Serikali kuja na njia mpya kulinda maslahi ya madereva wa mabasi, malori Julai 1

June 26, 2019 7:55 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Huenda mpango huo ukasaidia kuboresha hali za madereva na kusaidia kupunguza ajali za barabarani kwa sababu madereva watakuwa wamepata uhakika wa mishahara na posho. Picha|Mtandao.


  • Imesema imeunda mpango mkakati kuhakikisha kila dereva anakuwa na mkataba wa kazi. 
  • Pia utatoa viwango vipya vya posho wanazopaswa kulipwa wanapokuwa safarini. 
  • Wamiliki wa vyombo vya usafiri nao kubanwa zaidi. 

Dar es Salaam. Serikali imesema kuanzia Julai Mosi mwaka huu itaanza kutekeleza mpango mkakati mpya wa ajira za madereva wa malori na mabasi ambao utahakikisha kila dereva anakuwa na mkataba wa kazi unaoainisha mshahara na viwango vya posho anapokuwa safarini. 

Hatua hiyo inakuja baada ya utaratibu wa awali uliokuwa unawataka wamiliki vya usafiri kuwasilisha mikataba ya wafanyakazi wakati wakiomba leseni za magari kushindwa kutekelezwa kikamilifu. 

Leseni za magari zimekuwa zikitolewa na kusimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra). 

Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Anthony Mavunde amesema mpango huo umekamilika na siku mbili zijazo, Serikali itatoa tamko la maelekezo ya hatua gani zitachukuliwa kuanzia Julai 1 mwaka huu. 

“Katika mkakati ambao tumeuweka, kila dereva wa nchi hii atakuwa na mkataba wake na tutahakikisha kila mmiliki wa chombo cha usafiri anafuata masharti ya sheria kama kifungu cha 14 cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini kinavyoelekeza,” amesema Mavunde.  

Mavunde alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka ambaye alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuharakisha utekelezaji wa maboresho ya utoaji wa mikataba ya kazi kwa madereva wa malori na mabasi yaliyofanyika mwaka 2015. 

Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini amesema tayari wamekutana na wadau wote wa usafirishaji ili kuhakikisha mkakati huo unapewa kipaumbele na maslahi ya madereva na wamiliki yanazingatiwa. 

“Si maneno tu, mkakati umeshawekwa kabisa na tumekaa na wenzetu wa Jeshi la Polisi na muda si mrefu mwezi wa saba mtaona cheche za wizara,” amesisitiza Mavunde. 


Zinazohusiana: 


Huenda mpango huo ukasaidia kuboresha hali za madereva na kusaidia kupunguza ajali za barabarani kwa sababu madereva watakuwa wamepata uhakika wa mishahara na posho. 

Kwa mujibu wa Mavunde, Mei 2, 2015 aliyekuwa Waziri Mkuu,  Mizengo Pinda aliunda kamati maalum ya kutatua matatizo katika sekta ya usafirishaji chini ya Katibu Mkuu iliyokuwa Wizara ya Uchukuzi. 

Aidha, katika kipindi hicho, kamati ndogo iliyokuwa chini ya Wizara ya Kazi na Ajira iliundwa kwa ajili ya kushughulikia maslahi na mikataba ya madereva. 

Kamati hiyo kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi, madereva na viongozi wa umoja wa wamiliki wa vyombo vya usafiri nchini waliufanyia marekebisho na kuuboresha mkataba wa ajira wa madereva uliokuwepo awali.

Mkataba ulioboreshwa uliidhinishwa na wadau katika kikao kilichofanyika Mei 23, 2015 na Ilikubalika kuwa mkataba huo uanze kutumika Juli 1, 2015 lakini utekelezaji wake umekua ukisuasua mpaka sasa. 

Enable Notifications OK No thanks