Unywaji kahawa bado unasuasua kwa watanzania

April 23, 2019 5:04 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Unywaji wa kahawa una faida nyingi kwa afya ya mwanadamu ikiwemo kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya ini na saratani lakini inapswa kutumika kwa kiasi ili kuepuka madhara ya unywaji uliopitiliza. Picha|Mtandao.


  • Licha ya kuwa na viwanda vya kuongeza thamani hadi kupata kahawa ya mezani, unywaji wa kinywaji hicho uko chini ya asilimia 10.
  • Sababu ya unywaji mdogo ni soko la mnada wa pamoja wa kahawa kumilikiwa na makampuni machache ya nje ambayo hununua kiasi kikubwa na kusafirisha katika nchi zilizoendelea. 
  • Mikakati iliyopo ni kuongeza kiwango cha unywaji hadi kufikia asilimia 15 baada ya miaka 10. 

Dar es Salaam. Licha ya Tanzania kuwa nchi yenye viwanda vya kuongeza thamani hadi kupata kahawa ya mezani, bado unywaji wa kahawa upo chini kwa wastani wa asilimia tano hadi saba, jambo linaloleta changamoto ya wakulima kufaidika na soko la ndani. 

Unywaji wa kahawa una faida nyingi kwa afya ya mwanadamu ikiwemo kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya ini na saratani lakini inapswa kutumika kwa kiasi ili kuepuka madhara ya unywaji uliopitiliza.

Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Sekta ya Kahawa Tanzania  iliyotolewa Aprili 2019 na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) inaeleza kuwa sababu kuu zinazosababisha hali hiyo ni soko la mnada wa pamoja wa kahawa kumilikiwa na makampuni machache ya nje ambayo hununua kiasi kikubwa na kusafirisha katika nchi zilizoendelea. 

Muamko mdogo wa watu kunywa kahawa inayotengenezwa viwandani nayo ni changamoto nyingine inayokwamisha ukuaji wa sekta nhiyo nchini, licha ukweli kuwa baadhi ya wanywaji hutumia kahawa iliyotengenezwa kienyeji. 

Baadhi ya viwanda vinavyochakata na kuongeza thamani ya kahawa ni pamoja na Mbinga Coffee Curing limited na  Dan and Associates Enterprises Ltd (DAE Ltd) vya mkoani Ruvuma. Vingine ni kiwanda cha kusindika kahawa cha  Tanica na Bukop vya mkoani Kagera  na Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika (TCCCO) kilichopo Kilimanjaro.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa kuyumba kwa uzalishaji na ubora kunaathiri bei ya mkulima na  kuongezeka kwa kiasi cha kahawa kinachopelekwa mnadani kwa wakati mmoja kunachangia soko la ndani kutopata mwamko wa aina yake.

“Vyama vya wakulima vina utegemezi mkubwa kwa makampuni binafsi kutoa huduma za ugani na uendeshaji mitambo, licha ya juhudi za Serikali kuwezesha wakulima CPU, mashine nyingi hazifanyi kazi,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Watumiaji wa wakubwa wa kahawa ya Tanzania ni pamoja na Japani kwa asilimia 27, Ujerumani (17%), Ubelgiji (12%) na Italia (10%) huku masoko mpya ambayo yameanza kufikiwa ni pamoja na India, Urusi, Afrika Kusini, Australia na China. 


Soma zaidi:


Mikakati ya kuongeza unywaji wa kahawa

Hata hivyo, TCB imesema katika ripoti hiyo kuwa imejipanga kuongeza kiasi cha unywaji wa kahawa hadi kufikia asilimia 15 baada ya miaka 10 ambapo kazi kubwa itakuwa kupunguza utegemezi wa masoko ya nje na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya ndani. 

Viwanda vitakavyojengwa vitajikita zaidi kuchakata na kuongeza thamani ya zao hilo ili kuzalisha zaidi kinywaji cha kahawa ili watanzania wafaidike na faida zake. 

Lakini kuimarisha kampeni za uhamasishaji wa unywaji wa kahawa katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuongeza ukubwa wa soko la ndani litakalochochea uzalishaji na mnyororo wa thamani wa zao hilo ikiwemo kuongeza ajira kwa wananchi na mapato serikalini. 

Enable Notifications OK No thanks