CAG: HESLB imeshindwa kuwapata wadaiwa wa Sh1.46 trilioni

April 10, 2019 11:43 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Januari mwaka huu HESL ilisema kuwa ilikusanya Sh94 bilioni kutoka kwa wadaiwa wake ikiwa ni juu zaidi ya lengo la kukusanya Sh71.4 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2018. Picha!Mtandao.


  • Hayo yamebainika katika ripoti  yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 jambo linalopunguza uwezo wake wa kuendelea kuwakopesha wanafunzi wapya na wanaoendelea.
  • Amependekeza Bodi ishirikiane na taasisi nyingine na vyanzo vingine vya taarifa ili kuiongeza nguvu kanzidata yake na kuweza kuwatambua wakopaji ambao haijaweza kuwatambua.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Professa Mussa Juma Assad amesema Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeshindwa kuwapata wakopaji wenye mikopo yenye thamani ya Sh1.46 trilioni jambo linalopunguza uwezo wake wa kuendelea kuwakopesha wanafunzi wapya na wanaoendelea.

Katika ripoti hiyo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 kuhusu mashirika ya umma iliyotolewa leo, Prof Assad amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa sana kwa kuzingatia muongozo wa sheria ya HESLB ambayo inataka bodi hiyo kutengeneza mtandao na kushirikiana na taasisi na mashirika mbalimbali ili kuwatambua wadaiwa wa mikopo iliyotolewa.

“Kuwa na mikopo mikubwa ambayo wafaidika wameshindwa kupatikana kunapunguza uwezo wa bodi wa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea,” amesema Prof Assad katika ripoti hiyo.

“Ninapendekeza Bodi ishirikiane na taasisi nyingine na vyanzo vingine vya taarifa ili kuiongeza nguvu kanzidata yake na kuweza kuwatambua wakopaji ambao haijaweza kuwatambua,” ameongeza.

Mikopo ya HESLB ni miongoni mwa fedha muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa elimu ya juu nchini hasa kwa wanafunzi ambao familia zao haziwezi kumudu gharama za matibabu.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, urejeshwaji wa mikopo umekumbana na changamoto lukuki ikiwemo sehemu kubwa ya wakopaji kutowasilisha marejesho kwa bodi hiyo ambayo katikati ya Januari mwaka huu ilitangaza kuwa imevuka lengo la ukuasanyaji katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

HESL ilisema kuwa ilikusanya Sh94 bilioni kutoka kwa wadaiwa wake ikiwa ni juu zaidi ya lengo la kukusanya Sh71.4 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2018.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru aliwaambia wanahabari wakati huo kuwa makusanyo hayo yalitoka kwa wanufaika zaidi 198,659 ambao wamejiari au kuajiriwa katika sekta binafsi na umma.

“Katika kipindi hicho cha Julai – Desemba pia tumefanikiwa kuwabaini wanufaika wapya zaidi 12,600 ambao walikua hawajaanza kurejesha mikopo yao na sasa wameanza na hivyo kufanya wateja wanaorejesha kufikia 198,656 hivi sasa,” alisema Badru.

Enable Notifications OK No thanks