Rais Magufuli: Nitaongeza mishahara kabla sijaondoka madarakani
- Hajaweka wazi ni lini atatekeleza ahadi hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wafanyakazi kutolewa tamko.
- Asema wawe wavumilivu kwa sababu sasa anajenga uchumi wa nchi na fedha zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
- Tucta walia na kodi isiyolingana kwa vima vya mishahara na kuondolewa kazini wafanyakazi wenye elimu ya darasa la saba.
- Waziri Mhagama ataka meza ya majadiliano kumaliza migogoro ya wafanyakazi.
Dar es Salaam. Matumaini ya wafanyakazi ya kusikia habari njema leo za kuongezewa mishahara mwaka huu yameota mbawa baada ya Rais Dk John Magufuli kusema atatekeleza ahadi hiyo kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi mwaka 2020.
Hata hivyo, hajaweka bayana ni lini ahadi hiyo itaitekeleza ikizingatiwa kuwa amebakiza takribani mwaka mmoja na nusu tu wa kuwepo madarakani katika awamu ya kwanza ya utawala wake kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo yamefanyika kitaifa katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya leo (Mei 1, 2019), amesema ni kweli alitoa ahadi ya kuongeza mishahara mwaka jana katika sherehe za Mei Mosi lakini atatekeleza ahadi hiyo wakati wowote kabla hajaondoka madarakani.
“Katibu Mkuu wa Tucta (Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania) amenikumbusha kuhusu ahadi yangu niliyoitoa mwaka jana wakati sherehe kama hizi zilifanyika Iringa kwamba kabla sijaondoka madarakani nitaongeza mshahara. Hilo ni kweli kabisa! Nilitoa ahadi hiyo lakini ni lazima tuelewe hadi sasa sijaondoka madarakani,” amesema Rais Magufuli.
Amesema angeweza kuongeza mishahara lakini ni lazima kwanza nchi ijenge uchumi imara ili zipatikane pesa za kuwalipa wafanyakazi na kujenga miradi ya maendeleo itakayosaidia kutengeneza ajira nyingi zaidi.
“Ndugu zangu tuvumilie tu sikutaka kuwadanganya kuwa nimewaongezea mishahara halafu fedha mtakazozipata hazipo, ninyi endeleeni kuvumilia tupo katika muelekeo mzuri,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliyeambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali katika sherehe hizo akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema ongezeko la mishahara linategemea gharama za uendeshaji wa Serikali ambapo kila mwezi Sh580 bilioni hutumika kulipa mishahara ya wafanyakazi huku fedha zinazobaki hulipa madeni na kuelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Akizungumzia suala la kodi ya mishahara ambalo lilikuwa linasubiriwa na wafanyakazi kutolewa tamko, amesema wanaendelea na majadiliano na mamlaka husika kuangalia namna ya kupunguza kodi hiyo ambayo kwa sasa ni asilimia tisa kwa watumishi wa kima cha chini.
Lakini amebainisha kuwa Serikali ina sababu za msingi kutofautisha kodi kulingana na madaraja ya mishahara.
Muonekano wa juu wa viwanja vya Sokoine jijini Mbeya wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi ambayo yalihudhuriwa na Rais John Magufuli na viongozi wengine wa Serikali. Picha|Michuzi.
Kupandisha madaraja na madai ya wafanyakazi
Wakati matumaini ya kusikia habari njema ya kuongezewa mishahara leo yakiota mbawa, Rais Magufuli ameahidi kuwa katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 watumishi 193,166 wa umma watapandishwa vyeo wakiwemo walimu.
“Tangu Novemba 2015 tumewapandisha madaraja au vyeo watumishi 118,989 kwa gharama Sh29.5 bilioni ambapo waalimu ni 75,502 ambao wamelipwa Sh12.3 bilioni na watumishi wasio waalimu ni 43,487 ambao wamelipwa Sh13.2 bilioni,” amesema Rais Magufuli.
Kuhusu madai ya wafanyakazi, amebainisha kuwa wamelipa madai yasiyo ya mishahara yenye thamani Sh291.3 bilioni, mengi ya madai hayo yalikuwepo kwa zaidi ya miaka 10 baada ya kuyaakiki.
Hata hivyo, amemuagiza Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri mkuu Kazi, Ajira, Vijana, Wazee na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kuhakikisha bodi ya mishahara inakutana kushughulikia changamoto za wafanyakazi ikiwemo kupanga viwango vya mishahara kulingana na mahitaji ya sekta husika.
Sherehe hizo zimeandaliwa na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) ambapo kauli mbiu ya Mei Mosi ya mwaka huu wa 2019 ni “Tanzania ya Uchumi wa Kati Inawezekana, Wakati wa Mishahara na Masilahi Bora kwa Wafanyakazi ni sasa!”
Soma zaidi:
- Wafanyakazi wengi hawajui haki zao: Ripoti
- Maswali manne yanayosubiri majibu sherehe za Mei Mosi 2019
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Katibu Mkuu wa Tucta, Dk Yahaya Msigwa ameiomba Serikali kutatua changamoto mbalimbali za wafanyakazi ikiwemo kupanga viwango vya kodi vinavyolingana kwa vima vyote vya mishahara na kiwezesha bodi ya mishahara kutimiza majukumu yake kikamilifu.
“Tunaishauri Serikali iwezeshe bodi za mishahara kukutana na kufanya utafiti utakaowezesha kupanga viwango halisi vya vima vya mishahara ambavyo vitakidhi mahitaji kwa sekta zote ya umma na sekta binafsi,” amesema Dk Msigwa.
Pia ameiomba Serikali kuhakikisha waajiriwa wote wenye elimu ya darasa la saba walioajiriwa kwa kufuata taratibu ambao waliondolewa kazini wakati wa zoezi la uhakiki warudishwe kazini na walipwe haki zao za kiajira kwa sababu wamebaini kuwa baadhi ya wafanyakazi hao hawajarudishwa kazini.
Lakini ameishauri Serikali itilie mkazo katika uchumi wa bahari ambao umezinufaisha nchi nyingi duniani kwa kuongeza meli za mizigo zilizosajiliwa Tanzania ili kuongeza ajira kwa mabaharia na mapato ya Serikali.
Dk Msigwa ambaye alikuwa akisoma risala kwa niaba ya wafanyakazi nchini, amesema njia nyingine ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi ni Serikali kutumia fursa ya utalii kuongeza mapato na kujifunza kutoka katika nchi zinazotegemea utalii kukuza uchumi wa wananchi wao.
Kwa upande wake, Waziri Mhagama amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyakazi na kuendelea kutumia meza ya majadiliano kama nyenzo muhimu ya kupunguza migogoro mahala pa kazi.