Mtwara inavyotikisa matokeo ya kidato cha sita

May 4, 2019 6:19 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Mwaka 2018 mkoa huo ulishika nafasi ya kwanza kitaifa ambapo wanafunzi wake wote walifaulu kwa asilimia 100.
  • Hakuna hata mwanafunzi mmoja aliyepata daraja sifuri
  • Historia ya miaka minne inaonyesha  mkoa huo umekuwa ukifanya vizuri.

Dar es Salaam. Huitaji kutumia nguvu kumweleza mtu maajabu ya Mkoa wa Mtwara katika sekta ya elimu lakini matokeo yake ya kidato cha sita mwaka 2018 ni kielelezo tosha cha maajabu hayo.

Mkoa wa Mtwara ulifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa kati ya mikoa 29 nchini iliyoshiriki katika mtihani huo huku wa wanafunzi wake wakifaulu kwa viwango vya juu. 

Kwa mujibu wa Mpangilio wa Mikoa kwa Ubora wa Ufaulu katika mtihani wa kidato cha sita (ACSEE) uliotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) mwaka jana unaonyesha kuwa wanafunzi wa mkoa huo walifaulu kwa asilimia 100. 

Uchambuzi wa matokeo hayo uliofanywa na www.nukta.co.tz umebaini kuwa wanafunzi wote 1,499 waliofanya mtihani huo kutoka katika shule 11 walifaulu kwa kupata kati ya daraja la I hadi IV na hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepata daraja sifuri. 

Kwa mujibu wa viwango vya ufaulu vya Necta wanafunzi wanaopata daraja la I hadi la IV wanahesabika wamefaulu na wana sifa ya kupata cheti na kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Wanafunzi waliopata daraja la II walikuwa asilimia 56.5 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani au sawa na kusema kwa kila wanafunzi 10 waliofanya mtihani huo 6 walipata daraja la II. 

Lakini wanafunzi hao hawakutaka kabisa kulisogelea daraja la IV ambapo ni wanafunzi 11 tu sawa na asilimia 0.7 walitumbukia katika daraja hilo. 

Matokeo hayo ni ya kubahatisha?

Historia ya elimu ya Mtwara kwa miaka minne iliyopita yaani kuanzia 2015 hadi 2018 katika matokeo ya kidato cha sita imekuwa nzuri, jambo linalothibitisha kuwa uongozi na wanafunzi wa mkoa huo wamejipanga vizuri kuhakikisha kila mwaka wanatoboa katika mitihani hiyo.  

Katika mpangilio wa ufaulu kimkoa, bado inafanya vizuri. Mfano mwaka 2017 ilishika nafasi ya tatu kitaifa kabla ya kupanda hadi katika nafasi ya kwanza mwaka jana. 

Hata katika mpangilio wa ufaulu wa madaraja ya watahiniwa bado Mtwara inatikisa katika mitihani ya kidato cha sita ukilinganisha na mitihani ya kidato cha nne, pili na darasa la saba ambako haionyeshi cheche zake.

Mathalani, matokeo ya Necta katika kipindi hicho cha miaka minne iliyopita yanaonyesha kuwa ni wanafunzi 14 ndiyo walipata daraja sifuri huku wanafunzi 162 wakipata daraja la nne. 

Lakini mafanikio ya Mtwara yanachangiwa zaidi na shule tatu za Tandahimba, Aquinas na shule ya Wasichana ya Nangwanda. Katika kipindi hicho, hakuna hata mwanafunzi mmoja wa shule hizo aliyewahi kupata daraja la nne au sifuri.

Haya ni matokeo makubwa kwa mkoa huo ambayo yanaashiria mwanga mzuri kwa watoto kuelemika na kufika katika ngazi ya juu ya elimu ya chuo kikuu.

Maandalizi mazuri kupitia mitihani ya majaribio nayo ni sababu nyingine inayowabeba wanafunzi ambapo walimu hupata nafasi ya kurekebisha makosa yao mapema kabla ya mitihani ya mwisho. Picha|Mtandao.

Sababu ya matokeo hayo mazuri 

Mkuu wa mkoa wa Mtwara , Gelasius Byakanwa ameimbia www.nukta.co.tz  kuwa sababu ya kufanya vizuri kwa wanafunzi wa mkoa huo katika matokeo ya kidato cha sita mwaka jana ni jitihada za wanafunzi na walimu katika ufuatiliaji  na uongozi mzima wa mkoa huo.

Amesema mazingira mazuri ya kusomea na kufundishia katika shule za kidato cha tano na sita za mkoa huo  pamoja na kujitambua kwa wanafunzi kumesaidia mkoa kufanya vizuri kitaifa.

“Shule zetu nyingi zipo pembezoni mwa mjini hivyo kufanya wanafunzi kuwa na mazingira mazuri ya kusomea na kuepuka vishawishi,”amesema Byakanwa.


Zinazohusiana:


Maandalizi mazuri kabla ya mtihani kupitia mitihani ya majaribio nayo ni sababu nyingine inayowabeba wanafunzi ambapo walimu hupata nafasi ya kurekebisha makosa yao mapema kabla ya mitihani ya mwisho. 

“Kupitia maandalizi hayo yanasaidia kuwabaini wanafunzi na kuasaidia ili waweze kufanya vizuri kutoka mwenye sifuri ili aweze kwenda daraja la nne au zaidi na la nne kwenda madaraja mengine ya juu,”amesema Byakanwa.

Hata hivyo, amebainisha kuwa wamejiandaa vyema kuendeleza ushindi wao katika mtihani wa mwaka huu unaotarajiwa kuanza Mei 6. 

Ni imani yake kuwa mwaka huu watafanya vizuri zaidi katika mitihani hiyo inayowapa fursa wanafunzi kujiunga na elimu ya juu kwa fani mbalimbali.

Enable Notifications OK No thanks