Vodacom Tanzania yamteua Jacques Marais kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji

April 4, 2019 12:28 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Jacques Marais ameteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Vodacom Tanzania.Picha|Mtandao.


  • Alikuwa ni Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni hiyo tangu Julai 1, 2016 na uteuzi umefanyika ili kuhakikisha shughuli za kampuni hiyo zinaendelea kama kawaida.
  • Uteuzi huo unakuja siku moja baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa  kampuni hiyo, Hisham Hendi na wenzake nane kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa ya uhujumu uchumi. 

Dar es Salaam. Ikiwa imepita siku moja tangu Mkurugenzi Mtendaji wa  kampuni ya  Vodacom Tanzania, Hisham Hendi na wenzake nane kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, Jacques Marais ameteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo. 

Kabla ya Marais kuteuliwa katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji alikuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Vodacom Tanzania, nafasi ambayo ameishikilia tangu Julai 2016. 

Uamuzi huo umetangazwa leo (Aprili 4, 2019) na Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania ambapo katika taarifa yake imeeleza kuwa  uteuzi huo ni  kuhakikisha shughuli za kampuni zinaendelea kama kawaida na hakuna muingiliano wowote utakaosimamisha shughuli za utoaji huduma kwa wateja. 

Kufuatia kesi inayowakabili vigogo wa juu wa kampuni hiyo, Bodi imesema imeanzisha uchunguzi wa ndani kuhusiana na tuhuma zinazowakabili watendaji hao na itaendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuzingatia maadili na utawala bora katika uendeshaji wa kampuni.

Washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo jana ( April 3, 2019) wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwamo kuingiza mitambo ya mawasiliano ya kielektroniki bila kuwa na leseni na kuisababishia Serikali hasara ya Sh5.8 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 20/2019 ambayo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. 

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Uendeshaji Biashara katika kampuni ya Inventure Mobile limited, Ahmed Hashim Ngassa; Mtaalam wa Tehama, Brian Keneth Lusiola; Mkuu wa Uhakiki wa Mapato wa Vodacom Tanzania, Joseph Gichuchi Nderitu na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Vodacom Tanzania, Olaf Peter Mumburi. 

Wengine ni Mkuu wa Mauzo wa Vodacom Tanzania, Joseph Muhere na Meneja wa Fedha wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Bonzo. Pia katika kesi hiyo kampuni mbili za Vodacom Tanzania na Inventure Mobile Tanzania Limited (Tala Tanzania) nazo zimejumuishwa katika kesi hiyo.

Baada ya kusomewa tuhuma zinazowakabili, watuhumiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote na wamerudishwa rumande wakati wakisubiri kurudi mahakamani Aprili 17, 2019 kesi hiyo itakapotajwa tena. 


Soma zaidi:


Jacques Marais ni nani?

Kabla ya Marais kuteuliwa katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji alikuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Vodacom Tanzania, nafasi ambayo ameishikilia tangu Julai 2016. 

Kigogo huyo ambaye ni raia wa  alianza kufanya kazi na Vodacom mwaka 2001 kama Meneja wa Fedha katika kampuni ya Vodacom Afrika Kusini ambapo alifanya kazi kwa miaka mitatu kabla ya kuhamishiwa Lesotho akitumikia cheo cha Mkurugenzi wa Fedha hadi mwaka 2007. 

Baada ya hapo alihamishiwa nchini Congo DRC na mwaka 2012 alikwenda Msumbiji ambapo alikuwa kwenye cheo chake alichokishikilia kwa muda mrefu mpaka ilipofika 2016 alipohamishiwa Tanzania. 

Marais ambaye ana uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya fedha, ana Shahada ya kwanza ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini. 

Enable Notifications OK No thanks