Hakuna mkulima wa korosho atakayedhulumiwa haki yake: Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Picha|Mtandao.
- Amesema wakulima wote waliouza korosho kwa Serikali watalipwa fedha zao.
- Baada ya Serikali kumaliza uhakiki majina yao yatapelekwa katika benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya malipo.
Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia wakulima wa korosho ambao bado hawajalipwa kuwa Serikali italipa fedha hizo ambazo ni zaidi ya bilioni 20 mwaka huu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Juni 1, 2019) katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Lindi, ambapo amesema wakulima wote wakiwemo wa mkoa wa Lindi watalipwa pesa zao.
“Wakulima wote wanaodai malipo yao ya korosho watalipwa katika mwaka huu wa fedha kwa kuwa ni haki yao na kwamba Serikali haitodhulumu haki ya mkulima yeyote,” amesema Majaliwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, wakulima ambao bado hawajalipwa au malipo hayajakamilika baada ya Serikali kumaliza uhakiki majina yao yatapelekwa katika benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya malipo.
Zinazohusiana:
- Namna tani zaidi ya 200,000 za korosho zitakavyonunuliwa na Serikali
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage joto la korosho likipanda
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema zoezi la malipo ya fedha za korosho zilizohakikiwa linaendelea, ambapo hadi Mei 31 mwaka huu takribani kilo 52 milioni zenye thamani ya Sh171.6 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 87.6 zimeshalipwa kwa wakulima husika.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kiasi cha Sh23.4 bilioni bado hazijalipwa kwa wakulima wa korosho wa mkoa wa Lindi. Korosho hizo zilihakikiwa katika kituo cha Mtwara.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wabunge wa mkoa wa Lindi, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa pamoja na Wakuu wa Idara.