Taxify yaja kivingine, yabadili jina sasa kuitwa Bolt

March 7, 2019 9:45 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mabadiliko hayo yamefanyika leo ikiwa ni hatua ya kuongeza wigo wa utoaji huduma ikiwemo matumizi ya pikipiki ndogo zinazoendeshwa kwa umeme.
  • Mabadiliko hayo pia yanalenga kuongeza ushindani kwa kampuni nyingine kama Uber katika soko la usafiri mtandaoni.

Kampuni ya Taxify inayotoa huduma za uchukuzi duniani kwa watumiaji kuomba taxi kwa kutumia programu tumishi ya simu (App), imebadilisha jina na sasa inaitwa Bolt ikiwa ni hatua ya kujiimarisha na kutanua wigo wa kutoa huduma ikiwemo pikipiki ndogo zinazoendeshwa kwa umeme (electric scooter).

Mabadiliko hayo  yanaenda sambamba na kutumia nembo mpya ili kuongeza ushindani kwa kampuni nyingine kama Uber ambazo nazo zinatoa huduma ya mtandaoni za magari, bodaboda na bajaj. 

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bolt zamani Taxify, Markus Villig aliyekuwa akitangaza mabadiliko hayo leo (Machi 7, 2019) amesema App yao sasa ina muonekano mpya ambapo wanaamini kuwa sekta ya usafiri inapitia mageuzi makubwa ya kutumia umeme kama nishati ya vyombo vya moto na wao wameanza kuendana na wakati. 

“Taxify ilianzishwa miaka mitano iliyopita kwa malengo ya kurahishisha upatikanaji wa usafiri maeneo ya mjini. Bidhaa yetu ya kwanza ilikuwa ni kutoa suluhisho la taxi ambalo lilitoa jina kwa kampuni,” amesema Villig. 

Kampuni hiyo ina watumiaji 25 milioni katika nchi 30 duniani ambapo mabadiliko hayo pia yanalenga kuongeza mtaji wa kuendesha kampuni hiyo. Mei 2018 ilifanikiwa kupata ufadhili wa Dola za Marekani 175 milioni kutoka kwa kampuni ya Daimler, kampuni mama ya Mercedes-Benz na kufikisha mtaji wa Dola 1 bilioni. 


Soma zaidi: Mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Taxify


Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo imeeleza kuwa watumiaji wa App ya Taxify wakiwemo wa Tanzania hawatakiwi kufanya jambo lolote kwasababu App hiyo itajiboresha yenyewe na wao watashuhudia mabadiliko hayo makubwa katika viganja vyao. 

Jitihada za kuupata uongozi wa Taxify Tanzania hazikuweza kufanikiwa kuzungumzia mabadiliko hayo ambayo yana maana kubwa kwa huduma za usafiri zinazotolewa hapa nchini.

Bolt imeanza kutoa huduma za kukodisha pikipiki ndogo zinazoendeshwa kwa umeme ikiwa ni hatua ya kuendana na mabadiliko ya dunia ya kuachana na matumizi ya petroli na dizeli. Picha|Mtandao.

Taxify iliyoingia Tanzania Desemba 2017 ni mshindani anaeibukia kwa Uber inayoendesha shughuli zake kwenye zaidi ya miji 600 duniani. Kampuni zote mbili zinafanya jitihada za kuwavutia wateja wengi zaidi ili kuendelea kuwepo kwenye soko la ushindani. 

Uber ambayo imejiimarisha zaidi katika jiji la Dar es Salaam, mwenzake Taxify anajitanua zaidi kutoka katika jiji hilo sasa ameingia Dodoma na Mwanza.

Wakati Tanzania ikiwa na kampuni mbili, Kenya ina kampuni nne zikiwemo za Little na Mondo Ride kutoka Dubai ambazo zimeonyesha nia ya kuingia nchini ili kuongeza ushindani ikizingatiwa kuwa mahitaji ya usafiri na ukuaji wa miji unaongezeka kila siku. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW