Wadau wataka ubunifu wa hali ya juu sekta ya elimu
Washiriki wakifuatilia mdahalo wa Mstakabali wa Elimu ya Tanzania uliofanyika leo katika Wiki ya Ubunifu 2019, jijini Dar es Salaam. Picha|Tulinagwe Malopa.
- Wadau mbalimbali wa teknolojia wameshauri ubunifu wa hali ya juu katika sekta ya elimu ili kuongeza kasi ya maendeleo nchini kupitia Tehama.
- Walimu watakiwa kuvumbua mbinu mpya za kusaidia kufundishia wanafunzi mbali na zile zilizozoeleka.
Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa teknolojia wameshauri ubunifu wa hali ya juu katika sekta ya elimu ili kuongeza kasi ya maendeleo nchini kupitia Tehama.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha uvumbuzi cha Dar Teknohama Business Incubator (DTBI) Dk George Mulamula, aliyekuwa akizungumza katika mkutano uliohusu mustakabali wa elimu katika Wiki ya Ubunifu leo (Machi 29, 2019), amesema elimu ni muhimu kwa kuwa ndio msingi wa kila kitu nchini.
Amesema ni jukumu la walimu na wanataaluma kuvumbua mbinu mpya za kusaidia kufundishia wanafunzi mbali na zile zilizozoeleka.
“Uvumbuaji wa mbinu tofauti za ufundishaji kama matumizi ya ‘animations’ ni muhimu kwa kuwa yanampa mwanafunzi wigo mpana wa kufikiri na kuelewa tofauti na mbinu nyingine tulizozizoea,” amesema.
Mshauri wa masuala ya elimu kutoka Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID), Arianna Zanolini amesema walimu wanajukumu la kujua ni kwa namna gani wanaweza kubadili sekta hii kuwa bora zaidi.
“Walimu wanapaswa kujua ni kwa namna gani wanaweza kuwa chanzo cha ubunifu kwa wanafunzi ambapo itawasaidia hata katika kujifunza,” amesema.
Soma zaidi:
- Mbinu zitakazowasaidia watahiniwa darasa la saba kufanya vizuri.
- Mbinu zinazoweza kuisaidia Temeke kutokomeza sifuri elimu ya sekondari.
- Udanganyifu mitihani darasa la saba kujirudia tena mwaka huu?
Baadhi ya wadau wengine wameeleza kuwa ni vema kuangalia mchakato wa namna sekta husika itakavyoendeshwa kutokana na ukuaji wa ubunifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Smart Lab, Edwin Bruno amesema ni jukumu la kila mbunifu katika sekta husika kufahamu ni kwa namna gani sekta hiyo itaendeshwa.
“Ni muhimu kama mbunifu wa masuala ya elimu kujua ni vitu gani utatumia ili kuhakikisha mambo yanaenda kirahisi kutokana na mfumo ulio rafiki kwa wanafunzi,” amesema.
Pamoja na hayo baadhi ya kampuni zinazochipukia (start-ups) zimeeleza namna ambavyo zinavyochangia kuboresha sekta ya elimu ikiwemo Kasome International iliyounda mfumo wa kumfikia mwanafunzi asieingia darasani kuptia video katika masomo tofauti tofauti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kasome International, Sayi Michael amesema lengo lao lilikua kufikia watoto hata wasioweza kwenda shule kwa sababu ya changamoto mbalimbali ili waweze kutimiza malengo yao.
“Tunataka kutengeneza mfumo ambao vijana wanaweza kuziishi ndoto zao kwa kutumia ubunifu huu,” amesema.