Amon Kakwale anakuwa RPC wa mkoa wa kipolisi Temeke, Marwa Mahiga (RPC Ruvuma) na Jonathan Shana anakwenda kuwa RPC wa Arusha.

Wengine ni Salum Hamduni  anakuwa RPC wa mkoa wa Njombe na Zuberi Chembela anakwenda kuwa RPC mkoa wa kipolisi Ilala. 

Viongozi waliohamishwa vituo vyao vya kazi ni pamoja na Benedict Mapugila aliyeteuliwa kuongoza kikosi cha Bandari wakati Michael Marwa anapelekwa makao makuu Zanzibar.  Albert Nyamhanga na Nsato Marijani wanakwenda Idara ya Wakimbizi iliyopo Wizara ya Mambo ya Ndani.

Simon Haule ambaye alikuwa RPC wa Shinyanga anarudishwa Makao Makuu na Yusuph Sarungi ambaye alikuwa RPC Songwe anakuwa mkuu wa kitengo cha kushughulikia wizi wa mifugo (SPU).

IGP Sirro amesema makamishna walioteuliwa na Rais Magufuli wataapishwa tarehe itakayopangwa makao makuu ya jeshi hilo.

Haya ni moja ya mabadiliko makubwa ndani ya polisi yaliyofanywa siku za hivi karibuni hususan yanayohusu maofisa wa juu wa jeshi hilo. 

Enable Notifications OK No thanks