Tanzania, Kenya zinavyochuana katika ujenzi wa bandari kavu

July 16, 2019 9:08 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Tanzania na Kenya zina rasilimali ya bahari inayoziwezesha kuwa na bandari zinazotumika kusafirisha mizigo kimataifa. Picha|Mtandao.


  • Tanzania ina mpango wa kujenga bandari kavu ya Inyala mkoani Mbeya kuhudumia nchi za Kusini mwa Afrika. 
  • Kenya imetoa eneo la Naivasha kwa nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Rwanda kwa ajili ya kujenga bandari kavu. 
  • Bandari hizo zinalenga kukuza biashara katika nchi za Afrika. 

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiwa kwenye mchakato wa kujenga bandari kavu ya  Inyala mkoani Mbeya, Kenya inajipanga kuzipa nchi tatu eneo la kujenga bandari kavu katika mji wa Naivasha ili kuongeza wigo wa biashara katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. 

Bandari ya Inyala itahudumia wafanyabiashara wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kukabiliana na ushindani wa huduma za bandari katika nchi za Zambia, Congo DRC na Malawi zinazotumia reli ya Tazara kusafirisha mizigo. 

Taarifa kutoka Kenya zinaeleza kuwa nchi hiyo ina mpango kutoa ardhi kwa nchi tatu za Rwanda, Congo DRC na Burundi kwa ajili wa ujenzi wa bandari kavu za nchi hizo katika ukanda wa kiuchumi wa Naivasha

Bandari hizo zitaunganishwa na bandari ya Lamu chini ya mradi wa Korido ya Sudan Kusini-Ethiopia ambao unalenga kupanua wigo wa biashara baina ya  Kenya na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki na Kati. 

Tayari Uganda na Sudan Kusini zimepewa eneo katika mji huo ambao utakuwa kituo kikubwa cha utunzaji wa mizigo inayotoka katika bandari za Lamu na Mombasa ambayo imekuwa ikichuana na bandari ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, bado baraza la mawaziri la nchi hiyo halijaridhia kutolewa kwa ardhi hiyo, ikizingatiwa kuwa Uganda umepewa ekari 1,000 huku Sudan ikikabidhiwa ekari 10.


Soma zaidi: 


Katika mgao huo wa ardhi, Tanzania haijahusishwa kwa sababu ina rasilimali kubwa ya bahari na maziwa inayoipa fursa kuwa na bandari nyingi zinazohudumia nchi mbalimbali za Afrika. 

Wakati Kenya ikizigeukia nchi za Afrika Mashariki na Kati, Tanzania nayo inajenga reli ya kisasa ya SGR itakayounganisha bandari ya Dar es Salaan na nchi za Rwanda, Uganda na Burundi. 

Lakini ujenzi wa bandari ya Inyala itakayokuwa inasaidiana na bandari ya Kyela ambayo ipo katika mwambao wa Ziwa Nyasa itaunganishwa na reli ya Tazara ambayo imekuwa ni nyenzo muhimu ya usafirishaji wa mizigo katika nchi za Zambia na Congo DRC. 

Bandari ya Kyela ina jukumu la kusimamia bandari zote zilizopo katika Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania. Miongoni mwa bandari zilizo chini ya Bandari ya Kyela ni; Itungi, Kiwira (wilayani Kyela mkoa Mbeya), Mbamba Bay, Liuli na Ndumbi (wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma) Manda na Lupingu (wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe).

Enable Notifications OK No thanks