Hakutakuwa na uhaba wa mifuko mbadala baada ya Juni Mosi: Wawekezaji
Uzalishaji wa mifuko mbadala utaibua viwanda vingi vya nyumbani kwa sababu teknolojia yake ni rahisi na ipo ya aina nyingi kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje jambo likalosaidia katika ukuaji wa uchumi. Picha|Mtandao.
Umoja wa wazalishaji wa mifuko mbadala umesema umejipanga kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
- Wamesema malighafi za karatasi na vitambaa laini vinapatikana katika viwanda vya ndani.
- Mifuko hiyo itafungua fursa za ajira na ukuaji wa viwanda nchinii.
Dar es Salaam. Umoja wa Wazalishaji wa Mifuko Mbadala nchini umejipanga umesema umejipanga vyema kuzalisha mifuko mingi itakayokidhi mahitaji ya Watanzania mara baada ya marufuku ya mifuko ya plastiki kuanza Juni Mosi mwaka huu kutokana na kuwepo kwa malighafi na vitendea kazi vya kutosha.
Mwakilishi wa Umoja huo, Allan Ngumbuke aliyekuwa akizungumza leo (Mei 22, 2019) jijini Dar es Salaam kuhusu mipango na mikakati ya umoja huo katika uzalishaji wa mifuko mbadala, amesema watahakikisha kuwa baada ya Juni 1 wanasambaza mifuko hiyo katika maeneo mbalimbali ili kuziba pengo la mifuko ya plastiki ambayo matumizi yake yanafika ukingoni.
Amesema wanafanya kila jitihada za kutafuta malighafi na kuagiza mashine mpya ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa mifuko hiyo inayotajwa kuwa rafiki kwa mazingira.
“Baada ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki, wazalishaji wa mifuko mbadala wameongeza kasi ya uzalishaji na wengi wameshaagiza mashine zipo njiani kuja na nyingine zinatengeneza mifuko mbadala, mfano hai ni Tanpak Tissue Paper Ltd, Hanpal, Green Earth Paper Products Ltd na Harsho Group,” amesema Ngumbuke.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo wadau na wananchi wanaotaka kuwekeza kwenye mifuko mbadala wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwa kuwa malighafi zipo zikiwemo za karatasi zinazopatikana katika viwanda vya Mufindi Paper Mills Ltd na Tanpak Tissue Ltd.
Soma zaidi:
- Makamba awatahadharisha wafanyabiashara wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki
- Kanuni za kuzuia mifuko ya plastiki zakamilika
- Serikali kudhibiti mifuko ya plastiki kwa awageni wanaoingia Tanzania
Kwa upande wa malighafi ya vitambaa laini zitapatikana katika cha kiwanda cha Harsho Group kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Amebainisha kuwa uzalishaji wa mifuko mbadala utaibua viwanda vingi vya nyumbani kwa sababu teknolojia yake ni rahisi na ipo ya aina nyingi kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje jambo likalosaidia katika ukuaji wa uchumi.
Katika kuhakikisha mifuko hiyo inapata soko la uhakika, amesema wanashirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa Watanzania kuona mifuko hiyo kama fursa muhimu ya kujiajiri na kutunza mazingira.
“Tunaomba Shirika la Viwanda Vidogovidogo Nchini (SIDO) waweke kipaumbele na viatamizi vya uzalishaji wa mifuko mbadala kwa kuwa SIDO ipo nchi nzima na ni mahiri kwa kutoa mafunzo ili washiriki wake walete matokeo chanya na makubwa kwa haraka zaidi,” amesema Ngumbuke.
Mifuko hiyo siyo tu inafungua fursa za ajira, bali inaweza kutumika katika shughuli za utalii kwa kuiwekea urembo na michoro ya kitamaduni ili kuitangaza Tanzania kimataifa.
Kwa upande wake, Afisa Tawala wa Kiwanda cha Tanpak Tissue Ltd, Michael Mjungu amesema kiwanda chake kimejipanga kikamilifu kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa mifuko hiyo na kuwataka wafanyabiashara kuondoa hofu kuhusu uwezo wa viwanda vya ndani ya Tanzania kuweza kuzalisha mifuko mbadala.