Kutana na Aneth David mwanasayansi anayechipukia Tanzania
- Kwa sasa anafanya utafiti wa kina wa viumbe vidogo vidogo kwenye udongo utakaosaidia kuongeza tija katika sekta ya kilimo nchini.
- Ni mmoja ya wanawake ambao wanahitajika katika kuhakikisha wanakuwa mifano kwa kizazi cha sasa juu ya dhana ya ugumu wa masomo ya sayansi.
Dar es Salaam. Imekuwa ikiaminika kuwa watoto wa kike wengi wanaogopa masomo ya sayansi na kukukimbilia kuchagua masomo ya biashara au sanaa kwa kuwa ndiyo rahisi kuyasoma na hata baadaye kutoka kimaisha.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba kuna wanawake wamefanya mengi katika ugunduzi wa vitu mbalimbali duniani baada ya kusoma vema na kuipenda sayansi. Wao na sayansi, sayansi na wao tangu wakiwa wadogo na wanafanya vizuri hadi sasa kuliko hata wanaume.
Miongoni mwao ni binti wa Kitanzania, Aneth David (29), Mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi Shahada ya Uzamivu (PhD) aliyejikita kufanya utafiti wa namna viumbe vidogo vidogo vilivyo kwenye udongo (soil microorganisms vinavyoweza kuongeza uzalishaji kwenye sekta ya kilimo nchini.
Utafiti wake unajaribu kuelewa uhusiano kati ya viumbe hivyo na mfumo wa kilimo wa sukuma-vuta. Mfumo huu unatumiwa na wakulima wa mashariki na kusini mwa Afrika kupambana na visumbufu vya ‘stem borers’ na magugu aina ya kiduha ambayo husumbua mazao ya nafaka hasa mahindi na mtama.
“Matokeo ya utafiti huu yanaweza kutumiwa kuboresha mfumo wa sukuma-vuta kuupa tija zaidi na kuongeza uzalishaji wa mazao husika,” amesema Aneth.
Kwa mfumo wa elimu nchini na umri wake huenda ukapata maswali mengi likiwemo kama alisoma nje kutokana na mafanikio yake ya haraka ya kitaaluma.
Imekuaje binti wa miaka 29 akafika ngazi hiyo kubwa ya kitaaluma hususan katika masuala ya sayansi ambayo yametawaliwa na wanaume tu?
“Nimesoma elimu yangu ya msingi na sekondari mkoani Kilimanjaro na shahada yangu ya kwanza na umahiri nimesomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” Aneth ameiambia Nukta katika mahojiano ya hivi karibuni.
Binti huyo alisoma Shule ya Sekondari ya Mawenzi kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na Shule ya Sekondari ya Majengo katika elimu ya kidato cha tano hadi sita.
Ile dhana ya kuwa tatizo ni ubora hafifu wa shule nchini ndiyo sababu ya wasichana hawasomi sayansi kwa haifanyi kazi. Sayansi kwake ni wito wa ndani wa mtu unaoweza kumpeleka mbali kama akiamua kuamini katika ndoto zake.
Zinazohusiana:
- Uongozi, ardhi kuwatoa kimaisha wanawake vijijini
- Esther Mndeme: Muongozaji aliyewashangaza wengi tuzo za filamu 2019
- Rahma Bajun: Mjasiriamali anayetamba kimataifa
Aneth anasema kuwa kwa sasa mambo yanabadilika na anaona wanawake wanaingia katika sekta mbalimbali za sayansi lakini bado ni wachache kutokana na tatizo linaloanzia mbali tangu mashuleni ambapo wanafunzi wa kike kwenye baadhi ya kozi za sayansi sio wengi.
“Bado nguvu inahitajika sana kwenye kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi na kuendelea na ajira kwenye sayansi,” amesema.
Mbali na kuendelea na utafiti wake unaolenga kuchagiza uzalishaji wa mazao nchini, Aneth ni mdau mkubwa wa masuala ya usawa wa kijinsia na amekuwa akitumia muda wake wa ziada kuandaa na kushiriki katika makongamano mbalimbali yenye lengo ya kumwinua mtoto wa kike hasa katika sekta ya elimu kwenye mambo ya sayansi na teknolojia.
Sayansi na teknolojia ni chachu ya maendeleo kwa sasa ulimwenguni na kampuni kubwa zaidi duniani ni zile zinajihusisha katika sekta hizo kama Microsoft, Facebook, Amazon, Novartis na Pfizer.
Anaamini katika kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuleta matokeo chanya katika jamii, na mara nyingi hutumia muda wake kushirikiana na wadau kama Buni Innovation Hub ili waweze kufikia malengo ya kuwainua watoto wa kike katika sayansi.
Aneth ni mmoja wa mabinti wa mfano katika wanasayansi wachanga ambao wanapenda watoto wa kike wasome masomo ya sayansi. Picha| Kwa hisani ya Aneth David.
Licha ya kuwa hasikiki kama walivyo baadhi ya wanawake nchini, Aneth amewahi kupata tuzo ya balozi wa sayansi ambayo hutolewa na Jukwaa la Next Einsteins Forum (NEF). Jukwaa hilo linakuwakutanisha Wanasayansi na wadau mbalimbali duniani ili kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili Afrika na maeneo mengine ulimwenguni.
Ushindi huo ulimfungulia milango mingi zaidi ndani na kumpa uwanja mpana wa kuchangia katika kuleta mabadiliko kwenye sayansi na teknolojia Tanzania na Afrika kwa ujumla.
“Sio lazima wote tuwe wahandisi au wahadhiri au watafiti, wanasayansi wanahitajika kwenye kila eneo kwa sasa nchini na duniani kote,” amesema David.
Amewazaje kumudu vyote hivyo kwa pamoja?
Hata hivyo, kutokana na umri wake na vitu anavyofanya Aneth amesema kuwa kitu kikubwa anachofanya ni kupanga ratiba yake ili usiingiliane na muda wa kufanya utafiti ambao ameanza tangu mwaka 2016.
“Najipangia malengo ya kila wiki, mwezi, robo mwaka na mwaka, supervisors (wasimamizi) wangu wa PhD wanasaidia sana kuhakikisha ratiba ya shule inaenda na muda wangu haumezwi na mambo mengine ya nje,” amesema David.
Kwenye masomo ya sayansi, kwa mujibu wa Aneth, kuna fursa nyingi na maeneo mengi ya kushiriki ambayo kila mtu anaweza kupata nafasi kama kwenye mambo ya tiba, lishe, viwanda ,Tehama na mengineyo ni swala la kuchagua nini kinakufaa na kukifanyia kazi.
Ujumbe wake kwa watoto wa kike waliopo mashuleni ni kuwa watafute mifano hai ya wanasayansi wanawake ili wapate kuwa chachu kwa maendeleo yao na kujifunza kutoka kwao.