Maoni mchanganyiko Serikali kupiga marufuku mabasi yasiyo na leseni kusafirisha vifurushi

March 6, 2019 11:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi yao wamesema hatua hiyo itasaidia kurasimisha biashara na kutoa fursa kwa kampuni za umma na binafsi kujipatia wateja wengi. 
  • Wengine wamesema itawaumiza wananchi wanaosafirisha vifurushi kutokana na gharama kubwa na muda unaotumiwa na kampuni kufikisha kifurushi sehemu husika. 

Dar es Salaam. Kufuatia uamuzi wa Serikali kupiga marufuku mabasi yote ya abiria kusafirisha vifurushi vya aina yoyote zikiwemo barua bila kuwa na leseni, wadau wa usafiri wamekuwa na hisia tofauti huku wengine wakisema itasaidia kuifanya biashara hiyo kuwa rasmi na wengine wakieleza kuwa itaibua changamoto ya muda na kupanda kwa bei ya kusafirisha vifurushi hivyo. 

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema wamiliki wa magari wanaruhusiwa tu kusafirisha vifurushi  hivyo ikiwa wamepata leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kinyume na hapo wanakiuka sheria na taratibu za nchi.

Mhandisi Nditiye ametoa agizo hilo mjini Musoma mkoani Mara wakati akizungumza na watumishi wa taasisi mbalimbali ambazo ziko chini ya wizara hiyo ikiwemo kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) na Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Katika mkutano huo, ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kuendesha oparesheni ya kukagua mabasi hayo kama yana leseni na kuwasilisha orodha ya mabasi TCRA ili kuangalia kwenye kanzi data yao kama mabasi hayo yamekidhi vigezo vya kufanya biashara hiyo.

Agizo hilo la Serikali limepokelewa kwa hisia tofauti na wasafirishaji ambao wamekuwa wakisafirisha vifurushi ambapo baadhi yao wanaona hatua hiyo ni nzuri kwa sababu inaifanya biashara hiyo kuwa rasmi kuliko ilivyo sasa bila kufuata taratibu za usafirishaji. 

Ili mtoaji huduma wa basi apate leseni ya kusafirisha vifurushi kutoka mji mmoja hadi mwingine anatakiwa kulipa ada ya Sh798,000 kwa mwaka. Picha| Mtandao.

“Uamuzi wa waziri ni mzuri kwa maana ya kurasimisha hii biashara ya usafirishaji mizigo midogo (parcels) maana sheria/taratibu haziruhusu kwa njia hizi za mabasi pasipo urasimishaji,” amesema Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Muhunda Resources Limited, Gerald Nyerere. 

Nyerere, ambaye ni mdau wa usafiri nchini, amesema kama sheria na taratibu zitazingatiwa utawezesha biashara hiyo kuwa rasmi jambo litakalosaidia pande zote kunufaika kupitia mfumo imara unaohakikisha kunakuwa na usalama wa virufurushi vinavyotumwa.

Amebainisha kuwa uamuzi huo wa Serikali utakuwa ni fursa kwa kampuni za umma na binafsi zinazosafirisha vifurushi kujipatia wateja wengi zaidi na kuwaumiza wamiliki wa mabasi ambao hawana leseni. 

“Mbadala wa huduma hizi in ‘terms of affordability’ (unafuu wake) imekuwa ni kupitia njia hizi za mabasi japo utaratibu wake hivi karibuni umekuwa wa kiholela,” amesema Nyerere. 

Hata hivyo, Nyerere amebainisha kuwa kampuni hizo zinapaswa kuboreshwa huduma ikiwemo kupunguza gharama za usafirishaji na kuangalia namna ya kuhimiza matumizi ya anuani rasmi za makazi ikizingatiwa kuwa maeneo mengi ya Tanzania yamejengwa bila kuzingatia kanuni za mipango miji. 

“Wenye masanduku ya barua (postal address) ni wachache na gharama za huduma zisizohitaji anuani au sanduku la barua, huduma kama EMS, FedEx na DHL kwa ujumla ni kubwa,” amesema.

Uchunguzi mdogo uliofanywa na Nukta umebaini kuwa gharama ya kutuma bahasha kutoka Mbeya  hadi Dar es Salaam kwa njia ya basi ni kati ya Sh5,000 hadi 10,000 kulingana na ukubwa wake. Iwapo huduma hiyo ingetolewa na kampuni za huduma za posta kwa kasi ya basi huwa ni wastani wa Sh15,000.


Zinazohusiana: 


Mkazi wa Singida, Raheri Emanuel amesema uamuzi huo unaweza kuwa na matokeo hasi kama wamiliki wa mabasi hawana leseni kwa sababu watoa huduma watakuwa wachache na huenda mizigo ikachelewa kufika maeneo husika. 

Emanuel, ambaye amekuwa akitumia mabasi kwa muda mrefu kusafirisha vifurushi, amesema mzigo unaotumwa na basi unamfikia mhusika siku hiyo hiyo kwa gharama nafuu ukilinganisha na kampuni zingine ambazo hutumia siku moja hadi tatu kumfikishia mteja kwa sababu ya mchakato mrefu kidogo kufuata sheria na taratibu za usafirishaji. 

“Wananchi watapata tabu sana kutuma mizigo siyo kila mikoa kuna yale magari ya kusafirisha mizigo (cargo transportation) kwa sababu usafirishaji wa mabasi ni nafuu sana na wa haraka,” amesema Emanuel.

Anafikiri Serikali ijipe muda na kuhakikisha inaboresha mfumo wa usafirishaji hasa kuyawezesha makampuni ya umma kuboresha huduma zake ili kuwaondolea usumbufu wananchi ambao wamekuwa wakitegemea mabasi. 

Mwongozo wa kupata leseni ya kusafirisha vifurushi (Postal licensing procedures) zilizotolewa na TCRA mwaka 2015, unaeleza kuwa ili mtoaji huduma wa basi apate leseni ya kusafirisha vifurushi kutoka mji mmoja hadi mwingine anatakiwa kulipa ada ya Sh400,000 kwa mwaka.

Enable Notifications OK No thanks