Magufuli aagiza zoezi la kuwaachia mahabusi wanaoshikiliwa kimakosa lifanyike nchi nzima
- Amesema hawezi kuongoza watu wanyonge walioonewa.
- Aitaka Wizara ya Katiba na Sheria na DPP kutembelea magereza yote nchini.
- Watuhumiwa watakaobainika kuonewa waachiwe huru.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania DPP) kutembelea mahabusi na magereza katika mikoa yote ya Tanzania ili kubaini na kuwaachilia huru watuhumiwa wa makosa mbalimbali ambao hawajatendewa haki.
Agizo hilo la Rais linakuja baada ya watuhumiwa zaidi ya 70 wakiwemo askari polisi wanane walioshitakiwa kwa usafirishaji wa shehena ya dhahabu kuachiwa huru kutoka katika Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza.
Rais Magufuli amesema baadhi ya watuhumiwa wamepelekwa katika katika magereza mbalimbali kwa kuonewa ambapo DPP na vyombo vya usalama na ulinzi wanapaswa kuzungumza na watuhumiwa ili kubaini wale ambao hawajatendewa haki ili wafutiwe mashtaka na kuachiwa huru.
“Leo watakuwa katika gereza la Kasulamile na Geita. Wakimaliza kule nataka waende kila mkoa ili watu hawa maelfu ambao wako kwenye magereza, mahabusu wakisubiri hatma zao wale ambao wanawekwa mule kwa kuonewa waweze kutolewa,” amesema Rais Magufuli leo katika Wilaya ya Kongwa, mkoa wa Dodoma.
Soma zaidi:
- Rais Magufuli kuzuru Mwanza, Simiyu na Mara kwa siku saba
- Magufuli sasa aangazia rada kuongeza mapato Tanzania
Amesema zoezi hilo limeanza kutekelezwa katika mikoa ya kanda ya ziwa na litafanyika nchi nzima ili wale wasiostahili kukaa mahabusu waachiwe.
“Napenda nimshukuru sana DPP na Wizara ya Sheria, baada ya kutoa hayo maagizo jana walienda Butimba wamekaa na watu hao kwa zaidi ya masaa saba. Jana pale kwenye gereza la Butimba wameachia watu 75 hawana makosa wengine labda angehukumiwa miezi sita lakini kwa sababu hapelekwi mahakamani inakaa miaka minane.
“Na wameachia pale Bariadi watu 100, wameachia watu Bugumu Serengeti watu 52, wameachia Tarime watu sita, wameachia watu 24 Bunda na Kahama watu 43,” amesema Rais.
Wakati akihojiwa na Wanahabari jana, DPP Biswalo Mganga amesema zoezi hilo limezingatia maslahi mapana ya Taifa na linalenga kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa kwenye magereza nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewaomba askari kuacha kuwaonea raia kwa kuwabambikia kesi kwa sababu siyo jambo zuri na wanatakiwa kumuogopa Mungu.
“Siwezi nikatawala nchi ya machozi. Machozi haya yataniumiza. Siwezi nikatawala watu wanaosikitika wako kwenye unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa,” amesema Rais.