Magufuli amteua Prof Kabudi wizara ya mambo ya nje

March 3, 2019 5:18 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Prof Palamagamba Kabudi akizungumza bungeni. Kiongozi huyo ameteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Picha| Mtandao.

  • Ni baada ya Rais John Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri leo hii (Machi 3, 2019).
  • Kabla ya uteuzi huo Prof Kabudi alikuwa ni Waziri wa Katiba na Sheria, nafasi iliyochukuliwa na Dk Augustine Mahiga.

Dar es Salaam. Katika muendelezo wa kuimarisha safu ya baraza lake la mawaziri Rais  Dk John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya baraza hilo baada ya kumteua Prof Palamagamba Kabudi (63) kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Prof Kabudi anachukua nafasi ya Balozi Dk Augustine Mahiga (73) ambaye ameteuliwa leo Machi 3, 2019 kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Kiufupi mabadiliko yaliyofanywa leo na Rais Magufuli ni ya kuwabadilisha wizara viongozi hao.

Haya ni mabadiliko madogo ya pili kufanywa na Rais Magufuli ndani ya kipindi cha miezi miwili baada ya kumteua Dotto Biteko kuwa Waziri wa Madini huku akimpeleka Angellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji mapema Januari 9 mwaka huu.

Dk Mahiga, ambaye ni miongoni mwa wanadiplomasia mahiri nchini, aliiongoza wizara ya mambo ya nje kwa miaka zaidi ya mitatu sasa akiwa ni miongoni mwa mawaziri wachache katika Serikali ya Dk Magufuli ambaye amepona kubadilishwa wizara au kufutwa kazi katika nusu ya muhula ya awamu ya tano.

Dk Mahiga amekuwa akimwakilisha Rais Magufuli katika mikutano mbalimbali ya kikanda na ya kimataifa sanjari na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.


Zinazohusiana: 


Ukiachana na Dk Mahiga, Prof Kabudi yeye aliingia katika baraza la mawaziri mapema mwaka 2017 baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na baadaye Waziri wa Katiba na Sheria.

Prof Kabudi alichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Harrison Mwakyembe ambaye alihamishwa wizara na kwenda kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo baada ya Nape Nnauye kufutwa kazi na Rais Magufuli Machi 2017.

Licha ya Prof Kabudi kuwa katika wizara inayoshughulikia katiba na sheria amekuwa akipewa majukumu mbalimbali ya kitaifa ikiwemo kujadiliana na wawekezaji katika migogoro mbalimbali inayohusisha Serikali ikiwemo sakata la kampuni ya madini ya Acacia ambapo aliongoza jopo la Serikali katika majadiliano na kampuni ya Barrick Gold.

Majadiliano mengine makubwa aliyoyaongoza na kufikia suluhu siku za hivi karibuni ni yale yaliyohusu utata wa umiliki katika kampuni ya simu ya Airtel ambapo Bharti Airtel wamekubali kuiongezea hisa Serikali hadi kufikia asilimia 49 kutoka asilimia 41 za awali.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa mawaziri hao wataapishwa kesho (Machi 4, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, haijawekwa bayana sababu za Rais Magufuli kufanya mabadiliko hayo madogo yakiwa ni ya pili kufanywa ndani ya miezi miwili.

Enable Notifications OK No thanks