Kujiunga mafunzo ya JKT siyo ajira: Mwinyi

May 28, 2019 1:04 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi. Picha| Mtandao.


  • Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwapatia vijana stadi za kazi na maisha ili waweze kujiajiri wenyewe.
  • Amebainisha kuwa vyombo vya dola haviwezi kuajiri vijana wote wanaohitimu. 
  • Amewashauri waangalie fursa katika sekta binafsi.

Dar es Salaam. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ameeleza kuwa vijana wanapaswa kufahamu kuwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) siyo ajira bali ni sehemu ya kupata mafunzo ya kijeshi na stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe.

Dk Mwinyi amesema hayo leo (Mei 28, 2019) bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa viti maalum (CCM), Angelina Malembeka aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwaajiri vijana wanaohitimu mafunzo ya JKT kwa kuzingatia jinsia ambapo wanaohitimu wengi ni wanaume. 

“Nataka ieleweke kwamba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa lazima vijana waelewe kwamba siyo ajira. Kujiunga JKT ni kwenda kupata mafunzo ya kijeshi pamoja na stadi za kazi, wachache watapata ajira katika vyombo vya usalama, walio wengi itabidi wajiajiri wenyewe au waajiriwe na sekta binafsi,” amesema Dk Mwinyi. 

Amesema kila mwaka takriban vijana 20,000 hujiunga na mafunzo ya JKT lakini ni wachache wanapata fursa ya kuajiriwa na vyombo vya usalama kwa sababu havina uwezo wa kuwachukua wote.


Zinazohusiana: 


Amebainisha kuwa vijana wanaojiunga na JKT wafahamu wazi wanaenda kupata stadi muhimu za kazi zitakazowasaidia kujiajiri ili kujikimu kimaisha ambapo amewataka waondokane na mawazo kuwa wakipata mafunzo hayo lazima waajiriwe na Serikali. 

“Vyombo vya ulinzi na usalama havina uwezo wa kuchukua wote hao katika ajira. Watapata wachache na walio wengi watakuwa wamepata stadi za kazi waweze kujiajiri,” amesisitiza.

Katika swali lake, Malembeka amedai kuwa kuna manung’uniko mengi yanayotokana na vijana kujitolewa kwa muda mrefu katika jeshi hilo lakini hawapati ajira na hata wanaopata mafunzo, wengi ni wanaume na wanawake wanaachwa nyuma.

Waziri Mwinyi amesema kinachofanya kusiwe na uwiano mzuri wa wanaoiingia JKT ni kuwa wasichana walio wengi hawajitokezi kuchangamkia fursa za mafunzo hayo. Hata wanaojitokeza wanakosa sifa muhimu wakati wa usaili. 

Enable Notifications OK No thanks